Tangazo

April 12, 2012

Baada ya 'Lulu' Kupandishwa Kizimbani: Mama Kanumba azungumza ya Moyoni

Mama yake Kanumba, Bi. Flora Mutegoa

Na Waandishi Wetu

SIKU moja baada ya msanii maarufu wa filamu nchini na Afrika Mashariki na Kati, Steven Charles Kanumba (28), kuzikwa kwenye makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam, jana msanii Elizabeth Michael maarufu 'Lulu', anayedaiwa kusababisha kifo hicho, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa shtaka la mauaji ya msanii huyo.

Lulu alipandishwa kizimbani saa 5:20 asubuhi akiwa chini ya ulinzi wa polisi wawili wa kike waliovaa kiraia mmoja kati yao akiwa amemshika bega wakitembea kama mtu na rafiki yake.

Polisi hao walimpitisha Lulu mlango wa nyuma ya mahakama hiyo jambo ambalo liliwafanya watu waliokuwa na shauku ya kutaka kumuona wakiwemo waandishi wa habari, kupata shida ya kujua uwepo wa msanii huyo.

Lulu aliletwa mahakamani hapo akiwa ndani ya gari la polisi lenye namba za usajiri T 848 BNV Toyota Rav 4 nyeupe iliyokuwa na vioo vyeusi ambavyo bilikuwa na namba PT 2565.

Akiwa mahakamani hapo, Lulu alivaa dira la njano na kujifunika mtandio wa pinki, miguuni akiwa amevaa ndala nyekundu.

Akisomewa shtaka lake na wakili wa Serikali Bi. Elizabert Kaganda, mbele ya Hakimu Bi. Augustina Mmbando, ilidaiwa mshtakiwa alitenda kosa la mauaji Aprili 7 mwaka huu, Sinza Vatican.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, Hakimu Mmbando alimtaka mshtakiwa huyo kutojibu lolote mpaka upelelezi wa kesi yake utakapokamilika na kesi kuhamishiwa Mahakama Kuu.

Bi. Kanganda akidai kuwa, upeleleziwa kesi hiyo haujakamilika hivyo aliiomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa ambayo ni Aprili 23 mwaka huu.

Hata hivyo, wakati mshtakiwa akisomewa shtaka hilo, alikana kuwa na umri wa 18 uliotajwa na wakili wa Serikali na kuileza mahakama kuwa umri wake ni miaka 17.

Kauli nzito ya Mama Kanumba

Wakati huo huo, siku moja baada ya mazishi ya Kanumba, mama mzazi wa msanii huyo, Flora Mutegoa, ameamua kutoa yaliyo moyoni juu ya msanii Elizabeth Michael 'Lulu' anayedaiwa kusababisha kifo cha mtoto wake.

Akizungamza na Majira katika mahojiano maalumu Dar es Salaam jana, Mutegoa alisema yupo tayari kumsamehe Lulu kama vyombo husika vitamuona hana hatia juu ya tuhuma zinazomkabili.

Mutegoa pia alikanusha taarifa zinazodai kuwa, marehemu Kanumba alikorofishana na baba yake ndio maana hakuweza kushiriki mazishi na kusema kuwa, taarifa hizo hazina ukweli.

“Marehemu Kanumba na baba yake walikuwa na uhusiano mzuri ila watu waliipokea tofauti filamu aliyoitoa ambayo ilikuwa ikielezea maisha yake, hata mimi sijua baba yake aliipokeaje ila naishukuru Serikali, wananchi na watu wote ambao walijitokeza katika mazishi na mwanangu, sikutarajia kama angezikika kiasi kile,” alisema.

Aliongeza kuwa, Kanumba na baba yake hawakutofautiana kama inavyosemwa na baadhi ya watu ila anachojua yeye, mtoto wake aliamua kuwa mbali na mzee ili kujitafutia maisha yake.

“Baba yake alishindwa kuja kwenye mzsihi kwa sababu anasumbuliwa na miguu yote miwili tatizo ambalo alilipata akiwa ukubwani na limemuanza muda mrefu.

“Sina cha kusema zaidi ya kutoa shukrani zangu kwa Serikali na watu wote wakiwemo wasanii wenzake, hivi sasa tunaendelea na mambo ya kifamilia hapa nyumbani,” alisema.

Alipoulizwa ameupokeaje msiba wa mtoto wake na chanzo cha kifo jhicho, Mutegoa alisema “Kifo hiki hakina tofauti na vifo vingine ambavyo vinatokea, kila binadamu lazima afe”.

“Kama familia, tupo tayari kupokea taarifa zozote ambazo tutapewa na vyombo husika, daktari aliyeuchunguza mwili pamoja na polisi ambao bado wanaendelea na uchunguzi, kwa sasa siwezi kusema mengi ila naiachia Serikali ifanye kazi yake,” alisema.

Kampuni ya filamu aliyoiacha Kanumba

Mutegoa alisema, hivi sasa wapo katika wakati mgumu hivyo hawezi kuzungumzia suala la kampuni ya filamu aliyoiacha mtoto wake pamoja na filamu zake ambazo bado hazijatoka.

Alisema wapo watu wanaosema Kanumba alikuwa na mtoto jambo ambalo si kweli bali anachofahamu mwanae amekutwa na mauti akiwa hajaoa na hakuwahi kuwa na mtoto.

Aliongeza kuwa, zipo taarifa kwamba Kanumba ana watoto wawili alaokuwa akiwasomesha ambao aliigiza nao katika filamu ya “This Is It” na kudai kuwa kama jambo hilo lipo watalijua.

Alisema marehemu Kanumba ni mtoto pekee aliyezaa na baba yake pia ana watoto wengine wa kike na kiume ambao amezaa na mwanaume mwingine.

Kauli nzito aliyotoa mama 'Lulu'

Mama mzazi wa msanii Elizabethi Michael 'Lulu', anayedaiwa kusababisha kifo cha Kanumba, Lucrecia Kalugila, amewaomba wanaharakati wanawake kumsaidia mtoto wake ili kuhakikisha haki inatendeka.

Kalugila aliyasema hayo Dar es Salaam juzi usiku wakati akihojiwa katika mahojiano ya moja kwa moja 'Live', ya kipindi cha wanawake kinachorushwa kila Jumanne na Kituo cha Televisheni ya East African (EATV).

Aliisihi jamii kutomtupia lawama mtoto wake badala yake wasubiri vyombo vya dola vifanye kazi yake.

“Kutokana na uzito wa tukio hili, nawaomba wanaharakati wanawake waniunge mkono ili waweze kunusaidia katika suala hili kwa kuhakikisha haki inatendeka dhidi ya mtoto wangu, ukweli nimesikitishwa na taarifa kifo Kanumba, sikutegemea Lulu kama angekuwa na mahusiano naye, wote niliwaona kama watoto wangu.

“Siku zote Knumba alikuwa akiniita mama, sikuwa na imani kwamba angeweza kuwa na mahusiano na Lulu ila kwa kuwa limeshatokea, tuache sheria ifuate mkondo wake,” alisema.

Aliongeza kuwa, si busara kwa baadhi ya watu kwenda kwa mama mzazi wa Kanumba kuzungumza maneno ya uongo dhidi ya tukio hilo bila kuwa na uhakika wa kile wanachosema.

“Siku ya tukio waliokuwepo Kanumba na Lulu, iweje watu wengine waanze kuzusha maneno yasiyo na uhakika, tuache vyombo vya dola vifanye kazi na kutupa majibu,” alisema Kalugila.

Alitoa wito kwa vyombo vya habari, kuripoti habari zenye uhakika kwani si kweli kwamba mtoto wake alitaka kwenda makaburini kwa ajili ya kuaga mwili wa Kanumba.

“Lulu yuko kituoni chini ya ulinzi wa polisi, iweje leo atake kwenda msibani kumuaga Kanumba,” alisema na kudai kuwa, yupo pamoja na mzazi wa Kanumba kwani msiba huo ni wa wote hivyo amemtaka awe na moyo wa subira ili ukweli ujulikane.

“Mzazi mwenzangu kuwa na subira tupo pamoja, Kanumba ni mtoto wetu sote na mimi nina machungu na kifo chake,” alisema.

Katika hatua nyingine, siri iliyomo kwenye filamu ya mwisho iliyoigizwa Kanumba kabla ya kukutwa na mauti imejulikana.

Filamu hiyo ambayo imepewa jina la Mr. Price ambayo katika moja ya vipande vyake, kinafanana na mazingira ya kifo cha Kanumba.

Akizungumza na gazeti hili, aliyekuwa meneja matukio wa kampuni Kanumba, Rahimu Mtanga maaarufu 'Kiuno', alisema filamu hiyo ina kipande ambacho marehemu aliigiza akigombana na mpenzi wake.

“Kuna sehemu ambayo Kanumba alipewa msaada daktari wake ambaye kwenye filamu hii ameigiza kama rafiki, daktari huyu ndiye aliyefika kumpatia huduma ya kwanza siku alipofariki.

“Katika filamu hii, Kanumba alisukumwa na mpenzi wake na kuanguka, mtu aliyefika kumsaidia alikuwa ni rafiki yake ambaye ndiye daktari wake,” alisema.

Aliongeza kuwa, marehemu Kanumba katika filamu hiyo ameigiza kama mtu maskini ambaye alikuwa na mpenzi wake mwenye tatizo la figo ambapo aliamua kujitolea kumpa figo moja.

Kwa upande wake, Familia ya marehemu Kanumba imeomba radhi kwa wananchi ambao hawakufanikiwa kuuaga mwili mtoto wao kutokana na umati wa watu walioshiriki mazishi hayo.

Mutegoa ambaye ni mama mzazi wa Kanumba, alisema familia hiyo imelazimika kuomba radhi kutokana na watu wengi kukosa fursa ya kumuaga kipenzi chao kwani haikuwa rahisi kwa kila mmoja kuaga mwili huo.

“Sisi kama familia tunachukua fursa hii kuwaomba radhi wananchi wote waliokosa fursa ya kuaga mwili wa mtoto wetu Kanumba kwani haikuwa kusudio letu,” alisema Mutegoa.

Seth Bosco ambaye ni mdogo wa marehemu Kanumba, aliwashukuru wananchi wote walioguswa na msiba huo na kushiriki mazishi ya kaka yake kipenzi.

Baadhi ya watu jana walionekana katika kaburi la Kanumba, Kinondoni, Dar es Salaam ili kujionea sehemu aliyozikwa.
Chanzo: http://www.majira-hall.blogspot.com

No comments: