Tangazo

March 25, 2013

Mapato ya Tamasha la Pasaka kujenga kituo cha yatima Dar

 Mwenyekiti wa Maandalizi ya Tamasha la Pasaka Alex Msama akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo kuhusu maandalizi ya tamasha hilo lenye kauli mbiu ya Amani na Upendo. Kulia ni Mdau wa muziki wa Injili, Mcharo Mrutu. (Picha na Francis Dande) 

Na Francis Dande

WARATIBU wa tamasha la Pasaka litakalofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, jijini
Dar es Salaam hapo Machi 31, wamepanga kutumia sehemu ya mapato ya kiingilio
kujenga kituo cha watoto yatima kama ishara ya shukrani kwa jamii.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa Kamati maalumu inayoratibu tamasha hilo la kimataifa, Alex Msama, alisema kituo hicho kitakachokuwa chini ya kampuni ya Msama Promotions kitajengwa eneo la Pugu.

Alisema uamuzi huo umefikiwa kwa lengo la kuwapa faraja watoto yatima ambao nao wana haki ya kupatiwa matunzo na mahitaji muhimu katika makuzi yao ikiwemo elimu katika kujenga taifa bora la kesho.

“Tangu kuasisiwa kwa tamasha la Pasaka mwaka 2000, tumekuwa tukirejesha sehemu
ya mapato ya viingilio kwa jamii kwa njia ya misaada kwa yatima, wajane na walemavu, lakini safari hii tumeona twende zaidi ya hapo kwa kujenga kituo cha watoto,” alisema.

Alisema lengo ni kujenga kituo hicho cha kisasa ambapo kama mipango itakwenda vizuri, kitakamilika kabla ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda wake kwani wangependa ndiye akizindue kwa kutambua mchango wake kwa tamasha hilo.

“Mwaka 2011, Rais Kikwete ndiye alikuwa mgeni rasmi wa tamasha letu pale
Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.

“Kitendo cha Rais kuacha kazi nyingi na kuja kutuunga mkono kwenye shughuli hii
 ya kiroho, kwetu ni jambo kubwa sana ambalo kamwe hatutalisahau, hivyo tumeona tumpe heshima hiyo ya kuzindua kituo hicho akiwa bado madarakani,” alisisitiza.

Msama ametoa wito kwa wapenzi, mashabiki na wadau wa muziki wa injili kujitokeza kwa wingi kuunga mkono juhudi za kampuni yake kuandaa tamasha hilo kwa malengo mbalimbali ikiwemo kueneza injili ya Mungu na kusaidia makundi maalumu.

Kuhusu waimbaji, Msama alisema wale wa nje wataanza kuwasili wiki ijayo na kuongeza kuwa hadi kufikia Ijumaa, waimbaji wote  watakuwa wamefika tayari
kwa tukio hilo mbalo mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Aliongeza kuwa idadi ya waimbaji imeongezeka baada ya kujitokeza kwa mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Ntutuma kutoka nchini Kenya.

Baada ya kishindo cha tamasha hilo kutikisa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, itakuwa zamu ya Dodoma, Iringa, Mbeya, Mwanza kabla ya mashambulizi kuhimishwa mkoani Mara.

No comments: