Tangazo

January 21, 2013

NAPE: UBAGUZI UNAWAMALIZA CHADEMA

Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akihutubia maelfu ya wananchi waliofurika kwenye mkutano wa CCM uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza na mgeni rasmi akiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Phili Mangula.
***************************************
- Asema kwa dhambi hiyo hakuna dawa lazima Chadema kife.
- Adai ni laana ya Mwalimu wasitafute mchawi.
- Awaasa waandae mazishi mapema.

 
NA MWANDISHI WETU, MWANZA

KATIBU wa wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amewataka Chadema wasitafute mchawi anayewamaliza nje ya chama  chao kwa kuwa ubaguzi ulioota mizizi kwa muda mrefu ndani ya chama hicho ndiyo unaowamaliza.

Alisema kwa kukumbatia ubaguzi aliodai kulelewa na waasisi na viongozi wa kitaifa ndani ya Chadema, sasa iliyobaki  waandae mapema, mazishi ya chama hicho kwa kuwa hakuna jinsi ambavyo kitanusurika kufa kutokana na dhmabi hiyo mbayo hata Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliikemea akisema ni mbaya sawa na kula nyama ya mtu.

Nape aliyasema hayo jana Januari 20, 2013,  jijini Mwanza kwenye mkutano wa hadhara wa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Philip Mangula na baadhi ya mawaziri, uliohudhuriwa na maelfu ya wanachi wa jiji hilo na vitongoji vyake kwenye Uwanja wa mpira wa Nyamagana.

Nape alisema anashangazwa na viongozi wa Chadema kuendelea kunyooshea vidole CCM kuwa eti inahusika na mtafaruku na umahututi wa chama chao wakati CCM walishajitahidi kuwataadharisha mapema kuwa ubaguzi wanaoukumbatia, licha ya kuathiri umoja na mshikamano ni dhambi ambayo itakisambaratisha chama hicho.

"Hamuwezi kuwa na chama ambacho ili kiongozi wake adumu na kuheshimika lazima awe anatoka ukanda fulani au ukoo fulani ndio adumu, vinginevyo anasukiwa mizengwe na mwisho kutimuliwa" alisema Nape na kuongeza "walianza na kina Chacha Wangwe na Watanzania wote wanajua leo kilichompata Chacha Wangwe, sasa wameanza kumwandama Zitto na wanaoitwa vijana wake, na pia nasikia wamejipanga kumfukuza Shibuda wiki ijayo."

"Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alishasema dhambi ya ubaguzi ni kubwa,  na ni sawa na kula nyama ya mtu, ambapo mtu akishaila anazoea kiasi kwamba haachi,  basi nao Chadema hawana namna ya kuachana na ubaguzi unaoendelea ndani ya chama chao, hivyo watasambaratika kwa laana hiyo ya Mwalimu", alisema Nape.

Nape alilionya kwamba, ikiwa Chadema wanabaguana kiasi hicho ndani ya alichokiita kichama kidogo, kama hicho watafanyaje wakipewa dhamana ya kutawala nchi. " Ikiwa wanabaguana ndani ya kichama kidogo kiasi hichi ambacho hakijai hata mkononi, watafanyaje wakipewa dhamana ya kuongoza hata kipande cha nchi yetu?" alihoji.

Nape alidai kuwa ubaguzi ndani ya Chadema umejikita kwenye ukanda, ukabila na hata udini na kwamba ubaguzi huo unajionyesha zaidi kwenye safu ya uongozi wa chama hicho na maeneo mengine. "Sasa leo nimeamua kuwapa ushauri wa bure kabisa Chadema wasiendelee kutafuta mchawi nje ya chama chao", alisema.

Mkutano huo ambao umehusisha wananchi kutoka Wilaya za Ilelema na Nyamagana, ni moja ya mikutano ya Mangula ambayo amekuwa akiifanya tangu aanze ziara ya kwanza katika mkoa wa Mwanza ambapo tayari ameshapita katika wilaya za Magu, Ukerewe na Sengerema.


No comments: