Tangazo

April 23, 2012

IKULU YAKANUSHA HABARI POTOFU KATIKA GAZETI LA TANZANIA DAIMA

Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili Aprili 22, 2012 lina  habari katika ukurasa wake wa mbele yenye kichwa cha habari ‘JK alinda Mawaziri’,   inayodai  kumekuwa na mazungumzo baina ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda kuhusu hatua inayopaswa kuchukuliwa dhidi ya mawaziri waliotakiwa kujiuzulu.

Habari hiyo imedai kuwa  Mhe. Pinda anataka mawaziri wanaokabiliwa na tuhuma waondoke ili kuleta uwajibikaji serikalini, lakini, imeendelea  kudai habari hiyo, “Rais Kikwete amesema mawaziri hao waachwe waendelee na kazi zao, kwa kuwa suala hili ni la upepo tu, liachwe litapita”.

Tunachukua nafasi hii kuweka bayana kwamba habari katika hilo hazeti la Tanzania Daima Jumapili si za kweli, bali ni za uzushi na upotoshaji mkubwa.

Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi nchini Brazil, amerejea jana Aprili 21, 2012 jioni. Hajaonana wala kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Mhe. Pinda.
 
Hivi sasa Mhe. Rais anasubiri kupata taarifa rasmi  kutoka Bungeni Dodoma.

Mhe Rais anawasihi wananchi wasiamini habari hizo za upotoshaji zilizomo kwenye gazeti hilo la Tanzania Daima Jumapili.

Pia ametoa rai kwa wanahabari wasitoke nje ya mstari wa weledi katika kutekeleza kazi zao ili kuendelea kulinda heshima zao binafsi, vyombo wanavyofanyia kazi pamoja na taaluma yenyewe.
Mwisho

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
22 Aprili, 2012

No comments: