Na Anna Nkinda –
Maelezo,
Lindi
Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya
Lindi mjini Mama Salma Kikwete amewataka vijana kuwa na msimamo na kutokubali
kutumika katika vurugu zinazohatarisha amani na usalama wa nchi.
Mama Kikwete ambaye ni
Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alitoa rai hiyo hivi karibuni wakati akifungua
shina la vijana wakeleketwa la kikundi
cha Zahanati Kempu lililopo Kata ya Rasibura wilaya ya Lindi mjini.
Alisema vijana wengi
hawajui Historia ya nchi hivyo basi baadhi ya watu wasio na nia njema
wanaitumia nafasi hiyo kuwarubuni na kuwashawishi kufanya vurugu zinarudisha
nyuma maendeleo ya eneo husika.
“Msikubali mkoa wetu wa Lindi kuwa kichaka cha majaribio na kutumika katika vurugu, kuweni na msimamo
wa kuitetea amani yetu kwani mkifanya
vurugu matatizo yanapotokea ninyi ndiyo mnaoangamia na hao waliowashawishi wanawakimbia”.
Kama atakuja mtu hapa
na kuwashawishi kwa ajili ya shughuli za
maendeleo ni sawa hakuna atakayezuia tunahitaji kuwa na maendeleo katika mkoa
wetu, lakini kuwashawishi ili mfanye vurugu na kuharibu vichache tulivyonavyo
msikubali”, alisema Mama Kikwete.
Aidha MNEC huyo
aliwasisitiza vijana kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili waweze kujiletea
maendeleo yao na ya mkoa huo kwa kuwa vijana ndiyo wanaotegemewa na ni nguvu kazi ya Taifa.
Akisoma taarifa ya
kikundi hicho Hidaya Chivii ambaye ni Mtunza fedha alisema kikundi hicho kilianzishwa
tarehe 5/7/2014 kikiwa na wanachama 23 kati ya hao wanaume ni 18 na
wanawake ni watano.
Chivii alisema
madhumuni ya kuanzishwa kwa kikundi hicho ambacho kinajihusisha na kazi ya kuendesha
pikipiki (bodoboda) kwa upande wa wanaume na ususi kwa upande wa
wanawake ni kujikwamua na hali ngumu ya maisha na kuweza kujiendeleza.
“Waendesha pikipiki tunakabiliwa na changamoto ya kunyang’anywa pikipiki
hasa ifikapo wakati wa uchaguzi kwani wamiliki walio wengi ni wanachama wa chama
cha Wananchi (CUF) na sisi ni wanachama
wa CCM au wanatupa pikipiki zao kwa masharti magumu yakiwemo ya kukipigia kura
chama chao”, alisema Chivii.
Alizitaja changamoto
nyingine zinazowakabili kuwa ni pamoja
na kutokuwa na vitendea kazi vyao wenyewe na kutokupata mafunzo ya ujasiriamali.
Wakati huo huo Mama
Kikwete alifanya vikao na viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi ya CCM katika
matawi ya Kilimahewa na barabara ya Kawawa na kuwahimiza wajumbe kuendelea kushikamana na kuwa kitu kimoja ili waweze
kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Akiwa katika tawi la
Kilimahewa lililopo Kata ya Mwenge aliwapokea vijana wanne kutoka chama cha Wananchi
(CUF) ambao walijiunga na CCM.
Mama Kikwete ambaye ni
mjumbe wa NEC Taifa kupitia wilaya ya Lindi mjini yupo wilayani humo kwa ajili ya kuimarisha kazi za chama hicho
ikiwa ni pamoja na kufanya vikao na viongozi na kuangalia utekelezaji wa ilani
ya uchaguzi ya mwaka 2010.
No comments:
Post a Comment