Tangazo

September 23, 2011

AJALI MBAYA YA LORI YAUA WATU WA TATU MBEYA

Polisi wakiangalia gari aina ya roli lenye namba IT. 9518, lililopata ajali baada ya kugongana na gari jingine na hivyo kupinduka na kusababisha vifo vya watu watatu watembea kwa miguu na kuvunja nyumba.
Gari lenye T.438 BRT aina ya Landover, mali ya mchungaji Nduka wa kanisa la Uinjilist Mbalizi. Ambalo liligongana na Lori hilo.
Taswira ya mbele ya Lori hilo lililosababisha hasara kubwa.
Mwanafunzi wa chuo kikuu cha DIT kilichopo Dar es Salaam , Marehemu Dickson Nswila, ambaye alikuwa akielekea kwenye mazoezi ya vitendo TAZARA, jijini Mbeya.
Mfanyabiashara wa mitumba, mji mdogo wa Mbalizi Marehemu Charles Mwakanyuma.
                                     *********************
AJALI mbaya ya lori iliyotokea eneo la Tarafani mji mdogo wa Mbalizi, imesababisha vifo vya watu watatu waliokuwa wakitembea pembezoni mwa barabara ya Mbeya kwenda mji mdogo wa Tunduma, wilayani Mbozi.
 
Ajali hiyo iliyotokea jana saa 2:30 asubuhi, ilihusisha lori hilo , lenye namba IT.9518, lililokuwa likitokea mjini Dar es Salaam , kuelekea nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Kongo (DRC).
 
Muuguzi wa hospitali Teule ya Ifisi, wilaya ya Mbeya vijijini, Rhoda Kasongwa, alisema wamepokea miili ya marehemu watatu akiwemo mwanamke mmoja pamoja na majeruhi mmoja ambaye ni dereva wa lori hilo .
 
Alisema dereva huyo ambaye bado hajatambulika jina lake, wala makazi amepoteza fahamu na anaendelea kupatiwa matibabu, akiwa chumba cha wagonjwa mahuituti (ICU), hospitalini hapo.
 
Aliongeza dereva wa roli, ambaye jina halijatambulika amepoteza fahamu na amelazwa chumba cha wagonjwa mahututi na kuwa ameumia vibaya maeneo ya kichwani pamoja na miguuni, hivyo jitihada zaidi zinafanyika ili kuokoa maisha yake.
 
Aliwataja marehemu kuwa ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha DIT kilichopo Dar es Salaam , Dickson Nswila, ambaye alikuwa akielekea kwenye mazoezi ya vitendo TAZARA, jijini Mbeya na mfanyabiashara wa mitumba, mji mdogo wa Mbalizi Charles Mwakanyuma.
 
Kwa mujibu wa Muuguzi huyo wa hospitali Teule ya Ifisi, mtu wa tatu aliyefariki katika ajali hiyo ni Mariamu Said (31), mkazi wa mji mdogo wa Mbalizi.
 
 
Watu walioshuhudia ajali hiyo walisema lori hilo lililokuwa limepakia shehena ya Chokaa, lilikuwa katika mwendo kasi, na kabla ya kuwagonga na kisha kupinduka, liligonga gari T.438 BRT aina ya Landover, mali ya mchungaji Nduka wa kanisa la Uinjilist Mbalizi.
 
Walisema dereva wa Landlover alikimbizwa hospitali ya Ifisi na aliruhusiwa kurudi nyumbani baada ya kutibiwa na kuonekana hali yake ni nzuri, kwani alipata michubuko kidogo.
 
Waliongeza kabla ya kuligonga Landrover, lori hilo lilikwepa basi lililokuwa limewabeba wafanyakazi wa hospitali Teule ya Ifisi, ndipo liligonga gema lililopo pembeni  ya barabara, kupaa hewani kisha kwenda kuingia kwenye karakana ya mafundi seremala, iliyopo eneo la Tarafani.
 
Wananchi hao walisema polisi walifika eneo la tukio mapema, na hivyo kuweza kunusuru wananchi wasiendelee kupakua shehena ya Chokaa, ambayo walikuwa wakibeba mifuko na kutokomea nayo majumbani kwao.
 
Aidha, mwanamke mmoja alijitolea kwa kivua kitenge chake, kumfunika dereva aliyekuwa amepoteza fahamu na kisha kusaidia kumpakia kwenye gari ili kumuwahisha  hospitalini.
 
Aidha, kabla ya polisi hawajafika eneo la tukio, baadhi ya watu wasiofahamika walifanikiwa kufungua tenki la mafuta la lori hilo na kisha kutokomea nalo.
 
Baadhi ya wananchi walisema wanasikitishwa na kitendo cha baadhi ya watu waliowahi kufika eneo la tukio, kuanza kugombania mifuko ya Chokaa, badala ya kusaidia kuwaokoa majeruhi na kuondoa miili ya marehemu.
 
Miili ya marehemu wote watatu imehifadhiwa hospitali Teule ya Ifisi, iliyopo wilaya ya Mbeya vijijini.
 
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Anaclet Malindisa, alipotafutwa kwa simu yake ya mkononi, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi.


Habari na Picha kwa hisani ya Latest News Tz

No comments: