Tangazo

December 5, 2016

MFUKO WA LAPF KWA MARA NYINGINE KINARA WA UTUNZANI WA MAHESABU NCHINI

 Mkurugenzi wa Fedha wa Mfuko wa LAPF, John Kida (katikati mwenye tuzo), akiwa na wafanyakazi wenzake baada ya kutunukiwa tuzo ya Utunzaji Bora wa Mahesabu Dar es Salaam juzi. Kushoto ni Meneja Masoko na Mawasiliano wa LAPF, James Mlowe.
 Mgeni rasmi katika hafla hiyo akisoma hutuba kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), Profesa Isaya Jairo na katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa NBAA, Pius Maneno.
 Mkurugenzi Mkuu wa NBAA, Pius Maneno (kushoto), akimpongeza Mkurugenzi wa Fedha wa Mfuko wa LAPF, John Kida baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo. Katikati ni Mwenyekiti wa Bodi NBAA. Profesa Isaya Jairo.
 Wapiga picha za habari wakiwa tayari kwa kazi.
 Wafanyakazi wa Mfuko wa LAPF wakipita meza kuu baada ya kutunukiwa tuzo hiyo.
Washindi wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi na viongozi wa NBAA.

Na Dotto Mwaibale

MFUKO wa Pensheni wa LAPF, umetunukiwa tuzo ya kuwa kinara katika utunzaji  wa mahesabu dhidi ya mifuko mingine ya hifadhi ya jamii nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam juzi kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Elyudi Sanga baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi wa Fedha wa mfuko huo, John Kida, alisema kwao ni mafanikio makubwa kwa kupata tuzo hiyo.

"Tunatumia njia za kisasa ya utunzaji wa mahesabu huku tukifunga mahesabu yetu kwa wakati jambo linalotupa fursa ya kuweka sawa mambo yetu ya mahesabu" alisema Kida.

Alisema wamekuwa wakifunga mahesabu yao kwa kiwango cha kimataifa ndio maana wamekuwa wakiibuka washindi mara nyingi.

Kida alisema kuwa ushindi huo ni wa mara ya nane tangu kuanzishwa kwa utoaji wa tuzo hizo mwaka 2008.

Meneja Masoko na Mawasiliano wa LAPF, James Mlowe, alisema kuwa wanachama wao wanatakiwa kuendelea kuwa na imani na mfuko wao na kuwa fedha zao zipo kwenye mikono salama.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), Pius Maneno, alisema makampuni na taasisi 56 zilishiriki katika mashindano hayo kwa  mwaka huu ambapo waligawanywa katika makundi 12 kulingana na huduma wanazozitoa.

Alisema tuzo hizo zina lengo la kuongeza uwazi na uwajibikaji katika suala zima la mahesabu na kuhakikisha viwanago vya kimataifa vinazingatiwa katika utunzaji wa mahesabu.

Aliwataka wahasibu nchini kuandaa taarifa bora za fedha ili kuboresha hesabu za mashirika na makampuni na kuongeza uwazi katika shughuli zao.

Tuzo hizo ziliandaliwa na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) na zilitolewa juzi katika Kituo cha Taaluma ya Uhasibu (ACP) kilichopo Bunju nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

No comments: