Tangazo

December 20, 2017

TANESCO YAHIMIZA MATUMIZI BORA NA ENDELEVU YA MTO PANGANI NA BWAWA LA NYUMBA YA MUNGU

  NA K-VIS BLOG/Khalfan Said

MATUMIZI bora ya bonde la Mto Pangani, ndio njia pekee itakayosaidia kutunza vyanzo vya maji ambayo hutumika kuzalisha umeme kwenye vituo vya Pangani Hydro Systems, Meneja wa vituo hivyo, Mhandisi Mahenda S Mahenda amewaambia wahariri wa vyombo vya habari wanaotembelea bwawa la Nyumba ya Mungu lililoko mpakani mwa wilaya ya Mwanga na Simanjiro.

“Tanesco kama wadau wakubwa wa Mto huu, tumeona Mto umeingia mchanga na mchanga huo unatakiwa kuondolewa ili kuweza kuzalisha maji mengi zaidi kutoka bwawa la Nyumba ya Mungu na maji hayo yaweze kupatikana kwenye vituo na hatimaye kuzalisha umeme kama ambavyo inatakiwa.” Alisema Mhandisi Mahenda.
Pangani Hydro Systems ni mkusanyiko wa vituo vitatu vya kufua umeme vinavyofuatana ambavyo vimejengwa sehemu tofauti tofauti katika Mto Pangani.

Vituo hivyo ni pamoja na Nyumba ya Mungu, kituo cha Hale na kituo cha New Pangani Falls na vyote kwa ujumla wake huzalisha umeme wa Megawati 97 ambazo huingizwa kwenye Gridi ya Taifa, alisema Mhandisi Mahenda.

Kituo cha Nyumba ya Mungu, kilizinduliwa mwaka 1964 na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere, na kina mashine mbili za kufua umeme zilizofungwa tangu mwaka huo na kila moja inao uwezo wa kuzalisha Megawati 4 za Umeme na kufanya jumla ya Megawati 8.

Hata hivyo changamoto kubwa inayokikabili kituo hicho na vituo vingine ambavyo vyote huendeshwa kwa kutumia nguvu za maji, ni mabadiliko ya tabia nchi na ongezeko la shughuli za kibinadamu kandokando ya Mto huo pamoja na kwenye bwawa lenyewe na hivyo kupelekea upungufu wa mara kwa mara wa maji ya kutosha kuendesha mitambo.

“Tunashirikiana na wenzetu wanaosimamia bonde la Mto Pangani, kwa kufanya doria za mara kwa mara ili kuwaelimisha wananchi matumizi bora na endelevu ya maji ya Mto huo ili kuleta manufaa kwa pande zote, amesema Mhandisi Mahenda.


Mhandisi Mahenda S. Mahenda(kulia), akifafanua mambo mbalimbali kwa wahariri kwenye bwawa la Nyumba ya Mungu Desemba 19, 2017

No comments: