Tangazo

January 20, 2012

WAFANYABIASHARA WAONYWA KUACHA KUSAFIRISHA FEDHA BILA YA ULINZI WA POLISI

Shamsi Vuai Nahodha
Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi Zanzibar 
Wafanyabiashara wakiwemo wawekezaji wa kigeni waliopo hapa nchini, wameonywa kuacha mtindo wa kusafirisha fedha nyingi kutoka eneo moja hadi lingine pasipo na ulinzi wa Polisi.

Onyo hilo limetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Shamsi Vuai Nahodha, wakati akizungumza na wawekezaji wenye Mahoteli katika Fukwe za Bahari ya Hindi na Hifadhi ya Mjini Mkongwe mjini Zanzibar.

Waziri Nahodha amesema kuwa pamoja na kuwapo kwa usalama na amani hapa nchini, lakini hali hiyo isiwafanye watu wakajiamini na kusafirisha fedha nyingi pasipo na ulinzi wa kutosha ili kuepuka kuporwa na majambazi.

Akizungumzia Utalii Mh. Nahodha amesema kuwa kwa kutambua kuwa utalii ndio chanzo kikubwa cha uchumi wa Zanzibar na taifa kwa ujumla, Serikali itahakikisha kuwa inaweka miundombinu ya kutosha kiusalama ili kuondoa matishio yoyote kwa wageni wanaoitembelea nchi yetu kwa shughuli mbalimbali zikiwemo za kitalii.

Aidha amesema ili kuhakikisha usalama zaidi, wawekezaji hao hawanabudi kulitumia Jeshi la Polisi katika kufanya uchunguzi kwa watu wanaotaka kazi kwenye maeneo yao ili kuepuka kuajiri watumishi wasio waaminifu.

“Mnapotaka kuwaajiri wafanyakazi, wakiwemo walinzi kwenye maeneo yenu, hakikisheni kuwa mnaowapa nafasi hizo ni vijana wa maeneo jirani ambao wengi wao wanafahamika kwa sura na tabia kulikoni kutoa watumishi mbali ambao hata kama wakifanya uhalifu na kukimbia ni vigumu kumpata”. Alisema Mh. Nahodha.

Mh. Nahodha ameongeza kuwa athari za kumuajiri mtu wa mbali ni kuwa hata pale atakapofanya uhalifu na kukimbi haitakuwa rahiisi kwa Polisi kumpata mtuhumiwa huyo kwa urahisi.

Awali Mwenyekiti wa Umoja wa Wawekezaji wa Mahoteli Visiwani Zanzibar (ZATI) Zanzibar Association Tourism Industrial  Bw. Abullsamad Saidi, alisema kuwa ipo haja kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kusaidia kuongeza kasma ya Jeshi la Polisi Visiwani humo ili waweze kumudu vema kazi zao zikiwemo za ulinzi wa vivutio vya kitelii kwa wageni.

Amesema kuwa pamoja na Jeshi la Polisi kufanya kazi zao vizuri, lakini askari wamekuwa wakipata vikwazo kutokana na uduni na ukosefu wa vitendea kazi kama vile usafiri na radio za mawasiliano.

Hoja hiyo pia imeungwa mkono na Mshauri wa Rais katika Masuala ya Utalii Bw. Issa Ahmed Othman, ambaye amesema kusipokuwa na usalama wa kutosha kwenye maeneo ya fukwe na kuna hatari ya kukosa watalii na hivyo kudhoofisha na kupunguza pato la taifa linalotokana na utalii.

Wakichangia hoja kwenye mkutano huo, baadhi ya wawekezaji waliiomba Serikali kuwa na bajeti ya kutosha katika kulinda maeneo ya vivutio vya kitalii.

No comments: