Na Anna Nkinda –
Maelezo
TAASISI ya
Wanawake na Maendeleo (WAMA) imepongezwa kwa kazi inayoifanya ya kuhakikisha watoto wa kike ambao ni yatima na wanaoishi
katika mazingira hatarishi wanapata elimu sawa na watoto wengine.
Pongezi hizo zimetolewa
leo na Mke wa Rais wa Shirikisho la Ujerumani Mama Daniela Schadt (pichani), wakati
akiongea na wafanyakazi wa WAMA
alipozitembelea ofisi za Taasisi hizo zilizopo jijini Dar es Salaam.
Mama Schadt ambaye ni
Mke wa Rais Joachim Gauck alisema watoto
hao bila ya kupata ufadhili wa masomo wasingepata elimu lakini kutokana na
ufadhili huo wanapata elimu ambayo itawasaidia hapo baadaye na hivyo kuinua
hali ya maisha yao na familia zao na nchi kuweza kupata wataalamu wa aina
mbalimbali.
Kuhusu suala la afya
Mama Schadt aliishauri Taasisi hiyo kuendelea
kuwahimiza wanaume kuwapeleke wake zao ambao ni wajawazito katika vituo vya
afya ili wote wawili waweze kupima na kujua kama wamepata maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) au la.
“Baada ya kupima na
kugundulika kuwa na maambukizi ya VVU watapewa
dawa za kupunguza makali ya Ugonjwa huo na hivyo kumkinga mtoto aliyepo tumboni ili asizaliwe
akiwa na maambukizi pia na wao wataweza kujikinga na kutopata maambukizi mapya”, alisema Mama Schadt.
Kwa upande wake Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete alimshukuru Mama Schadt kwa kutembelea ofisi hiyo na kumueleza
kwamba aliamua kuanzisha Taasisi ya WAMA
ili aweze kutoa mchango wake katika kuboresha hali ya maisha ya wanawake nchini.
Alisema wamewawezesha
wanawake kiuchumi kwa kuwapa elimu ya ujasiriamali katika program ya Mwanamke
Mwewezeshe ambayo kwa muda wa miaka mitatu imeweza kuwafikia wanawake wapatao 60,000 katika mikoa ya Dar es
Salaam Lindi na Pwani.
Mama Kikwete alisema, “Licha
ya kutoa ufadhili wa masomo kwa watoto wa kike, tunafanya kazi ya kuimarisha
afya ya wanawake na watoto kwa kutoa elimu ambayo inawawezesha kuzuia
maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi, kuwahimiza ili waweze kushiriki katika upimaji wa saratani za shingo ya kizazi na
matiti pia tumejenga uelewa kwa watoto
wa shule ili waweze kujizuia na mimba za utotoni na maambukizi ya HIV”.
Wakati huo huo Mama Schadt
na Mwenyeji wake Mama Kikwete walitembelea Hospitali ya CCBRT na kujionea kazi
inayofanywa na Hospitali hiyo ya kuwahudumia wagonjwa ambao wengi wao ni wahitaji
wakiwemo wanawake na watoto.
Akiwa Hospitalini hapo Mama
Schadt alisema wataendelea kushirikiana na CCBRT kwa kuboresha utoaji wa huduma
za afya.
Naye Mama Kikwete
alisema nchi za Ujerumani na Tanzania ni washirika wa Hospitali ya CCBRT ambayo
ni maalum kwa ajili ya kuwasaidia watanzania, wanawake na watoto wenye mahitaji
maalum kama walemavu wa miili na ngozi ambao
wanasaidiwa bure.
“Kuna tatizo la Fistula
ugonjwa ambao ni mgumu na unamdhalilisha mwanamke na kumpotezea matumaini lakini hivi sasa
kuwepo kwa Hospitali hii kumewapa wanawake
matumaini mapya , tatizo la Fistula linatokana na mwanamke kupata
uchungu wa muda mrefu wakati wa kujifungua kitendp kinachosababisha kibofu cha mkojo kupasuka”.
Lakini wao wanaweza kuchukulia ugonjwa huu kuwa ni tatizo
lingine kumbe mgonjwa wa Fistula anaweza
kutibiwa, akapona na kurejea katika hali yake ya kawaida”, alisema Mama Kikwete.
Serikali ya Ujerumani
ni mmoja wa washirika wa miaka mingi wanaotoa huduma za Afya katika Hospitali
hiyo na hivi sasa fedha nyingi wanaelekeza
katika ujenzi wa jengo la wazazi .
Wakiwa Hospitalini hapo
walitembelea wodi ya watoto waliofanyiwa upasuaji wa mdomo sungura, waliongea
na wanawake wanaosubiri na waliofanyiwa upasuaji wa ugonjwa wa fistula, waliona
utengenezwaji wa miguu bandia na kujionea ujenzi wa jengo la wanawake pia
waliwasalimia wagonjwa waliofika
kutibiwa.
Mama Schadt ameambatana
na mumewe Rais Joachim Gauck aliyepo nchini kwa ajili ya ziara ya kikazi ya
siku tano.
No comments:
Post a Comment