Tangazo

June 23, 2017

AKINAMAMA WALIMA NYANYA KINYEREZI DAR WAJIFUNZA KILIMO CHA UYOGA

Mafunzo kwa vitendo. Akinamama wa Kinyerezi Green Voices wakiweka udongo kwenye mifuko kama maandalizi ya kilimo cha uyoga.

Mafunzo ya nadharia: Mkufunzi wa kilimo chau yoga wa kikundi cha Bunju Tunza Women, Bi. Esther Chiombola, akitoa mafunzo kwa wanakikundi wa Kinyerezi Green Voices waliotembelea mradi wa akinamama wa Bunju kwa nia ya kubadilishana uzoefu.
Mshiriki kiongozi wa kikundi cha akinamama walima uyoga Bunju, Bi. Magdalena Bukuku, akimkabidhi Dkt. Sophia Mlote kitabu cha namna ya kulima uyoga.

Mkufunzi wa kilimo chau yoga, Bi. Esther Chiombola, akiwapatia vipeperushi washiriki wa mafunzo hayo ya siku moja.
Akinamama wa kikundi cha Kinyerezi Green Voices wakipita kwenye banda (shamba) la uyoga walipokwenda hivi karibuni kwa mafunzo ya siku moja ya kubadilishana uzoefu.


AKINAMAMA wanaojishughulisha na kilimo cha nyanya, spinachi, kabichi na mapapai kutoka Kinyerezi jijini Dar es Salaam wameamua kujifunza pia kilimo cha uyoga kutoka kwa wenzao wa Bunju ikiwa ni hatua ya kuongeza fursa ya ujasiriamali pamoja na kubadilishana uzoefu.

Wakiongozwa na Dkt. Sophia Mlote, akinamama hao wa kikundi cha Kinyerezi Green Voice wameamua kuchukua hatua hiyo katika awamu ya pili ya kutekeleza Mradi wa Green Voices unaolenga kuwawezesha wanawake kujihusisha na shughuli za kiuchumi zinazoendana na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na uhifadhi wa mazingira.

Ziara hiyo ya mafunzo ya siku moja ilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita ikiwahusisha akinamama 13 wa kikundi hicho cha Kinyerezi ambao wanashiriki kilimo hai katika maeneo yao kwa kutumia mabanda maalum ambapo kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita wameweza kunufaika na bidhaa wanazozalisha.

Awamu ya pili ya mradi huo wa Green Voices imeanza mwezi Aprili 2017 na itaishia Aprili 2018, ambapo mradi huo unafadhiliwa na taasisi inayojihusisha na maendeleo ya wanawake wa Afrika, ijulikanayo kama Foundation for Women of Africa inayoongozwa na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, María Teresa Fernández de la Vega.

Dkt. Mlote alisema kwamba, wameamua kwenda kujifunza kilimo chau yoga siyo tu katika kubadilishana uzoefu, bali pia kuongeza ujuzi ili kupata tija katika shughuli za kilimo rafiki wa mazingira katika utekelezaji wa mradi huo wa Green Voices.

“Tunataka kujifunza aina mbalimbali za kilimo kwa sababu hii ni fursa nzuri ya kumwezesha mwanamke kujiajiri na kuongeza pato kiuchumi,” alisema Dkt. Mlote.

Dkt. Mlote, ambaye ni Ofisa Mwandamizi katika Wizara ya Kilimo, Chakula na Mifugo, alisema mazingira walioyonayo katika kuendesha kilimo hifadhi cha nyanya, kabichi na mapapai huko Kinyerezi hhayana tofauti na mazingira ya kilimo cha uyoga kwani shughuli zote zinafanyika katika maeneo madogo ya nyumba zao huku wakihitaji kiasi kidogo cha maji.

“Ni rahisi kuendesha miradi hii kwa kuwa shughuli zote zipo nyumbani na hata utarudi usiku kutoka kazini, bado unaweza kuingia shambani na kuhudumia mimea kwa kutumia mwanga wa taa zilizomo kwenye banda,” alisema.

Kikundi hicho cha ‘Kinyerezi Green Voices’ kinaundwa na wanawake 10, ambao baada ya mafunzo walioyoyapata katika awamu ya kwanza ya mradi wa Green Voices walijikita katika kilimo cha mazao mbalimbali yakiwemo nyanya, kabichi, pilipili hoho, matango na matikiti maji.

Esther Chiombola ‘Mama Uyoga’, Ofisa Kilimo Msaidizi Mwandamizi wa Manispaa ya Kinondoni ndiye mkufunzi wa kikundi cha ‘Bunju Tunza Women Group’ kinachojihusisha na kilimo cha uyoga, ambaye allitumia muda mwingi kuwaelimisha akinamama wa Kinyerezi kuelezea umuhimu wa kilimo chau yoga pamoja na faida zake.

Alisema uyoga ni lishe bora iliyojaa kiasi cha asilimia 20 hadi 49 cha protini pamoja na Vitamini B, C, D, E, na K, na madini joto, chuma, fosforas, potashi, zinki na shaba na kwamba hauna lehemu (cholesterol).

Alisema baadhi ya aina za uyoga kama Ganoderma husaidia kuzuia na kupunguza kasi ya magonjwa sugu kama saratani, kisukari, kifua kikuu, moyo, shinikizo la damu na figo.
“Kilimo cha uyoga ni ajira kubwa kwa akinamama, vijana, wazee na wastaafu na ni kilimo rafiki kinachopunguza uchafuzi wa mazingira kwa vile kinatumia mabaki ya shambani na viwandani,” alisema na kuongeza kwamba kilimo hicho ni endelevu ambacho hakina msimu.

Bi. Magdalena Bukuku ni mshiriki kiongozi wa Bunju Tunza Women Group ambaye alisema kwamba, tangu walipoanzisha mradi huo mwaka 2016 akinamama wameweza kunufaika na kuongeza mapato kutokana na bidhaa zao kupata soko kubwa katika maeneo mengi ya jijini Dar es Salaam.

“Hata kwenye maduka makubwa (super markets) wamekuwa wakiuhitaji kwa ajili ya wateja, hivyo soko la uhakika lipo la kutosha,” alisema Bi. Magdalena.

Aidha, aliongeza kwamba, kikundi chao kimekuwa kama darasa kwani watu wengi, wanawake kwa wanaume, kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar wamekuwa wakienda kujifunza kila mara kuhusu kilimo hicho.

“Ni mradi mzuri, unatumia gharama kidogo huku mavuno yake yakiwa endelevu hasa ukiwa na nia, dhamira na jitihada, soko lake lipo kubwa,” alieleza Magdalena.

Dkt. Mlote na Bi. Magdalena Bukuku ni miongoni mwa akinamama 15 wanaotekeleza Mradi wa Green Voices nchini Tanzania baada ya kupatiwa mafunzo nchini Hispania mwaka 2016 ambapo lengo ni kupaza sauti za wanawake kwa ajili ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa kushiriki shughuli za kilimo rafiki wa mazingira.

Akinamama wengine wanatekeleza miradi mbalimbali ya ujasiriamali unaoendana na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Kigoma, Kilimanjaro, Pwani na Mwanza.

Mratibu wa mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Bi. Secelela Balisidya, alisema katika awamu ya pili, mbali ya akinamama hao kuendeleza miradi yao ya awali, pia watapata fursa ya kubadilisha uzoefu na kuona uwezekano wa kutekeleza mmiradi mingine tofauti kwa faida yao.

huo wa kilimo hai cha nyanya kwa kutumia green house ni sehemu ya miradi 10 inayoendeshwa nchini Tanzania kupitia Green Voices ambapo inaendeshwa katika mikoa sita ya Tanzania Bara.

Mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Pwani, Mwanza, Kigoma, Morogoro na Kilimanjaro ambapo inahusisha kilimo, usindikaji, ufugaji na utafiti.

“Jumla kuna miradi 10 ikiwemo ya kilimo cha miti ya matunda mkoani Kigoma, kilimo cha viazi lishe visiwani Ukerewe mkoani Mwanza, Ufugaji Nyuki mkoani Morogoro na Pwani, ukaushaji wa mbogamboga kwa kutumia nishati ya jua mkoani Morogoro, usindikaji wa vyakula mbalimbali kutokana na muhogo mkoani Pwani, kilimo hai cha mbogamboga, kilimo cha uyoga mkoani Dar es Salaam, mradi wa majiko banifu mkoani Pwani na mradi wa utafiti wa jiko linalotumia nishati ya jua mkoani Kilimanajro,” alifafanua Secelela Balisidya.

Aidha, alisema, lengo kubwa la mradi wa Green Voices ni kupaza sauti za akinamama kueneza ujuzi wao wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi ili jamii nzima ya Kitanzania iweze kujifunza zaidi na kuzitumia mbinu hizo katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

No comments: