Na Jumia Travel Tanzania
Je, unafahamu kwamba umebaki takribani mwezi mmoja mpaka kufikia sikukuu ya Pasaka? Umejiandaa vya kutosha katika kusherehekea au unasubiria mpaka zibakie siku chache ndio uanze maandalizi?
Kwa watanzania wengi suala la kuweka mipango kwa ajii ya mambo yajayo limekuwa ni changamoto kubwa kutokana na sababu mbalimbali wanazozifahamu wenyewe. Jumia Travel inakushauri kuzingatia yafuatayo ili kuondokana na presha ya maandalizi ya siku za mwishoni ya sikukuu ya Pasaka ambayo husherehekewa kuanzia siku ya Ijumaa kuu mpaka Jumatatu duniani kote.
Anza kufikiria kuhusu Pasaka na kujiandaa
Kama unaona mwezi mmoja uliobaki mpaka ifike Pasaka bado ni mapema kujipanga basi nakushauri ubadili hayo mawazo. Kutokana na kuwa na shughuli nyingi zinazotukabili kila siku, muda huwa hautoshi kwenye kila jambo siku zote. Anza sasa kwa kuifikiria siku hiyo, ninaamini utapata picha kamili ya namna utakavyoisherehekea.
Andaa bajeti mapema
Bila shaka lazima kuna gharama zitakazohusika katika kusherehekea siku hizo nne za mapumziko ya sikukuu hii. Muda ulionao sasa hivi unatosha kabisa kukaa chini, kutafakari na kujua ni kiasi gani kitatumika. Ukipanga na kujua mapema itakusaidia kutenga hiyo bajeti pembeni na kuendelea na shughuli zako kama kawaida bila ya kuhofia kuhusu kufurahia mapumziko hayo na wapendwa wako.
Weka utaratibu wa kujua ni siku ngapi zimebakia kabla ya sikukuu
Tunafahamu kwamba ni watu wachache wenye uwezo wa kukumbuka vitu kwa kutumia vichwa vyao bila ya kunakili sehemu. Buni mbinu bora ya kukufanya uweze kutambua ni siku ngapi zimebaki kabla ya Pasaka kufika. Hii itakusaidia kufuatilia kwa ukaribu zaidi kujua malengo na mipango uliyojiwekea inakamilika ndani ya wakati.
Fahamu namna utakavyosherehekea
Unaweza ukawa una bajeti ya kutosha lakini usiwe na mawazo ya namna utakavyoisherehekea Pasaka. Ili kuifanya siku hiyo iwe ya kuikumbuka zaidi lazima kuwe na utofauti kidogo wa namna itakavyokuwa tofauti na unavyofanya siku zote au mara ya
mwisho. Je utasherekea nyumbani pamoja na familia, ndugu au marafiki? Au kama utasafiri basi panga mapema kwa kuingia kwenye tovuti ya Jumia Travel kujua sehemu utakazokwenda.
Shirikisha watu wako wa karibu kupanga namna ya kusherehekea
Suala la kupanga namna ya kufanya jambo fulani hutofautiana kutokana na utofauti wa vipato baina ya mtu mmoja na mwingine. Ukiwa na kipato kikubwa inakupatia fursa kubwa ya kuwa na machaguo mengi zaidi ya kufanya jambo fulani. Lakini hata ukiwa na kipato kidogo haimaanishi kuwa hauwezi kufanya jambo la utofauti, ni suala la ubunifu tu. Hivyo basi jaribu kushirikisha watu wa karibu yako kama vile, familia, ndugu, marafiki au majirani zako ili kupata mawazo mengi na tofauti.
Fikiria kuipamba nyumba yako kunogesha sikukuu
Unaweza kujijengea utamaduni wa kuipamba nyumba yako kila ifikapo sikukuu kubwa ndani ya mwaka, Pasaka inaweza kuwa mojawapo. Unaweza kushirikiana na familia yako, mke na watoto (kama unao) ili kupata mawazo tofauti. Inawezekana watoto wakawa na mawazo mazuri zaidi ya kuipamba nyumba ili kupendezesha shamrashamra za sikukuu hiyo.
Fanya manunuzi mapema
Baada ya kukamilisha mambo yote itakuwa ni vizuri endapo utafanya manunuzi mapema ili kuepukana na pilikapilika za siku za mwishoni. Vitu kama vile vyakula, vinywaji, nguo pamoja na mapambo ni vema vingefanyika mapema kabla ya bei kupanda na watu kufurika madukani. Unaweza kujikuta unaokoa gharama, muda na usumbufu ambao hujitokeza siku za mwisho kwa sababu watu wengi hufanya hivyo.
Mwezi mmoja sio mwingi kama unavyofikiria, liwezekanalo leo lisingoje kesho. Watu wengi hujikuta hawafurahii mapumziko ya sikukuu zao kwa kudharau maandalizi ya mapema.
No comments:
Post a Comment