Tangazo

January 3, 2012

Rais Kikwete Aiagiza TAWIRI kutafiti sababu za kutoweka kwa Mnyama aina ya Palahala

Rais, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ameiagiza taasisi ya utafiti wa wanyamapori (Tanzania Wildlife Research Institute - TAWIRI-) kutafiti sababu za kutoweka kwa mnyama aina ya Palahala (Roosevelt Sable Antelope) katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani mkoani pwani na maeneo mengine  walikokuwa wakionekana kwa wingi hapo awali.

Rais Kikwete ametoa agizo hilo mwanzoni mwa wiki kwa Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI Dkt. Simon Mduma, baada ya kupokea maelezo ya  Mpango wa Kitaifa wa Kuhifadhi Tembo nchini  (Tanzania  Elephant   Management   Plan), alipokutana na uongozi  wa taasisi hiyo katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara.

Mpango   huo  umeainisha   vipaumbele vinavyohitaji   kutiliwa   maanani katika   kuhifadhi  na   kudhibiti  Tembo   katika   kipindi   cha miaka  mitano ijayo.

Rais aliiagiza TAWIRI kwamba pamoja na kupata chanzo cha kutoweka kwa wanyama hao, pia itafutwe njia ya kuwarejesha tena, akisisitiza kwamba Palahala  ni mnyama anayevutia sana na  anaweza  akawa kivutio cha ziada katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani,  hasa kwa utalii wa upigaji picha.

Palahala ni mnyama anayevutia sana kutokana na umbo lake ambapo wawindaji hupendelea sana kumuwinda ili kupata pembe zake ndefu ambazo hutumika kama mapambo katika nyumba.  Pembe hizo pia hutumika kuchezea ngoma za kiasili.

Rais Kikwete pia ameagiza kufanyike uchunguzi wa kina ili kujua sababu zilizosababisha kupungua kwa kasi kwa idadi ya tembo katika ukanda wa mbuga za wanyama za  Selous na Mikumi, baada ya kustushwa  na ripoti inayoonyesha kwamba zaidi ya tembo 30,000 wametoweka katika kipindi kifupi.

Rais alitoa agizo hilo baada ya Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI. Simon Mduma kutoa takwimu zilizoonyesha  kwamba  katika mbuga za Selous na Mikumi mwaka 2006 kulikuwa na tembo 74,900, na sensa iliyofanyika mwaka 2009 ilionyesha wamesalia 43,552.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

No comments: