Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KAMPUNI inayokwenda kwa jina la Watch Film Company
Ltd, ipo mbioni kukamilisha filamu yake ya kwanza itakayojulikana kama ‘Lifti’ inayotengenezwa
kwa umakini wa hali ya juu.
Adam Mchomvu, mmoja ya wasanii walioshiriki katika filamu ijulikanayo kwa jina la Lifti.
Filamu hiyo itakuwa ya kwanza tangu kampuni hiyo
iliposajiliwa kwa ajili ya kujihusisha na kazi mbalimbali za sanaa, ikiwamo
filamu hapa nchini, huku ikiwa na mipango lukuki.
Akizungumza leo asubuhi, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kampuni
hiyo, Athuman Kilo, maarufu kama 'Dr Kilo' alisema kuwa wamejipanga imara kuteka
soko la filamu hapa nchini.
Alisema mashabiki wa filamu watapata burudani kamili pamoja
na kujifunza kutoka kwenye filamu hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa inaandaliwa kwa
utulivu wa hali ya juu.
“Hii ni kazi ya kwanza ambayo tunaamini itaanza vyema
kwasababu vichwa vimetulia na kuangalia namna gani akili zetu zinafanikisha
kutoa kazi nzuri.
“Naomba wadau wote wakae mkao wa kula kuisubiri filamu hii
ambayo kwa sasa ipo katika hatua za mwisho kabisa kukamilika na itakuwa moto wa
kuotea mbali,” alisema Dr Kilo.
Baadhi ya watu walioshiriki katika filamu hiyo ni pamoja na
Adam Mchomvu, Khamis Said, Sudi Ally ‘Akui’, Sadiki Manyeko, Jazzmin, Tatu Kingwande,
Mzee Jengua na wengineo.
No comments:
Post a Comment