Tangazo

November 15, 2011

Twiga Cement kupandisha Bei ya Cement

Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa Kampuni ya Twiga Cement, Ekwabi Mgigo (kushoto) akizungumza katika semina kuhusu utengenezaji wa matofali iliyoandaliwa na kampuni hiyo jijini Dar es Salaam jana. Katikati ni Meneja wa Idara ya Mauzo na Manunuzi, Inginia Danford Semwenda na (kulia) ni Meneja Udhibiti Ubora wa Saruji, Richard Magoda.
                                         **************************************************

NA MWANDISHI WETU

KAMPUNI ya Saruji ya Twiga ya jijini Dar es Salaam imesema haina jinsi ya kuepuka kupandisha bei ya saruji kiwandani kutokana na kulazimika kununua gesi asilia kwa kutumia Dola ya Marekani.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku moja ya wafyatua matofali iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko wa kampuni hiyo, Ekwabi Magigo alisema kuwa wao hulazimika kununua gesi kutoka SONGAS kwa fedha za kigeni.

“Lakini pia hulazimika kuagiza malighafi kutoka nje. Hili nalo maana yake ni kuwa tunatumia fedha za kigeni zaidi. Wakati washindani wetu hupewa ruzuku na serikali zao kwa ajili ya kuzalisha saruji ya kuuza nje, sisi Tanzania hatupewi nafasi kama hiyo,” alisema Magigo.

Alisema kuwa kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani nako pia kunachangia kuyumba kwa bei ya saruji inayozalishwa nchini.

Hata hivyo, aliwathibitishia washiriki wa warsha hiyo kuwa saruji ya Twiga itaendelea kupatika kwa wingi na ubora ule ule kwani kiwanda chao kilichopo Wazo Hill, Dar es Salaam, kiko imara.

Warsha hiyo ya mafunzo iliyowajumuisha wagavi wa saruji ya Twiga, wateja na wafyatua matofali kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro ililenga kuwaelimisha njia sahihi za kutumia saruji kwenye biashara zao.

Huu ni mwaka wa tatu mfululizo kwa kampuni hii kubwa na kongwe nchini kutoa mafunzo yenye lengo la kuimarisha sekta ya ujenzi nchini.

Meneja wa Ubora na Viwango wa kampuni hiyo, Richard Magoda aliwaambia zaidi ya washiriki 150 wa mafunzo hayo kuwa ili kuwa na biashara endelevu wanapaswa kufahamu ubora wa malighafi wanayotumia na pia ubora wa bidhaa wanazozalisha.

Magoda aliwaambia wafyatua matoli kuwa kuna masuala kadhaa yanayopaswa kufuatwa ili kupata matofali bora zaidi.

“Mnapaswa kujua aina ya saruji mnayotumia kwenye shughuli zenu za kila siku ili kuwa na ujenzi wa nyumba imara nchini,” alisema huku akiwaasa wateja hao kutumia saruji ya Twiga Extra kwani ndio yenye uwezo mkubwa wa kuhimili hali ya chumvi chumvi iliyopo maeneo ya pwani.

No comments: