Mama Salma Kikwete |
Na Anna Nkinda –
Maelezo
Wazazi wenye watoto
ambao wanatatizo la usonji (Autism) nchini wametakiwa kuwapenda, kuwatunza na kuwapa mahitaji yao kama watoto wengine
kwani ni makusudi na mapenzi ya Mwenyezi Mungu kuwapa watoto hao.
Mwito huo umetolewa leo
na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Mama Salma Kikwete
wakati akiongea na walimu, walezi na wazazi wa watoto hao katika Shule ya
Msingi Msimbazi Mseto kitengo cha usonji iliyopo wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Mama Kikwete ambaye pia
ni Mke wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alisema ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu
kuwapatia watoto hao jambo la muhimu ni
kumshukuru na kuacha kujiuliza ni kwa
nini aliwapa watoto wenye tatizo la usonji.
“Ninawapongeza kwa kazi
mnayoifanya na moyo wa huruma na upendo wa kuwatunza watoto hawa, msilalamike na
kuhudhunika bali wapendeni kama watoto
wengine na kuwapatia mahitaji yao”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa WAMA
alisema yeye kama mzazi anaguswa sana na maisha ya watoto hasa wenye mahitaji
maalum ambao ni yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi, walemavu wa
ngozi na viungo.
Kwa upande wa walimu
wanaowafundisha watoto hao aliwapongeza kwa kazi wanayoifanya na kusema kuwa
kazi hiyo ni wito na inahitaji moyo wa ziada hata kama watalipwa malipo kiasi gani hayawezi kuendana na kazi
wanayoifanya.
Akisoma risala ya Chama
cha kuwahudumia watu wenye Usonji (National Association for People with Autism
in Tanzania (NAP-T)) Daniel Longhway alisema chama hicho kinawanachama 41 na
kitengo hicho katika shule ya Msingi Msimbazi Mseto kina wanafunzi 24
wanaohudumiwa na walimu tisa na kinawafuatilia watoto 50 ambao wame maliza muda
wao wa kuwa shuleni na hivi sasa wako majumbani.
Alisema Usonji ni hali
ya udhaifu katika ukuaji wa ubongo ambayo huleta athari kubwa katika mawasiano,
mahusiano ya kijamii na utambuzi.Tatatizo hili ni la dunia nzima na bado hakuna
maelekezo kamili ya chanzo chake wala tiba. Wanaoathirika zaidi ni watoto wa
kiume kuliko wa kike kwa uwiano wa nne kwa moja hii ikiwa na maana kuwa kila
watoto watano wenye usonji wanne ni wa kiume na mmoja wa kike.
“Chama chetu kina
mafanikio mbalimbali ikiwa ni pamoja na muamko wa wazazi kutowaficha watoto
wenye usonji umekuwa mkubwa, vitengo vya kutoa elimu kwa watoto vimeongezeka,
utengemano umekuwa mkubwa kwa watoto waliopo mashuleni pia wazazi na walezi hasa
wenye watoto waliopo mashuleni wanapata ushauri nasaha”, alisema Longhway.
Alizitaja changamoto
zinazowakabili kuwa ni eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo ambako patajengwa chuo
cha ufundi kwa watoto wakubwa wanaomaliza shule ambao hawana mahali pa kwenda,
mabweni ya wanafunzi, madarasa, nyumba za walimu, viwanja vya michezo na
ukumbi, upungufu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
Kutokuwa na usafiri wa kuwapeleka
shuleni na kuwarudisha nyumbani watoto pamoja na kuwapeleka walimu kuwatembelea
wanafunzi majumbania ,kutokuwa na wataalamu wa speech therapy, Physiotherapy na
occupational Therapy, chakula kwa wanafunzi na wanahitaji wasaidizi wawili kwa
ajili ya kuwahudumia wanafunzi.
Mwaka 1997 wizara ya
Elimu na Utamaduni ikishirikiana na wanachama wa NAPA - T walianzisha kitengo
cha watoto wenye usonji katika shule ya msingi Msimbazi Mseto ambacho ni
kitengo mama cha kutoa huduma. Hivi sasa Serikali inavitengo vitano, viwili
vipo Dar es Salaam, viwili Arusha na kimoja Morogoro. Pia kuna vitengo kadhaa
vilivyoendeshwa na watu binafsi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment