Tangazo

December 25, 2014

Vijiji 45 Mkoani Mara kupatiwa umeme

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (pichani), amesema kuwa  vijiji  vipatavyo  45 vilivyopo katika mkoa wa Mara vinatarajiwa kuunganishiwa na  huduma   ya umeme kupitia Wakala  wa Nishati  Vijijini (REA).

Profesa Muhongo aliyasema hayo  katika  ziara yake ya siku sita katika mkoa wa Mara lengo likiwa ni kukagua na kuzindua miradi ya umeme vijijini inayosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini  (REA) awamu ya  pili   kwa kushirikiana na  Shirika la  Umeme  Nchini (Tanesco).

Profesa Muhongo alisema  ziara  yake  iliyohusisha   wilaya za  Musoma Vijijini, Tarime, Rorya, Bunda na Serengeti ililenga pia kubaini na kukagua mahitaji ya umeme katika  wilaya hizo  ili vijiji vilivyokosa  umeme kwenye awamu ya  pili  viingizwe katika awamu  nyingine ya umeme vijijini.

Alieleza kuwa Wizara imekuwa ikisambaza umeme katika kila Mkoa na Wilaya za Tanzania kwa awamu kulingana na mahitaji na idadi ya watu katika maeneo hayo.
Alisema kwa sasa umeme unaosambazwa upo katika awamu ya pili ambapo awamu ya tatu itakuja baada awamu ya pili kumalizika. 

Alisema   vipaumbele  vinavyotolewa katika uunganishaji wa umeme  vijijini Profesa Muhongo  alitaja kuwa ni maeneo yenye  huduma muhimu   za kijamii kama  vile  mashule, vituo  vya afya, makanisa, misikiti, ofisi za vijiji na kata, na sehemu zenye miradi ya maji.

“Lengo  letu  kuu kwanza ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma za jamii kwa urahisi na baada ya  kuboreshwa kwa huduma hizo tunakwenda kuwaunganishia  umeme wananchi mmoja mmoja, ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha  maisha  ya wananchi  yanaboreshwa kupitia nishati ya umeme”, alisema  Profesa Muhongo.

 Profesa Muhongo aliongeza kuwa ili nchi yoyote duniani iweze kupiga hatua katika ukuaji wa uchumi wake, inahitaji  nishati ya umeme na kuongeza kuwa kwa kutambua hilo serikali  imeanza kwa upande wa vijijini ili wananchi hao waweze kujiingizia  kipato kupitia ajira za kujiajiri.

Alifafanua kuwa wananchi  wa vijijini kupitia  nishati ya umeme wanaweza kuwekeza kupitia mashine  za kusaga nafaka, kukamua mafuta, kuhifadhi  vyakula  vya kuuza kwenye majokofu  na kujipatia fedha na kuongeza kuwa itapunguza wimbi  la watu  kukimbilia mjini  kutafuta ajira.

Wakati huohuo   Mwenyekiti  wa kijiji  cha  Bukabwa Thomas Makwera alisema kuwa  wananchi wa  kijiji chake wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kutokuunganishiwa  umeme kwa muda mrefu hali inayopelekea maendeleo  ya kijiji hicho kudorora.

Hata  hivyo  aliongeza kuwa  wakandarasi  wamekuwa wakionekana wakisimika  nguzo za umeme hali inayotia  hamasa kwa wananchi ya kutaka kujua ni lini wataunganishiwa na huduma ya umeme.

Akijibu swali la Mwenyekiti huyo Profesa Muhongo alimtaka mkandarasi anayesimamia mradi huo kutoka kampuni ya Derm Electrical Huseni  Ayubu kutoa ufafanuzi ambapo mkandarasi huyo alieleza kuwa  kazi ya kusimika nguzo  pamoja na  kuunganisha  umeme inatarajiwa kukamilika mapema Februari mwakani.

Naye Profesa Muhongo aliwataka wanakijiji wa Bukabwa kuchangamkia  fursa ya  kuunganishiwa umeme kwa gharama  ya shilingi  27,000. wakati mradi wa umeme ukiwa bado upo katika kijiji chao.

Alisema kuwa  lengo la  utekelezaji wa miradi ya umeme  vijijini kupitia Wakala  wa Nishati Vijijini (REA)  ni kuhakikisha kuwa vijiji vyote ambavyo umeme umepita lakini  havijaunganishiwa  vinaunganishiwa ili  kuhakikisha  vijiji vyote  vilivyopitiwa umeme  vinapata  umeme kwa  kufuata utaratibu huo.

No comments: