Tangazo

July 29, 2012

MAKALA YA JUMAPILI: Bengu (Dondatumbo) Ugonjwa wa Ajabu unaotishia maisha ya Watoto Kigoma

Kopo la bati na kipira chekundu ni (Mwino), bomba ambalo hutumika kupitisha mchanganyiko wa dawa hadi tumboni na baadhi ya miti tiba inayotibu ugonjwa wa bengu.  (Picha na Magreth Magosso)
***********************
Na Magreth Magosso, Daily Mitikasi Blog - Kigoma

Jamii ya wakazi wa mkoa wa Kigoma Ujiji, inakabiliwa na changamoto ya chanzo cha maradhi ya Bengu (Dondatumbo), ambayo huwakumba watoto  wadogo hasa walio chini ya miaka mitano.

Hayo yamebainika hivi karibuni, baada ya Daily Mitikasi Blog  kufanya mahojiano na baadhi ya wenyeji  na madakitari waishio mkoani Kigoma  kuhusu ugonjwa huo ili  kufahamu chanzo chake, tiba sanjari na kinga ambapo wakazi wake wamekiri kufahamu maradhi hayo na kubainisha kuwa matibabu yake ni  tiba asilia.

Ugonjwa wa Bengu (donda tumbo) umekuwa na tabia ya kuwashambulia watoto wadogo ambapo dalili zake hurandana na mtoto aliye na ugonjwa wa utapiamlo na  kwa wageni wa mkoa huo hupata shida kuugundua.

Mmoja wa  watoa tiba asilia, Anzelami Byongo anasema  kuwa Ugonjwa wa Bengu ulinza kujitokeza katika Miaka ya 1980, baada ya ujio mkubwa wa raia  wa nje hasa kutoka  nchini za Burundi, Rwanda na Congo.
Byongo ambaye anadai  kurithi utaalamu wa tiba hizo toka enzi za  wazee wao ambao nao amedai walioteshwa ndotoni.

“Dalili zake hazitofautiani na mtoto mwenye ugonjwa wa utapiamlo kwani nywele hubadilika na kuwa rangi ya kahawia, ngozi yake hujikunja na kupauka kama majivu, hutokwa na vipele vidogovidogo pamoja na kuharisha  kinyesi cha majimaji yenye mafuta “ anabainishwa Byongo.

Aidha Byongo amebainisha kwamba pamoja na dalili hizo pia mtoto huanza kutapika pindi alapo chakula na kadiri anavyougua fupa la uti wa mgongo hujitokeza  hali inayotishia kupoteza  uhai wa mtoto.

Katika kujua chanzo cha maradhi haya Byongo amesema  hajajua  chanzo kamili ingawa husadikika umetokea DRC, japo tiba za hospitali hazina uwezo wa kutatua changamoto hiyo, kwani wengi hurudia dawa za miti ya asili ambazo huchanganywa na za hospitali.

Akibainisha baadhi ya dawa tiba ya ugonjwa wa Bengu,  Byongo  anasema mti wa Mbona Makaburi,T etesaclini, Majani ya mwembe, Peremende (dawa ya mende) huchanganywa na maji kwa kufuata kiwango maalum cha umri wa mtoto na kutiwa kwenye kipira maalum na kumwinama maji hayo yenye mchanganyiko wa dawa( kupitia njia ya haja kubwa) ambapo wenyewe huita ( Mwino).

Naye Diwani wa Viti Maalum  Kata ya Mwamgongo,  Hidaya Kwapi alikiri kuwepo kwa ugonjwa huo na tiba zake ni miti ya asili  na alishindwa kubainisha chanzo cha ugonjwa huo, japo alikiri maradhi hayo hutoka nchi za jirani hali inayowafanya wakazi wengi mkoani Kigoma kuwa na Mwino (mabomba) ili kujipatia huduma hiyo inapolazimu.

“Kwa kweli wengi tunadhani kuwa nepi ndio sababu ya Bengu, wengine udongo lakini wengine hupatwa kabla ya mtoto kutambaa japo tiba tunaijua chanzo kamili bado.” Anasema Kwapi.


Lucy Matias amekiri na kufahamu tatizo hilo na chanzo cha kuwalazimu  jamii ya watu wa kigoma kuishi na zana za mwino ni jambo la kawaida kwao, kwani mwino ni suluhisho lao la mwisho katika kutatua maradhi  hayo sanjari na wakubwa kwa watoto hutumia kusafisha tumbo pindi washindwapo kula vizuri.

Daily Mitikasi Blog  haikuishia kwa jamii tu, ilipiga hodi kwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Vijijini, Dk. Kilimba ambaye naye alishindwa kulitolea ufafanuzi kamili kwa kusema kuwa hajawahi kumuona mtoto mwenye shida hiyo.

Dk.Kilimba anasema inawezekana ukawepo lakini jamii husika ikaishia kwenye tiba asilia pasi wao kujua na kudai kuwa labda hospitali ya mkoa wanaweza wakalijua hilo.

Dk.Moses Jaba amekiri kushindwa kubaini ugonjwa huo kwa kitaalamu hali iliyomfanya ashindwe kulitolea ufafanuzi ,huku akihaidi kulifanyia kazi ili aweze kuisaidia jamii pale inapotakiwa.

Ugonjwa wa bengu ( donda tumbo) umekuwa ukiwaathiri watoto wadogo kwa miaka mingi  mkoani Kigoma hali inayotishia hata ukuaji bora  wa  mtoto pindi uchelewapo kupata tiba kwa wakati, idara ya afya ifanye mazungumzo na jamii ili kulifanyia tafiti ya kitaalamu zaidi ili kupata kinga na tiba yenye kutambulika nchini.kwa sasa ugonjwa huu hauna kinga zaidi ya tiba.

 Mkoa wa Kigoma upo Magharibi ya pembezoni mwa nchi ya Tanzania, ambapo umepakana na nchi nne za jirani ikiwemo Jamhuri ya Watu wa Congo (DRC), Burundi, Rwanda na Zambia.

Kutokana na mwingiliano wa ujirani mwema ni rahisi wakazi wa mkoa huo kupata maradhi toka nchi hizo hasa kutokana na shughuli za kibiashara.

4 comments:

Marry said...

Hata mwanangu anaumwa Leo tupo kigoma

Unknown said...

Kwahyo tiba yake kwaujumla ikoje sasa

FETCH IT NOW said...

Mtoto anaeumwa hiyo anakuaje?

Anonymous said...

Mungu ingilia kati