Tangazo

July 23, 2012

Sheria Mpya ya Mafao miaka 55-60, wafanyakazi wamehusishwa?- WATANZANIA TUJADILI

Serikali imepitisha sheria rasmi kuwa hakuna mtumishi yeyote anaeweza kuchukua mafao yake katika mfuko wowote wa pensheni mpaka tu afikie umri wa kustaafu miaka 55 kwa hiari au 60 kwa lazima.

Uamuzi huu unazua maswali yafuatayo:-

1. Je, mdau wa kwanza katika hili ambaye ni mfanyakazi amehusishwa katika maamuzi haya?

2. Je, Mifuko hii ya Pensheni itaongeza riba katika michango? maana ikumbukwe kuwa thamani ya milioni moja ya leo si sawa na milioni moja baada ya miaka 10 ijayo?

3. Iwapo mtumishi hahitaji tena kuajiriwa na kuchangia katika mfuko, kwanini pesa hii asipewe afanyie kazi anazozijua mwenyewe za kimaendeleo?

4. Kwanini serikali inawakumbuka wananchi pale tu inapohitaji jasho la wananchi?

5. Kwanini serikali impangie mtu binafsi mahitaji yake?

6. Uwezo wa kutumia mafao haya kujipatia mkopo wa nyumba ni kweli au changa la macho?

7. Vipi kuhusu Wabunge, je watachukua pension baada ya bunge kuvunjwa (miaka mitano), au watasubiri umri huo pia?Wafanyakazi katika sheria hii mpya wana mambo muhimu ya kujiuliza:
 

Upitishwaji wa Sheria Hii Mpya
Sheria zote zinazopelekwa bungeni ikiwa pamoja na marekebisho yake, wadau hupewa na nafasi ya kuzijadili na kutoa maoni yao kabla ya kujadiliwa bungeni. Kwa nini mabadiliko ya sheria hayakujadiliwa, yakapitishwa kinyemela bila ya kupata maoni ya wenye mifuko yao? Wamiliki wa mifuko hii ni wafanyakazi, wala si serikali maana serikali haichangii chochote katika mifuko hii.
 
Uzuri ya Mabadiliko Haya
Wafanyakazi ni watu wenye akili timamu, si punguani wala si watoto kiasi cha kuonekana kuwa kuna watu wengine wanaojua uzuri na faida ya mabadiliko haya zaidi ya wafanyakazi wenyewe. 

Wafanyakazi wana haki ya kuamua kwa utashi wao juu ya nini kilicho na manufaa kwa maisha yao ya sasa na ya baadaye, haki hiyo haipo kwa serikali wala bunge au chombo kingine chochote. 

Kama mabadiliko haya yanafanywa kwa manufaa ya wafanyakazi kwa nini manufaa hayo yasipelekwe kwa wafanyakazi ambao ndiyo wadau wakubwa, wakayajadili na kuona faida badala ya kuyapitisha kwa siri?
 
Wafanyakazi Kunyang'anywa Pesa Yao
Mifuko hii inatunza fedha za Wafanyakazi, si fedha ya serikali. Lakini mifuko inavyoendeshwa hapa Tanzania, imefanywa kuwa ni pesa za serikali na hivyo serikali kuamua kuzitumia pesa hizo kadiri inavyotaka au hata kuiwekea sheria na kanuni bila ya ushiriki kamilifu wa Wafanyakazi ambao ndiyo wachangiaji wa mifuko hii. 

Serikali imeifanya mifuko hii ndiyo hela ya serikali ya kuendeshea miradi mikubwa ya maendeleo bila kuangalia faida watakayopata wachangiaji wa mifuko hii kwenye hiyo miradi ya maendeleo. 

Mifuko hii haipo kwaajili ya kuendesha serikali au kugharamia miradi ya serikali, jukumu lake la kwanza ni kuangalia manufaa ya wanachama wake ambao ni Wafanyakazi lakini haki hii ya msingi ya wanachama wa mifuko hii imeporwa na serikali.
 
Njama za Kuwaibia Wafanyakazi
Faida zinazotajwa na wanaotetea mabadiliko haya ni za kinadharia sana. Katika nchi ambayo ni 6% tu ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi ndiyo walioajiriwa kwenye sekta rasmi, uhakika wa mfanyakazi kuwa katika ajira wakati wote mpaka kufikia umri wa miaka 55 au 65 ni mdogo sana. 

Wafanyakazi wengi kwenye sekta binafsi wanafanya kazi kwa mikataba ya muda mfupi, na baada ya kumaliza mikataba yao hakuna uhakika wa kupata ajira tena. Mathalani mfanyakazi ameajiriwa mara moja kwa kipindi cha miaka 2, ni vipi atanufaika na mabadiliko haya? 

Na wakati huo atakapofikisha miaka 55 (kama atafika) atapata nini wakati thamani ya shilingi inaporomoko kila siku na huku mfumko wa bei ukikua kwa kasi ya ajabu? Ndiyo maana mabadiliko haya hayana manufaa kwa wanachama wa mfuko bali ni njia nyingine ya kupokonya hela ya mfanyakazi kwa kutumia lugha ya udanganyifu. 

Kilio cha wafanyakazi wa Tanzania ni kodi kubwa ya PAYEE, badala ya serikali kusikiliza kilio hiki cha wafanyakazi, imezidi kuwapokonya hata kile kidogo walichokuwa wanakipata wamalizapo mikataba yao ya kazi. 

Baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wakitumia mafao haya kuanzishia miradi midogo midogo, wengine huyatumia kwa kujisomesha na wengine hata kuwasomesha watoto wao ambao kwa vipato vyao vya mwezi wanashindwa kufanya hivyo.
 
Serikali kwa sasa inachukua karibu 20-30% ya mshahara wa mfanyakazi kama PAYE, sasa imeamua kuchukua tena 20% ya mshahara wa mfanyakazi. Hii ina maana sasa serikali itakuwa ikichukua karibu 40-50% ya pesa yote ya mfanyakazi.
 
Hoja ya Kuiga Mfumo wa Mataifa Mengine
Kati ya sababu zinazotolewa ni kuwa mfumo huu mpya unafuata maelekezo ya ILO na jinsi nchi nyingine zinavyofanya. 

Undumilakuwili wa serikali ni kama ifuatavyo. Tumekuwa tukiongelea matumizi mabaya ya fedha za umma yanayofanywa na serikali na watendaji wake. 

Kwa mfano katika serikali kukifanyika kikao wanalipana posho ya malazi na chakula, na posho ya kukaa. Posho hii ya kukaa hailipwi na nchi yoyote iliyoendelea, ukiwauliza kwa nini wasifuate taratibu zinazofuatwa na mataifa mengine, jibu ni kuwa 'sisi ni taifa jingine na hivyo hatulazimiki kufuata taratibu za mataifa mengine'. 

Mataifa ya wenzetu kiongozi yeyote ambaye taasisi yake inakumbwa na kashfa, lazima mkuu wa kitengo hicho huwajibika, lakini hapa kwetu ukiwauliza kwa nini tusifuate mfumo huo wa wenzetu, tunaambiwa hutulazimiki kufuata mifumo hiyo maana sisi ni Taifa huru ambalo halilazimiki kufuata taratibu za mataifa mengine, na yapo mengi ya namna hiyo.

 Inapokuja kwenye suala la kumkamua mfanyakazi, ukiuliza juu ya kodi kubwa anayokatwa kwenye PAYE, utapewa takwimu za kodi za mataifa mengine (hapo haielezwi tena kuwa sisi ni Taifa huru lisilohitaji kufuata juu ya nini mataifa mengine yanafanya). 

Kwenye hili la mifuko ya jamii nalo wafanyakazi wanaambiwa kuwa ndivyo mataifa mengine yanavyofanya. Wakati katika uhalisia mataifa hayo yana uhakika mkubwa wa ajira kwa watu wake, yana umri mkubwa zaidi wa tegemeo la kuishi, sarafu zao ni imara, na mfumko wa bei upo chini sana ukilinganisha na Tanzania. Serikali iache kuendekeza mambo yanayowadhulumu wafanyakazi wakati huo huo ikiyatetea yale yenye kuwanufaisha viongozi wa serikali.
 
Wafanyakazi Wanatakiwa Kufanya Nini?
 
Wafanyakazi Wamiliki Mifuko Yao
Wafanyakazi, katika katiba mpya wahakikishe inaingizwa kwenye katiba mpya kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii ni mali ya wafanyakazi na itasimamiwa na wafanyakazi wenyewe kwa kupitia vyama vyao vya wafanyakazi. 

Mifuko hii itakapokuwa chini ya wafanyakazi wenyewe itaweza kufanya kazi kwa manufaa ya wanachama wake, itaweza kuanzisha vitega uchumi ambavyo vitamwezesha mwanachama kuwa na gawio la faida maisha yake yote kwa kutegemeana na kadiri alivyochangia. 

Kwa kiasi cha pesa kinachopatikana kwenye mifuko hii kuna uwezekano mkubwa wa wafanyakazi wanapoondoka kazini kupewa pesa yao yote waliyochangia, na bado wakaendelea kushikilia hisa katika vitega uchumi kutokana na faida zilizopatikana. 

Hili litaondoa wajumbe wa bodi na wakurugenzi wanaoweza kuteuliwa kwa manufaa ya kisiasa na kisha wakaamua kuwatumikia waliowateua kuliko wanachama wa mifuko.
 
 Kudai Ripoti ya Mchakato wa Mabadiliko ya Sheria
Wafanyakazi kwa kupitia vyama vyao vya wafanyakazi wadai taarifa juu ya mchakato wa namna mabadiliko yalivyofikiwa. Kama ikigundulika kuwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi walishirikishwa lakini wao hawakuwashirikisha wafanyakazi, viongozi wote wa wafanyakazi wafukuzwe kwenye nafasi zao.

 Kama hilo halitawezekana, basi wafanyakazi wote wajitoe kwenye uanachama wa vyama vyote vya wafanyakazi na kuunda vyama vingine vyenye kufanya kazi kwa manufaa ya wanachama wake na siyo kwa manufaa ya serikali.
 
Njia za Kisiasa
Wenzetu katika mataifa yaliyoendelea, ikifika wakati wa uchanguzi makundi mbalimali huweka bayana matakwa ya kundi lao, na hutoa tamko kuwa, 'sisi kama kundi mojawapo la kijamii, tutamchagua kiongozi au chama kitakachosimamia au kufanya mambo 1) -----, 2) ----n.k.'. Wafanyakazi wa Tanzania, sasa ni wakati wa kuungana na kuachana na ushabiki wa kisiasa na badala yake kama kundi mojawapo la kijamii kuangalia maslahi ya kundi letu. 

Ifike mahali, kama wafanyakazi wa Tanzania tutamke kuwa, 'wafanyakazi wote tutakiunga mkono chama au mgombea ambaye atashusha PAYE kwa 25% kutoka ilipo sasa na kwa namna yeyote ile mtu asilipe PAYE inayozidi 20% ya mshahara wake. 

Pili tuseme kuwa tutamchagua kiongozi au chama kitakachokuwa tayari kuiachia mifuko ya kijamii irudi kwa wanachama wake na iendeshwe na wanachama wenyewe.
 
Wafanyakazi wa Tanzania tukiendekeza siasa na ushabiki wa vyama, wanasiasa wataendelea kuwachezea wafanyakazi miaka yote huku wao wasiozalisha wakijipangia maslahi mazuri na mazingira ya malipo starehe huku mchangiaji mwenyewe akibakia hoi bin taabani.

UFAFANUZI KUHUSU FAO LA KUJITOA KATIKA MAREKEBISHO YA SHERIA ZA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII.
 
Ufuatao ni ufafanuzi mfupi kuhusu marekebisho ya Sheria za Mifuko hasa kuhusu fao la kujitoa.
 
1.    Kama mtakumbuka Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pamoja na Sheria ya Mamlaka zimefanyiwa marekebisho na kupitishwa na Bunge tarehe 13 Aprili, 2012. Sheria hiyo tayari imeshasaininiwa na Mheshimiwa Rais na imeanza kutumika rasmi. Marekebisho haya yanawahusu wafanyakazi wote nchini mwetu bila kubagua sekta yoyote ile.
 
2.    Kwa mujibu wa marekebisho hayo fao la kujitoa (withdrawal benefits) yamefutwa na kuanzia sasa hayatakuwepo. Mafao hayo yalikuwa yanatolewa pale mwanachama alipokuwa anaacha kazi. Sasa mwanachama wa Mfuko atapata mafao yake pale atakopfikisha umri wa kustaafu kwa hiari (miaka 55) au kwa lazima (miaka 60) au pale anapopata ulemavu wa kudumu.
 
3.    Kwa kuzuia fao la kujitoa mwanachama anapata fursa ya kupata mikopo ya nyumba kwa kutumia dhamana ya michango yake kama ilivyoelezwa kwenye Sheria ya SSRA kipengele cha 38.
 
4.    Marekebisho hayo kuhusu kuzuia mafao ya kujitoa yamefanyika ili kutimiza lengo na madhumuni ya hifadhi ya jamii ambayo ni kuhakikisha kuwa mwanachama anapostaafu anapata mafao bora yatakayomwezesha kumudu maisha ya uzeeni wakati ambapo nguvu ya kufanya kazi tayari imeshamwishia. Mafao ya kujitoa yanapunguza na hata kuondoa kabisa kinga ya mfanyakazi pale anapoumia kazini au anapofika uzeeni.
 
5.    Tunawaomba muwaelimishe wafanyakazi umuhimu na madhumuni ya mafao ya hifadhi ya jamii. Hifadhi ya jamii ni nyenzo mahususi iliyowekwa kuwasaidia
 
1Wafanyakazi kuendesha maisha yao wakati wanapokuwa wameishastaafu tayari. Umasikini wa kipato wakati wa uzee ni mojawapo ya changamoto ngumu kukabiliana nazo kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Tunawasihi tena muelimishe wafanyakazi kuhusu jambo hili. Tafadhali msisite kuwasiliana na Mamlaka pale ufafanuzi zaidi utakapohitajika
 
6.    Kwa kuwa marekebisho hayo yamesainiwa na kuanza kutumika rasmi kama sheria, mafao ya kujitoa hayawezi kutolewa tena na wafanyakazi watakaoacha kazi kwa sababu ya marekebisho ya kipengele hicho watakuwa hawajaijitendea haki wao wenyewe na pia itakuwa ni kunyume cha Sheria. Mamlaka inaandaa kanuni za mafao ambayo lengo lake ni kuboresha maslahi ya wanachama, kanuni hizo zitajadiliwa na wadau wakiwemo vyama vya wafanyakazi na waajiri ili kupata maoni yao.
 
7.    Tafadhali muwaelimishe wafanyakazi kwamba pamoja na kuzuia fao la kujitoa, mafao mengine ambayo ni muhimu kwa sekta ya Madini yataendelea kutolewa kama kawaida. Mafao hayo ni Kama vile kuumia kazini pamoja na fao la ulemavu
 
8.    Tumesikia kwamba tayari kuna hofu imejijenga kwa wanachama kuhusiana na fao la kujitoa. Ikumbukwe kwamba baadhi ya Mifuko ilikuwa inatoa fao hilo kinyume cha Sheria kwani katika Sheria zao hakuna fao la kujitoa. Tunapenda kusisitiza kwamba wanachama wawe watulivu wakisubiri miongozo.
 
9.    Tunapenda kuwahakikishia kwamba katika hili maslahi ya wanachama yatalindwa na hakuna mwanachama atakayepunjika kutokana na utaratibu huo. Mamlaka imepanga kutembelea wafanyakazi wa sekta ya madini katika juma la kwanza la mwezi Agosti 2012 ili kutoa ufafanuzi zaidi kwa wanachama wote.
 
Tunatanguliza shukrani za dhati kwa ushirikiano.
 
 
Wenu.
Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii

No comments: