Mama Salma Kikwete |
Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Wazazi na
walezi wilayani Lindi mjini wametakiwa kuwekeza katika elimu ya
watoto wao kwa kuhakikisha wanakwenda shule kwa wakati kwani elimu ni
ukombozi wa maisha na kuolewa katika umri mdogo kwa watoto hao hakutawasaidia
kimaisha.
Mwito huo umetolewa jana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa (NEC) wilaya ya Lindi mjini Mama Salma
Kikwete wakati akiongea kwa nyakati tofauti na viongozi wa
Halmashauri kuu ya tawi ya Chama hicho katika matawi yaliyopo kweye kata za
Chikonji, Tandangongoro na Ng’apa wilaya ya Lindi mjini.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mke wa Rais Jakaya Mrisho
Kikwete alisema ni jukumu la mzazi na mlezi kusimamia elimu ya mtoto wake
pamoja na kumpa malezi mazuri kwa kufuata malezi ya zamani yanayoendana
na mila na utamaduni wa mtanzania kwani hivi sasa kutokana na utandawazi
mienendo ya vijana wengi siyo mizuri.
MNEC huyo pia aliwataka watoto waliofika kumsalimia
mara baada ya kumaliza mkutano wake wa ndani na viongozi hao wa CCM kusoma kwa
bidii na kuacha tabia ya utoro kwani elimu pekee ndiyo itakayowakwamua na
hali ngumu ya maisha.
Aidha Mama Kikwete aliwahamasisha viongozi wa
Halmashauri kuu ya tawi ya CCM kujiunga katika vikundi mbalimbali vya maendeleo
na kuandika maandiko ya kibiashara ili wapate mkopo kutoka
Serikalini na kuweza kufanya miradi kama ufugaji wa kuku, mamalishe,
ufundi seremala, kwa kujishughulisha na biashara hizo watakuwa
wamejikwamua kiuchumi.
“Mkijiunga katika vikundi vya ujasiriamali mtaweza
kukopa fedha kutoka Serikalini jambo la muhimu mkumbuke kuwa fedha hizi
hampewi bure mnatakiwa kuzirudisha ili na wenzenu waweze kukopa”,
alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wa Afya aliwahimiza kina mama
kujitokeza kwa wingi kupima afya zao ikiwemo saratani ya matiti na shingo
ya kizazi ambayo inatibika ikiwa itagundulika mapema mgonjwa atapata
matibabu na kupona.
“Hivi sasa
kuna maradhi mengi ikiwemo saratani ya matiti na shingo ya kizazi
msiogope kwenda kupima na kujua afya zenu. Nanyi kinababa wahimize wake
zenu wakapime ugonjwa huu, mkiona dalili wawapeleke Hospitali
mapema kwani ugonjwa huu unatibika kama mgonjwa atawahi
mapema kupata matibabu”, alisisitiza.
Alimalizia
kwa kuwataka viongozi hao kuonyesha mfano kwa wananchi kwa kujenga nyumba bora
za matofali ya kuchoma na kuezeka kwa bati na siyo za miti kwani moja ya sera
ya CCM ni kuwahamasisha wananchi kutunza mazingira na kutokukata
miti hovyo.
Akiwa katika Kata ya Chikonji MNEC huyo alikagua mradi
wa maji wa Kwamtokama na kujionea maendeleo ya mradi huo ambao
ukikamilika utawanufaisha wananchi wapatao elfu saba kutoka vijiji
vya Jangwani, Nanyanje , Chikonji Kusini na Kaskazini.
Mama Kikwete ambaye ni mjumbe wa NEC Taifa kupitia
wilaya ya Lindi mjini alikutana na viongozi hao wa Halmashauri kuu ya matawi ya
CCM katika matawi ya Chikonji Kusini na Kaskazini,Nandambi, Kilolombwani
na Cheleweni kwa ajili ya kuimarisha kazi za chama hicho ikiwa ni pamoja na
kufanya vikao vya ndani na viongozi na kuangalia utekelezaji wa ilani ya
uchaguzi ya mwaka 2010
Mwisho.
No comments:
Post a Comment