Tangazo

January 21, 2014

VIONGOZI TFF WAIWEKEA TAIFA STARS MKAKATI SINGIDA

Makamu wa Rais TFF Taifa,Wallace Kiria (wa saba kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa TFF mikoa mbalimbali hapa nchini wanaohudhuria mafunzo ya utawala,ukaguzi wa taarifa za fedha na maendeleo ya timu ya taifa.Wa sita kulia ni mwenyekiti wa TFF mkoa wa Singida,Baltazar Kimario. Mafunzo hayo yalidhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager ambayo pia inadhamini Timu ya Taifa, Taifa Stars.

###########################

Na Mwandishi Wetu

VYAMA vya soka mikoani,vimetakiwa kuweka mikakati madhubuti itakayosaidia kuwajengea vijana mazingira mazuri ya kuibua vipaji vyao,ili waweze kuendelezwa kwa lengo la kupata timu bora ya Taifa (Taifa stars).

Hayo yanasemwa jana na makamu rais wa TFF taifa,Wallace Kiria,wakati akifungua mafunzo ya siku mbili yaliyohudhuriwa na viongozi wa TFF kutoka mikoani yanayofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Katala Hotel Beach mjini hapa.

Mafunzo hayo yalihusu utawala,ukaguzi wa taarifa za fedha na maendeleo ya soka la vijana na yalidhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager ambayo pia inadhamini Timu ya Taifa (Taifa Stars).

Huu ni mwaka wa pili tangu Kilimanjaro Premium Lager ianze kudhamini Timu ya Taifa na imewekeza zaidi ya Sh Bilioni mbili kila mwaka kwa Taifa Stars.

Kiria alisema vijana kutoka sehemu mbalimbali nchini wenye vipaji vya soka wakiendelezwa,watasaidia kuunda timu bora ya Taifa itakayokuwa na uwezo wa kutoa  ushindani wa kweli na sio ya kusindikiza.

“Watanzania wamechoka au wamechoshwa na mwenendo wa Taifas stars wa kila inaposhiriki mashindano yo yote,inatolewa mapema.Uongozi huu mpya wa TFF,malengo yake ni kuona Taifa stars inayotoa ushindani wa hali ya juu na ikiwezekana ianze kuleta makombe mbalimbali nchini mapema”,alisema.

Aidha,Karia alisema kuwa maandalizi hayo ya kuendeleza vijana hasa under 17,ni kuandaa mapema timu ya vijana ambayo itashiriki mashindano ya bara la Afrika ambayo, Tanzania itaomba mashindano ya mwaka 2019,yafanykie Tanzania.

Kuhusu mafunzo hayo,alisema kuwa ni mwendelezo wa mafunzo yaliyoanza kutolewa Zanzibar ambayo pamoja na mambo mengine,kuwaongezea uwezo viongozi ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

“TFF ya sasa inataka kuwafanya kazi kama mnyororo moja na viongozi/wadau mbalimbali wa soka,ili kufikia malengo tarajiwa kwa ufanisi mkubwa.Tunapaswa tuonyeshe tunaongoza mchezo wa mpira mpya,soka lenye malengo lenye kutoa burudani na kuleta nchini makombe mbalimbali”,alisema.

Wakati huo huo,makamu huyo wa rais,ameitaka mikoa itakayoandaa mikutano ya TFF taifa,iweke utaratibu wa kuandaa wajumbe kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii.

Kwa mujibu wa Karia,TFF taifa,inatarajia kufanya mkutano wake mkuu mkoani Singida Aprili mwaka huu.

No comments: