Tangazo

March 6, 2012

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUFUNGUA MKUTANO MKUU WA MWAKA WA MAAFISA WAANDAMIZI WA JESHI LA POLISI, CHUO CHA POLISI MOSHI, TAREHE 06 MACHI 2012

Rais Jakaya Kikwete
Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi;

Inspekta Generali wa Polisi, Said Ally Mwema;

Mheshimiwa Leonidas Gama, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro;

Makamishna na Manaibu Makamishna wa Jeshi la Polisi;

Maofisa Wakuu wa Jeshi la Polisi;

Wageni waalikwa;

Mabibi na Mabwana;

 

Nakushukuru sana wewe Mheshimiwa Waziri pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kwa kunialika kuja kufungua Mkutano wenu.  Nakupongeza kwa dhati Mkuu wa Jeshi la Polisi na viongozi wenzako kwa kuwa na utaratibu wa kukutana kila mwaka kufanya tathmini ya shughuli zenu.  Huu ni utaratibu mzuri kwa vile kila Kamanda kwa ngazi yake anatoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa sera, mikakati na mipango mbalimbali ihusuyo usalama wa raia na mali zao katika eneo lake la uongozi.

Nathubutu kusema kuwa msingeweza kuwa na utaratibu mwingine mzuri kushinda huu. Matumaini yangu ni kuwa taarifa hizo zinafanya uchambuzi wa kina wa mafanikio yaliyopatikana, kasoro zilizojitokeza na changamoto mlizokabiliana nazo na mnazoendelea kukabiliana nazo.  Aidha, ni matumaini yangu kuwa mjadala unakuwa wa uwazi na ukweli na kwamba hamtaoneana muhali kuambiana ukweli kuhusu kasoro za mwenzenu pale inapostahili.  Ni jambo jema na la kijasiri kujiwekea utaratibu wa kujipima wenyewe.

Mheshimiwa Waziri,

Ndugu Mkuu wa Jeshi la Polisi;

Nimefurahishwa sana na Kauli Mbiu ya mkutano wenu “Usingoje, tumia rasilimali ulizonazo kuongeza ufanisi”. Ni Kauli Mbiu muafaka inayohimiza uwajibikaji na ufanisi wa kazi kwa kuzingatia rasilimali zilizopo. Inatambua hali halisi kwamba utegemee ulichonacho kutimiza majukumu yako. Usisubiri usichokuwa nacho.  Usisubiri ulichoomba au ulichoahidiwa kupata. Nawaomba mkitoka hapa mwende kwenye vituo vyenu vya kazi mkiwa mmebeba ujumbe huu mzito wa Kauli Mbiu. Mwende mkatekeleze maudhui yake kwa vitendo, kwa kushirikiana na maofisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali. Mkifanya hivi, bila shaka mtaweza kukidhi matarajio ya wananchi na hivyo kulinda heshima ya Jeshi letu la Polisi.

Ni ukweli ulio wazi kuwa sote tungetamani muwe na zana na vitendea kazi vilivyo bora, vingi vya kutosheleza mahitaji yetu.  Lakini uwezo wa kifedha uliopo ni mdogo, vitu hivyo unavyovitaka hutavipata vyote kwa wakati mmoj.  Hivyo basi hamna budi kuwa na subira, kupanga vipaumbele vyenu vizuri na hasa kuwa wabunifu ili kwa kutumia vifaa vilivyopo vizuri muweze kutekeleza majukumu yenu kwa kiwango cha kuridhisha.   

Mheshimiwa Waziri;

Ndugu IGP,

Maafisa na Askari,

Nataka kuwahakikishia kuwa mimi na viongozi wenzangu Serikalini tunatambua umuhimu wa kuendelea kuliongezea Jeshi la Polisi uwezo wa kibajeti ili liweze kutimiza kwa ufanisi zaidi majukumu yake. IGP ni shahidi kwa kiasi gani tumeendelea kuongeza bajeti ya Jeshi la Polisi mwaka hadi mwaka.  Kwa mfano, mwaka 2005 Bajeti ilikuwa Shilingi 69 bilioni na mwaka huu wa fedha zimetengwa Shilingi 134 bilioni. Nawaahidi kuwa tutaendelea kuongeza fedha kila mwaka katika miaka ijayo.  Pia tumetumia uhusiano wetu na nchi rafiki kuomba misaada inayoendelea kuimarisha Jeshi letu kwa zana, mafunzo na weledi.

Napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza Maofisa, Wakaguzi na askari wote kwa kazi kubwa na nzuri muifanyayo katika kulinda maisha na mali za raia.  Nawapongeza kwa uchapakazi wenu na moyo wenu wa kujitolea na kujituma. Hakika maudhui ya Kauli Mbiu yenu ya mwaka huu mmekuwa mnayatekeleza kwa vitendo.  Matokeo ya jitihada zenu yanaonekana. Mafanikio ya kutia moyo yanazidi kupatikana na sote tunayashuhudia. Mwenye macho haambiwi tazama. Uhalifu (hususan wa kutumia nguvu) unaendelea kupungua nchini kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma. Kulingana na takwimu za mwaka wa jana makosa makubwa ya jinai yalipungua kutoka 94,390 mwaka 2010 hadi  76,052 mwaka 2011.

Haya ni mafanikio ya kutia moyo, lakini hamna budi  mtambue kuwa bado idadi ya makosa 76,052 ni kubwa mno. Hivyo bado mnayo na tunayo kazi kubwa ya kufanya mbele yenu na yetu. Inatupasa tuongeze juhudi maradufu au hata zaidi ili tupunguze kabisa uhalifu nchini.

Ndugu Makamanda,

Maofisa Waandamizi wa Polisi;

Mheshimiwa Waziri na Inspekta Generali wamezieleza vizuri changamoto zinazolikabili Jeshi la Polisi na mimi sina haja ya kuzirudia. Napenda kutumia nafasi hii kurudia kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kusaidiana nanyi kwa kuwawezesha ili muweze kuzikabili changamoto hizo kwa mafanikio.  Tumefanya hivyo miaka iliyopita, tunafanya hivyo hivi sasa na tutafanya hivyo miaka ijayo.

Tutaendelea kuliwezesha Jeshi la Polisi kifedha ili muweze kutekeleza ipasavyo majukumu yenu. Tutaendelea kuwawezesha muongeze idadi ya askari.  Tutawawezesha mpate vyombo vya usafiri, zana na vitendea kazi vya kisasa vya kufanyia kazi za kukabiliana na uhalifu.  Kazi ya kulipatia Jeshi la Polisi zana na vifaa vipya vya kazi inaendelea ikiwa ni sehemu ya Programu ya Maboresho ya Jeshi la Polisi.  Nawahakikishia kuwa tutaendelea kutoa fedha za kutekeleza Programu hiyo na shughuli nyingine za Jeshi la Polisi.

Tutaendelea kuwawezesha katika kuboresha mafunzo ya askari na maafisa wa Jeshi la Polisi.  Natambua mahitaji ya kuviboresha vyuo vilivyopo sasa.  Panapohitaji kukarabati pakarabatiwe na panapotakiwa ujenzi wa majengo mapya yajengwe. Na panapotakiwa kuanzishwa  chuo kipya kianzishwe. Hatuna budi kuwekeza katika mafunzo kwani mafunzo ni msingi mzuri wa weledi na kuwa na askari wenye tabia na mwenendo mwema. Kupata zana za kisasa za upelelezi na kudhibiti uhalifu pekee hazitoshi kama zitakuwa mikononi mwa askari asiyejua kitu, asiyekuwa na nidhamu na utiifu.  Kufanya hivyo kunalihakikishia Jeshi uwezo wa kutimiza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa na kuleta sifa kwa Jeshi la Polisi Tanzania.

Dunia imebadilika, Tanzania imebadilika na mbinu za uhalifu na aina za uhalifu yamebadilika.  Pia, mbinu, mikakati na maarifa ya kukabiliana na uhalifu, nayo yamebadilika duniani.  Lazima tusisitize mafunzo, kwani ndiyo msingi wa weledi na ufanisi. Mafunzo ndiyo njia ya kuwawezesha askari na maofisa wa Jeshi la Polisi kupata elimu na maarifa mapya kuhusu uhalifu na namna ya kukabiliana nao.  Mafunzo ndiyo yatakayowezesha kuelewa zana na vifaa vipya vya kupambana na uhalifu na kujua namna ya kuvitumia. Hakuna badala ya mafunzo.

Mheshimiwa Waziri,

Ndugu Inspekta Jenerali,

Maofisa,

Wakaguzi na Askari;

 Mimi na wenzangu katika Serikali tunatambua umuhimu wa kuboresha maslahi ya maofisa na askari wa Jeshi la Polisi pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na kuishi.  Mara baada ya kuchaguliwa mwaka 2005, nilipotembelea Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na baadhi ya kambi nilijifunza mengi kuhusu hali ya maslahi na mazingira ya kazi na malazi ya wanajeshi wetu.  Baada ya hapo tulianza kuyachukulia hatua mambo hayo na tumekuwa tunaendelea kufanya hivyo hadi sasa.  Tumeboresha maslahi kwa kiasi chake na bado tunaendelea.  Tumeanza ujenzi wa nyumba bora za kuishi na bado tunaendelea na mpango huo.

Napenda kurudia kuwahakikishia kuwa kwangu na wenzangu Serikalini, hakuna upungufu wa dhamira ya kuboresha na kuimarisha Jeshi la Polisi nchini kwa maana ya idadi, mafunzo, vitendea kazi, maslahi na mazingira ya kuishi.  Kinachotutatiza ni uwezo wa kifedha wa Serikali ambao si mkubwa sana kuweza kumudu sawia mahitaji yote ya kugharamia shughuli zote za Serikali na Taifa.  Pamoja na changamoto hizo, bado tumeendela kuthubutu kuchukua hatua na kwa haya tuliyoweza kufanya kwa upande wa Jeshi la Polisi si haba. Tunaendelea.

Mheshimiwa Waziri,

Ndugu IGP;

Sina budi kuelezea furaha yangu na pongezi za dhati kwako IGP, Makamishna walioko Makao Makuu ya Polisi pamoja na Makamanda wa ngazi mbalimbali kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana kutokana na rasilimali iliyopo. Huu ni uthibitisho wa uongozi wako makini ukishirikiana na viongozi wa ngazi mbalimbali wa Jeshi letu. Hakika Kauli Mbiu ya mwaka huu kwenu si jambo geni hivyo tunategemea kuona mafanikio makubwa zaidi miaka ijayo. Aidha, mnanipa moyo kuwa hapo rasilimali zitakapoongezeka Jeshi la Polisi litastawi sana.

Usalama Barabarani

Mheshimiwa Waziri,

Inspekta Generali wa Polisi,

Ndugu Makamanda;

Napenda kutumia nafasi hii kurudia maombi yangu kwenu kuimarisha usimamizi wa usalama barabarani.  Ajali za barabarani zimezidi mno, hatuna budi kuzizuia zisizidi kuongezeka. Tufanye kila tuwezalo zipungue. Nawaomba mtumie fursa ya mkutano wenu huu kujadili tatizo hili kwa marefu na mapana yake na mkubaliane juu ya nini cha kufanya. Naamini mtaweza.

Nawaomba jambo hili mlipe uzito unaostahili kabla halijageuka kuwa janga la kitaifa. Ukweli kwamba katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka juzi (2010) jumla ya watu 3,687 walipoteza maisha kutokana na ajali za barabarani. Mwaka na jana (2011) katika kipindi hicho hicho idadi hiyo iliongezeka na kufikia watu 4,013. Hili si ongezeko dogo inatulazimu kushtuka na kuchukua hatua.  Nafahamu dhana ya kuwianisha kuongezeka kwa ajali na kuongezeka kwa pikipiki na magari na hali ya barabara zetu.  Hata hivyo hivi visiwe visingizio vya kuona kuongezeka kwa ajali za barabarani ni jambo la kawaida. Tuseme ukweli kuwa ajali nyingi zinasababishwa na uzembe wa madereva kutokuheshimu Sheria ya Usalama Barabarani na ubovu wa vyombo vya usafiri. Kwa sababu zote hizi mbili Jeshi la Polisi lina wajibu maalum kukabiliana nazo.  Tafadhali timizeni ipasavyo wajibu wenu.  Mkajipange vizuri, kwa kushirikiana na Idara nyingine husika za Serikali, ili ajali na vifo viweze  kupungua.

Madereva wazembe, walevi na wasiotaka kufuata Sheria na Kanuni za usalama barabarani wachukuliwe hatua kali. Wakati umefika madereva wakaidi wanyang’anywe leseni zao ili wasihatarishe tena maisha ya Watanzania. Najua haiwezekani kukomesha kabisa ajali za barabarani, lakini naamini kuzipunguza inawezekana.  Endapo kuna msaada mnahitaji au jambo mnataka kutoka kwetu, tuambieni. Kama mnadhani Sheria ya Usalama Barabarani na Kanuni zake zinahitaji marekebisho, tuleteeni mapendekezo yenu tuyafanyie kazi.  Au kama mnaona kuna mapungufu katika mfumo wa kitaasisi uliopo, msisite kutushauri na sisi tutaangalia namna ya kurekebisha.

Mheshimiwa Waziri,

Ndugu IGP,

Makamanda, Maafisa na Askari,

          Jambo lingine ninalopenda mlizungumze kwa kina na mkubaliane katika Jeshi letu ni juu ya hatua za kuchukua dhidi ya tuhuma za kuenea kwa vitendo vya rushwa katika Jeshi la Polisi. Najua mnajitahidi lakini bado ni hisia ya muda mrefu ya wananchi na haionekani kubadilika. Utafiti unaofanywa na taasisi zinazojihusisha na masuala ya utawala bora kuhusu rushwa bado zinalinyooshea kidole chombo chetu hiki muhimu sana cha dola. Natamani sana hisia na taarifa hizo ingekuwa hazina chembe ya ukweli lakini, bahati mbaya huo ndio mtazamo wa jamii na inaelezea wakati mwingine kwa nini baadhi ya wananchi huchukua sheria mikononi mwao.

Pamoja na kuwepo kwa hisia hizo mimi naamini wapo Polisi wengi wazuri na kwamba hali haijafikia kusema imeshindikana kupambana na kukomesha vitendo vya rushwa katika Jeshi la Polisi.  Penye nia pana njia.  Tafadhali sana tieni  nia ya dhati kupambana na tatizo hili na kushinda.  Watambueni wale wenzenu miongoni mwenu wenye tabia ya kuomba kitu kidogo muwawajibishe ipasavyo kwa adhabu zinazostahili.  Hawa ni watu wanaosaidia wahalifu wasibanwe na mkono wa sheria hivyo ni kikwazo kwa Jeshi la Polisi  kutimiza ipasavyo wajibu wake wa msingi wa kupambana na uhalifu. Waondoeni katika Jeshi kwani wanaharibu sifa yenu nzuri na kudhoofisha Chombo chetu.

Mheshimiwa Waziri,

Ndugu IGP,

Ndugu Makamishna,

Maofisa Waandamizi wa Polisi;

Mabibi na Mabwana;

Yamekuwapo malalamiko mengi ya ukiukwaji wa haki za binadamu yanayoelekezwa kwa Jeshi letu la Polisi katika utendaji kazi. Taarifa za kila mwaka zinazotolewa na Tume ya Haki za Binadamu na taasisi nyingine mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa zimekuwa zikionesha hivyo. Yapo pia madai ya watu kunyanyaswa na Polisi kwa kukamatwa bila makosa, kubambikiwa makosa, kuteswa wakiwa mahabusu na hata kuuliwa. Kuna madai ya Polisi kutumia nguvu kupita kiasi na hata kusababisha vifo ya raia.

Nawaomba mtumie fursa ya mkutano huu myazungumze madai hayo na kuamua hatua zipasazo za kuchukua.  Natambua kuwa katika Programu ya Maboresho ya Jeshi kuwaelimisha wanajeshi wetu kuhusu masuala ya haki za binadamu ni moja ya mambo yaliyopewa kipaumbele.  Nawaomba mtekeleze dhamira yenu hii njema kwa kasi zaidi  ili katika kipindi kifupi muwafikie Polisi wetu wote.  Aidha, mafunzo kuhusu haki za binadamu yawemo katika mitaala ya vyuo vyetu hapa CCP, Police College - Kurasini na Chuo cha Maafisa Wakuu Kidatu.

Aidha, Jeshi liweke utaratibu mzuri na unaoeleweka wa kupokea na kufanyia kazi malalamiko au maoni yanayopelekwa kwao na wananchi.

Ni muhimu kwa Jeshi la Polisi kusisitiza na kusimamia kwa dhati nidhamu ya maofisa na askari wake. Nidhamu ni sifa ya msingi ya askari. Askari asiye na nidhamu amepoteza sifa ya kuendelea kuwa mwanajeshi. Ni hatari sana kwa usalama wa raia na anaharibu sifa ya Jeshi. Vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyofanywa na baadhi ya maofisa na askari kamwe visivumiliwe. Hivi majuzi nimesikia kuwa hapa Moshi askari ametoroka lindo na kwenda disco, tena akiwa na silaha! Vitendo vya namna hii vinaleta fedheha kwa Jeshi la Polisi na kuwaacha watu wakishangaa na kuwa na maswali mengi juu ya Jeshi lao.  Inawezekanaje ifikie hapo kwa askari aliyefunzwa vizuri.

Nawaomba mzingatie upya taratibu zenu za ajira. Wakati umefika wa kuwepo na utaratibu mzuri wa upekuzi wa vijana kabla ya kuteuliwa kusomea kazi ya Polisi.  Pawepo na utaratibu thabiti na kufuatilia mienendo ya askari wakati wote wa utumishi wao.  Majeshi mengine yanafanya hivyo. Kufanya hivyo kutasaidia kupata vijana walio safi kwa tabia na mwenendo kuajiriwa na kuendelea na utumishi katika Jeshi la Polisi.  Kwa ajili hiyo tutakuwa na askari walio watiifu, waaminifu, wachapa kazi hodari na kuliletea sifa Jeshi letu.

Mwisho

Mheshimiwa Waziri,

Inspekta Generali,

Makamanda wa Polisi;

Kabla ya kumaliza hotuba yangu napenda kurudia kutoa pongezi za dhati kwa kazi kubwa na nzuri muifanyayo pamoja na changamoto mbalimbali mnazokabiliana nazo. Nawapongeza sana kwa kubuni utaratibu wa Polisi Jamii ambao ni mfano mzuri wa ubunifu wa kutumia rasilimali zilizopo.  Tafadhali uimarisheni na kuuboresha utaratibu huu mzuri. Sisi katika Serikali tutafanya kila linalowezekana kuongeza rasilimali kwa Jeshi la Polisi ili kuliwezesha kukabiliana na uhalifu nchini. Nawaomba mkumbuke na kuzingatia ukweli kwamba katika kila hatua mnayopiga, sisi Serikalini na taifa zima kwa ujumla tutakuwa pamoja nanyi kuwapa moyo na kuwaunga mkono kwa rasilimali muhimu.

Ndugu Inspekta Jenerali,

Makamanda wa Mikoa na Vikosi,

Mabibi na Mabwana,

Baada ya kusema hayo, ninayo furaha sasa kutamka kwamba, Mkutano Mkuu wa Mwaka 2012 wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi umefunguliwa rasmi. Nawatakia mkutano mwema, mazungumzo yenye ufanisi na matokeo mazuri.

“Ahsanteni kwa kunisikiliza”

No comments: