Tangazo

January 8, 2015

Serikali yatumia Shilingi Bilioni 881 katika Mradi wa REA Awamu ya Pili

Mmoja wa wakazi kutoka katika Kata ya Nkoma iliyopo  Wilayani Meatu mkoani Simiyu  (kushoto) akitoa neno la shukrani mbele ya  Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kulia) baada ya Wizara ya Nishati na Madini  kusambaza umeme  katika kata hiyo kupitia  Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Pili. Kijiji cha Nkoma ni moja ya vijiji  170  vilivyopo mkoani Simiyu vilivyofaidika na mradi wa umeme  vijijini  unaotekelezwa na  REA Awamu ya Pili.
Mtaalamu kutoka  Kampuni ya  LTL (PVT) LTD inayosambaza miundombinu  ya umeme vijijini katika Wilaya ya Maswa  chini ya mradi wa REA Awamu ya PIli  Michael  Marenye (kulia), akifafanua hatua iliyofikiwa ya uunganishaji wa umeme  katika  Kata ya Balyanaga mbele  ya  Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) mara Waziri  Muhongo alipofanya mkutano  na wakazi wa Kata Balyanaga ili  kusikiliza kero zao.

Na Greyson Mwase, Maswa.

Meneja Utaalamu Elekezi  kutoka  Wakala wa Nishati  Vijijini (REA) Gissima Nyamohanga amesema kuwa serikali imetumia shilingi bilioni 881 katika mradi wa kusambaza umeme  vijijini  unaotekelezwa na  Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Pili.

Nyamohanga aliyasema hayo kwenye  sherehe za uzinduzi wa mradi wa umeme vijijini unaofadhiliwa na REA uliofanyika katika kata ya Shishiyu wilayani Maswa mkoani  Simiyu.

Alisema kuwa Mradi wa  REA  Awamu ya Pili  utaiwezesha  idadi ya  vijiji  vilivyounganishwa   na umeme 3734  kati ya vijiji 15,180 ambayo ni asilimia 24.6 kufikia vijiji 5,234 ambayo ni asilimia 34.5 ifikapo  mwezi Juni mwaka huu.

Aliongeza kuwa mradi wa REA Awamu ya Pili wa miaka miwili  ulioanza mwaka 2013, lengo lake lilikuwa  ni kuhakikisha kuwa vijiji vyote Tanzania vinapatiwa umeme hivyo kuboresha maisha  ya wananchi na kukuza uchumi wa nchi.

Akielezea mchango wa mradi wa usambazaji wa umeme  vijijini  unaotekelezwa na  REA katika kuboresha maisha  ya wananchi Nyamohanga alisema kuwa awali wananchi  wote walikuwa wakilipa  shilingi  467,000 kama  gharama ya kuunganishiwa umeme ambayo ilikuwa ni kubwa na kupelekea  wananchi wachache wenye uwezo kuwa na  nishati ya  umeme huku  ikiacha kundi kubwa la wasio na uwezo kuishi  gizani.

Alisema kuwa katika Awamu ya Kwanza ya REA gharama za uunganishaji wa umeme  zilishuka kutoka  shilingi 467,000 hadi shilingi 177,000 na kuongeza kuwa katika kuhakikisha  kila mwananchi anakuwa na uwezo wa kuunganishiwa umeme  Serikali iliamua  kubeba  gharama zote kupitia REA Awamu ya Pili na wananchi kutakiwa kuchangia shilingi 27,000 tu kama kodi ya ongezeko (VAT)
Alieleza kuwa mara baada ya kumalizika  kwa Awamu ya Pili ya REA, viongozi wataainisha  vijiji ambavyo havijapata  umeme REA Awamu ya Pili, ambapo vitajumuishwa katika mradi wa REA Awamu ya Tatu.

Nyamohanga alieleza michango mingine kuwa ni  kufungua  fursa za ajira na uwekezaji kwa vijana wa kitanzania, ufaulu  kuongozeka kwa shule za sekondari na kuboreshwa kwa huduma za afya.

“Kwa mfano kwa shughuli za kiuchumi bei ya kusaga  debe la mahindi ilikuwa ni shilingi 1,000 itashuka  hadi shilingi  500 kutokana na kwamba mashine za kusaga zitakuwa zinatumia  umeme badala ya  dizeli kama zamani,” alisema Nyamohanga

Wakati huohuo Meneja wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) Kanda ya  Ziwa Mhandisi  Joyce Ngahyoma akielezea jinsi ya kuunganishwa na huduma ya umeme kwa wananchi wa vijiji  vilivyopitiwa na mradi wa REA  Awamu ya Pili alisema kuwa wananchi wanaoishi  mita 30 karibu na miundombinu ya umeme wataunganishiwa kwa shilingi  27,000 na kuwataka kuchangamkia fursa hiyo kwa kuboresha makazi yao.

Alisema kwa wananchi wenye  nyumba zenye  vyumba viwili na vioski hawahitaji kufunga mfumo wa umeme kwenye nyumba zao (wiring) badala yake watashauriwa kununua kifaa maalumu kijulikanacho kama “UMETA” (Umeme Tayari) kinachoweza kutumika kama mfumo kwa kuwa na uwezo wa kuunganisha taa mbili na vifaa vingine  kama  vile jiko, friji na pasi.

Aliendelea kusema kuwa kifaa hicho kinachouzwa kwa gharama ya shilingi 37,000 kitakuwa ni mali ya mteja na endapo atahama makazi basi atakuwa huru kuhama pamoja na kifaa chake.

No comments: