Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika mazungumzo na
Balozi mpya wa Marekani nchini Tanzania, Mark Childres, wakati alipofika
Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Juni 9, 2014 kwa mazungumzo na
utambulisho wa balozi huyo. Picha na OMR
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal leo amekutana na Balozi mpya wa Marekani, Mheshimiwa
Balozi Mark Childress ambaye amefika ofisini kwa mheshimiwa Makamu wa Rais kwa
ajili ya kujitambulisha.
Balozi Childress alimueleza Mheshimiwa Mkamu wa
Rais kuwa, Tanzania ni nchi yenye uhusiano maridhawa na Marekani na kwamba
katika kipindi chake kama Balozi atahakikisha uhusiano huu mzuri uliojengwa
unadumishwa na kwamba, nchi hizi mbili zinazidi kuwa na maeneo ya kushirikiana
hasa yanayolenga kuboresha maisha ya watu na kuwapatia maendeleo.
Balozi Childress pia alisema kuwa Tanzania
imekuwa ikitumia kama mfano kufuatia kuonesha mabadiliko ya haraka katika
miradi mbalimbali inayoendeshwa hapa nchini kwa ushirikiano na watu wa Marekani
na akafafanua kuwa, kazi iliyoko mbele ni kuhakikisha kuwa Tanzania inapiga
hatua zaidi na sio kurudi nyuma.
“Mheshimiwa Makamu wa Rais, kila nikipata fursa
ya kukutana na wenzangu tumekuwa tukizungumzia suala la Tanzania kupiga hatua
kwa haraka. Mna mambo mengi yaliyofanyika na kazi iliyopo ni kuendelea kupiga
hatua pasipo kurudi nyuma,” alisema.
Kwa upande wake Mheshimiwa Makamu wa Rais
alimueleza Balozi Childress kuwa, Tanzania ipo katika kipindi ambacho
kinaonesha mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kwamba kazi ya serikali ya
Tanzania ni kuhakikisha kuwa uchumi unakuwa na unasaidia vizazi vya sasa na
vijavyo.
“Mtazamo wetu katika serikali ni kuwa Tanzania
itapiga hatua kubwa katika miaka michache ijayo. Lengo letu ni kutazama kuwa
ukuaji wa uchumi hauwi wa muda mfupi, tunatazama pia maendeleo kwa vizazi
vijavyo.
Kuhusu suala la utunzaji mazingira, Balozi
Childress alisifu hatua za Mheshimiwa Makamu wa Rais hasa katika kazi ya
uhamasishaji upandaji miti na akasema, utunzaji wa mazingira ni jambo la muhimu
ili kuifanya nchi yetu iweze kuendelea na isikabiliane na matatizo yanayotokana
na mazingira kuharibiwa.
“Nakupongeza Mheshimiwa Makamu kwa kazi yako ya
uhamasishaji utunzaji wa Mazingira. Usichoke kufanya hivyo maana unasaidia
dunia,” Balozi Childress alisema.
Imetolewa na :
Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment