Tangazo

January 11, 2015

FORUMCC YATOA MREJESHO WA YALIYOJIRI KWENYE MKUTANO WA KIMATAIFA WA MABADILIKO YA TABIANCHI DUNIANI COP20 ULIOFANYIKA DESEMBA MWAKA JANA JIJINI LIMA PERU

Taasisi isiyo ya kiserikali ya ForumCC imetoa mrejesho wa mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabia nchi  duniani wa COP20 uliofanyika mwezi Desemba jijini Lima nchini Peru mwaka jana.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijni Dar es salaam Afisa Miradi wa ForumCC Fazal Issa  amesema  wanachama wa mkutano huo wamekubaliana kusaini mkataba mwaka huu jijini Paris Ufaransa wenye lengo la kupunguza gesi joto duniani na kusaidia upatikanaji wa rasilimali fedha na teknolojia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi  duniani kwa sasa.
 Afisa Miradi wa ForumCC Fazal Issa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano huo

Afisa Miradi huyo amesema katika mkutano huo wa Peru kulikuwa na makundi mbalimbali kutoka kila pembe ya dunia yakiwamo kundi la nchi za Afrika ambazo ndizo zimekuwa muathirika mkubwa wa mabadiliko ya tabianchi. Mkutano huo pia ulizikutanisha nchi 72 zilizokwenye kundi la nchi zilizoendele na ambazo ni chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa kuwa na viwanda vinavyozalisha hewa ukaa na kuongeza joto duniani.
Aidha Afisa huyo amesema kuwa  kulikuwa na kundi kutoka nchi za Bara la Asia na kundi la nchi za  visiwa  pamoja na makundi mengine ya wanaharakati wa mazingira ambao walipigana kuzibana nchi zilizoendelea kupunguza uharibifu na kutoa pesa  kwa nchi zilizoathirika na zinazoendelea kuathirika na mabadiliko ya tabianchi. 
 
Amesema nchi zinazoendelea ikiwamo  Tanzania  walikuwa na msimamo mmoja ambao ni kupunguza gesi joto duniani , na kuzitaka nchi zenye viwanda kutoa fedha zaidi katika mfuko wa pamoja wa mazingira katika kujenga uwezo kwa nchi maskini na zinazoathirika kupunguza na kumaliza changamoto za mabadiliko ya tabianchi

“Zinahitajika dolla bilioni 100 kwa mwaka katika kushughulikia mabadiliko ya tabianchi duniani na kiasi kilichochangwa ni  dolla bilioni 10 sawa na asilimia 10% tu ya fedha ambazo  zinazohitajika, Utaona hapo ni kwa kiasi gani nchi zilizoendelea  zinahitajika kuchangia mfuko huu” anasema Fazal.
Mwezeshaji kutoka Youth Can Tanzania, Rahma Mwita, akifafanua jambo wakati wa mkutano huo
 Afisa Habari ForumCC, Tajiel Urioh akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano huo
 Waandishi wa habari wakifuatilia taarifa ya mrejesho wa yaliyojiri kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP20 uliofanyika Peru mwishoni wa mwaka jana.


Naye katibu mkuu wa asasi ya kiraia ya (Youth-CAN)  Justine Mponda amesema wao kama vijana wapambanaji wa mazingira hapa nchini wameshiriki katika mkutano huo wa COP 20 Peru kwa lengo la kujifunza  zaidi kutoka kwa vijana wenzao duniani walioshiriki katika mkutano huo wa mabadiliko ya tabianchi.

“ tunajihusisha  na kutoa elimu ya mabadiliko ya tabianchi kwa jamii  juu ya athari ya mabadiliko ya tabia nchi, pamoja na  kuwashawishi vijana nchi  juu ya  kukabiliana  na mabadiliko ya tabia nchi. Pia  kufikisha madai na vilio vya vijana nchini  waathirika wa mabadiliko ya tabia nchi kwa serikali na taasisi za kimataifa kwa utatuzi zaidi”

Taasisi  hiyo ya Youth –CAN  ina lengo  la kufanya kampeni  nchini  kabla ya mkutano wa mabadiliko ya tabianchi wa mwaka huu  Paris Ufaransa. Kmpeni yenye lengo la kuwafikia watu zaidi ya milioni 1 nchini ambao ni makundi ya vijana, wazee, wanawake na  wanahabari na katika kampeni hiyo watatumia  usafiri wa  baiskeli katika ile hali ya kuepuka kuchafua mazingira.

Mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi maarufu kama COP20 ulifanyika jijini Lima nchini Peru kuanzia Desemba mosi  na kumalizika Desemba 14 mwaka 2014 ambao ulikuwa na malengo  ya kujadiliana na kupitisha maadhimio ya mkataba ambao utaenda kusainiwa  mwishoni mwa mwaka huu jijini Paris Ufaransa.

No comments: