Kopo la bati na kipira chekundu ni (Mwino), bomba ambalo
hutumika kupitisha mchanganyiko wa dawa hadi tumboni na baadhi ya miti tiba
inayotibu ugonjwa wa bengu. (Picha na Magreth
Magosso)
|
***********************
Na Magreth Magosso, Daily Mitikasi Blog - Kigoma
Jamii ya wakazi wa mkoa wa Kigoma Ujiji, inakabiliwa na
changamoto ya chanzo cha maradhi ya Bengu (Dondatumbo), ambayo huwakumba
watoto wadogo hasa walio chini ya miaka
mitano.
Hayo yamebainika hivi karibuni, baada ya Daily Mitikasi
Blog kufanya mahojiano na baadhi ya
wenyeji na madakitari waishio mkoani
Kigoma kuhusu ugonjwa huo ili kufahamu chanzo chake, tiba sanjari na kinga
ambapo wakazi wake wamekiri kufahamu maradhi hayo na kubainisha kuwa matibabu
yake ni tiba asilia.
Ugonjwa wa Bengu (donda tumbo) umekuwa na tabia ya
kuwashambulia watoto wadogo ambapo dalili zake hurandana na mtoto aliye na
ugonjwa wa utapiamlo na kwa wageni wa
mkoa huo hupata shida kuugundua.
Mmoja wa watoa tiba
asilia, Anzelami Byongo anasema kuwa
Ugonjwa wa Bengu ulinza kujitokeza katika Miaka ya 1980, baada ya ujio mkubwa
wa raia wa nje hasa kutoka nchini za Burundi, Rwanda na Congo.
Byongo ambaye anadai
kurithi utaalamu wa tiba hizo toka enzi za wazee wao ambao nao amedai walioteshwa
ndotoni.
“Dalili zake hazitofautiani na mtoto mwenye ugonjwa wa
utapiamlo kwani nywele hubadilika na kuwa rangi ya kahawia, ngozi yake
hujikunja na kupauka kama majivu, hutokwa na vipele vidogovidogo pamoja na
kuharisha kinyesi cha majimaji yenye mafuta
“ anabainishwa Byongo.
Aidha Byongo amebainisha kwamba pamoja na dalili hizo pia
mtoto huanza kutapika pindi alapo chakula na kadiri anavyougua fupa la uti wa
mgongo hujitokeza hali inayotishia
kupoteza uhai wa mtoto.
Katika kujua chanzo cha maradhi haya Byongo amesema hajajua
chanzo kamili ingawa husadikika umetokea DRC, japo tiba za hospitali
hazina uwezo wa kutatua changamoto hiyo, kwani wengi hurudia dawa za miti ya
asili ambazo huchanganywa na za hospitali.
Akibainisha baadhi ya dawa tiba ya ugonjwa wa Bengu, Byongo
anasema mti wa Mbona Makaburi,T etesaclini, Majani ya mwembe, Peremende
(dawa ya mende) huchanganywa na maji kwa kufuata kiwango maalum cha umri wa
mtoto na kutiwa kwenye kipira maalum na kumwinama maji hayo yenye mchanganyiko
wa dawa( kupitia njia ya haja kubwa) ambapo wenyewe huita ( Mwino).
Naye Diwani wa Viti Maalum
Kata ya Mwamgongo, Hidaya Kwapi
alikiri kuwepo kwa ugonjwa huo na tiba zake ni miti ya asili na alishindwa kubainisha chanzo cha ugonjwa
huo, japo alikiri maradhi hayo hutoka nchi za jirani hali inayowafanya wakazi
wengi mkoani Kigoma kuwa na Mwino (mabomba) ili kujipatia huduma hiyo
inapolazimu.
“Kwa kweli wengi tunadhani kuwa nepi ndio sababu ya Bengu,
wengine udongo lakini wengine hupatwa kabla ya mtoto kutambaa japo tiba
tunaijua chanzo kamili bado.” Anasema Kwapi.
Lucy Matias amekiri na kufahamu tatizo hilo na chanzo cha
kuwalazimu jamii ya watu wa kigoma
kuishi na zana za mwino ni jambo la kawaida kwao, kwani mwino ni suluhisho lao
la mwisho katika kutatua maradhi hayo
sanjari na wakubwa kwa watoto hutumia kusafisha tumbo pindi washindwapo kula
vizuri.
Daily Mitikasi Blog
haikuishia kwa jamii tu, ilipiga hodi kwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya
Kigoma Vijijini, Dk. Kilimba ambaye naye alishindwa kulitolea ufafanuzi kamili
kwa kusema kuwa hajawahi kumuona mtoto mwenye shida hiyo.
Dk.Kilimba anasema inawezekana ukawepo lakini jamii husika
ikaishia kwenye tiba asilia pasi wao kujua na kudai kuwa labda hospitali ya
mkoa wanaweza wakalijua hilo.
Dk.Moses Jaba amekiri kushindwa kubaini ugonjwa huo kwa
kitaalamu hali iliyomfanya ashindwe kulitolea ufafanuzi ,huku akihaidi
kulifanyia kazi ili aweze kuisaidia jamii pale inapotakiwa.
Ugonjwa wa bengu ( donda tumbo)
umekuwa ukiwaathiri watoto wadogo kwa miaka mingi mkoani Kigoma hali inayotishia hata ukuaji
bora wa
mtoto pindi uchelewapo kupata tiba kwa wakati, idara ya afya ifanye
mazungumzo na jamii ili kulifanyia tafiti ya kitaalamu zaidi ili kupata kinga
na tiba yenye kutambulika nchini.kwa sasa ugonjwa huu hauna kinga zaidi ya
tiba.
Mkoa wa Kigoma upo Magharibi ya pembezoni mwa
nchi ya Tanzania, ambapo
umepakana na nchi nne za jirani ikiwemo Jamhuri ya Watu wa Congo (DRC), Burundi,
Rwanda na Zambia.
Kutokana na mwingiliano wa
ujirani mwema ni rahisi wakazi wa mkoa huo kupata maradhi toka nchi hizo hasa
kutokana na shughuli za kibiashara.
4 comments:
Hata mwanangu anaumwa Leo tupo kigoma
Kwahyo tiba yake kwaujumla ikoje sasa
Mtoto anaeumwa hiyo anakuaje?
Mungu ingilia kati
Post a Comment