Tangazo

December 29, 2011

'2011 MWAKA WA HUKUMU KWA VIGOGO WENGI WA RWANDA ICTR'

Na Nicodemus Ikonko, Hirondelle, Arusha
 
Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) inaweza kusherehekea mwisho wa mwaka 2011 kwa kujivuna kutokana na hukumu nzito na nyingi zilizotolewa katika mwaka huo.

Mahakama hiyo imetoa jumla ya hukumu 10 katika ngazi zote mbili za mahakama ya awali na mahakama yake ya Rufaa zenye kuhusisha watu 21, akiwemo mwanamke pekee kuwahi kushitakiwa na mahakama hiyo, Pauline Nyiramasuhuko na mtu anayesadikiwa kuwa mpangaji mkuu wa mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994, Kanali Theoneste Bagosora.  

Hukumu za ICTR 2011

Gatete ahukumiwa kifungo cha maisha: Machi 29, 2011, ICTR ilianza mwaka mpya kwa kutoa hukumu yake ya kwanza katika kesi inayomkabili aliyekuwa afisa mwandamizi wa serikali ya Rwanda, Jean-Baptiste  Gatete ambaye alitiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari na kuteketeza kizazi. Alipewa adhabu ya kifungo cha maisha jela na kesi hiyo sasa iko mahakama ya Rufaa.

Aliyekuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi ahukumiwa kifungo cha miaka 30: Mei 17, 2011, Mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa ilitoa hukumu nyingine nzito katika kesi inayohusisha maafisa wanne wa zamani wa jeshi la Rwanda wakiwemo Afisa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi hilo , Jenerali Augustin Bizimungu na Afisa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Polisi, Jenerali Augustin Ndindiliyimana.

Majenerali hao walitiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.Bizimungu alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela huku mwenzake, Ndindiliyimana alipewa adhabu ya muda aliokwisha tumikia akiwa kizuizini tangu mwaka 2000.Aliachiwa huru mara moja.

Maafisa wengine waliotiwa hatiani ni pamoja na Mkuu wa Bataliani ya Usalama Jeshini, Meja Francois-Xavier Nzuwonemeye na Kapteni Innocent Sagahutu pia wa Bataliani hiyo ambao walipewa kila mmoja wao adhabu za vifungo vya miaka 20 jela baada ya kutiwa hatiani kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita. Pande zote mbili za mwendesha mashitaka na utetezi zimekata rufaa.

Mwanamke pekee na wengine watano watiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari: Juni 24, 2011 ilikuwa siku ya pekee katika historia ya ICTR kwa kutoa hukumu ya kesi iliyokuwa na watuhumiwa wengi zaidi kuliko kesi yoyote katika mahakama hiyo.
 
Kesi hiyo maarufu kwa jina la Kesi ya Butare, inajumuisha watuhumiwa sita akiwemo mwanamke pekee, Pauline Nyiramasuhuko, Waziri wa zamani wa Familia na Masuala ya Wanawake na mtoto wake wa kiume, Arsene Shalom Ntahobali. Wawili hao walihukumiwa vifungo vya maisha jela baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu ukiwemo ubakaji na kuteketeza kizazi na uhalifu wa kivita.

Wengine waliotiwa hatiani katika kesi hiyo ni pamoja na Eli Ndayambaje, aliyehukumiwa pia kifungo cha maisha jela, Alphonse Nteziryayo, alipewa adhabu ya kifungo cha miaka 30, Sylvain Nsabimana atatumikia miaka 25 jela ambapo Joseph Kanyabashi alipewa adhabu ya miaka 35 jela. Wote sita wanasubiri tarehe ya kusikilizwa kwa rufaa zao.

Mawaziri wawili waachiwa huru na wengine wawili watiwa hatiani: Septemba 30, 2011, hukumu nyingine ilitolewa katika kesi inayohusisha mawaziri wanne wa zamani wa Rwanda katika serikali ya mpito ya mwaka 1994. Mahakama iliwaachia huru mawaziri wawili ikiwa ni pamoja na Casimir Bizimungu (Afya) na Jerome Bicamumpka (Mambo ya Nje). 
 
Waliotiwa hatiani ni Justin Mugenzi (Biashara) na Prosper Mugiraneza (Utumishi wa Umma) ambao kila mmoja wao alipewa adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kula njama za kufanya mauaji ya kimbari na uchohezi.Kama ilivyokuwa kwa wote waliotiwa hatiani nao wamekata rufaa kupinga hukumu hiyo.

Meya wa zamani ahukumiwa kifungo cha miaka 15 jela: Novemba 17, 2011 Mahakama pia ilitoa hukumu nyingine katika kesi ya meya wa zamani nchini Rwanda, Gregoire Ndahimana. Alitiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari na ukatili dhidi ya binadamu na kuhukumiwa adhabu ya kifungio cha miaka 15. Anasubiri kupangiwa tarehe ya kusikilizwa rufaa yake.

Wanasiasa vigogo wawili wa Rwanda kutumikia jela maisha: Desemba 21, 2011 ICTR ilitoa hukumu ya mwisho kwa mwaka huu katika kesi ya wanasiasa wawili wa kilichokuwa chama tawala cha MRND wakati wa mauaji ya kimbari ikiwa ni pamoja na Rais wa chama hicho Mathieu Ngirumpatse na Makamu wake, Edouard Karemera.Walitiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita. Walipatikana na hatia hususa ni kwa sababu ya nafasi yao kama viongozi wa juu wa chama hicho kwa kushindwa kuwazuia wala kuwaadhibu wanamgambo wa chama chao maarufu kama Interahamwe waliokuwa wanashiriki katika mauaji ya kimbari.

Hukumu za Mahakama ya Rufaa    

Luteni Kanali Muvunyi kuendelea kutumikia miaka 15 jela: Aprili 1, 2011, Mahakama ya Rufaa ya Mahakama ya ICTR, ilithibitisha adhabu ya kifungo cha miaka 15 jela aliyopewa afisa wa zamani wa jeshi la Rwanda Luteni Kanali Tharcisse Muvunyi. Afisa huyo aliyekuwa katika Chuo cha Maafisa wa Jeshi Wasiokuwa na Kamisheni (ESO) alitiwa hatiani kwa uchochezi wa mauaji ya kimbari katika hotuba yake aliyoitoa Kusini mwa Rwanda wakati wa mauaji ya kimbari mwaka 1994.

Luteni Kanali Setako kuendelea kutumikia miaka 25 jela:  Septemba 28, 2011 Mahakama ya Rufaa pia ilithitisha adhabu ya kifungo cha miaka 25 jela aliyopewa aliyekuwa afisa wa zamani wa jeshi la Rwanda, Luteni Kanali Ephrem Setako baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.

Maafisa wawili waandamizi wa zamani wa jeshi wanusurika vifungo vya maisha: Desemba 14, 2011, Mahakama ya Rufaa ilipunguza hadi miaka 35 jela adhabu ya kifungo cha maisha aliyopewa mtu anayesadikiwa kuwa alikuwa mpangaji mkuu wa mauaji ya kimbari ya Rwanda Kanali Theoneste Bagosora baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari,uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita. 
 
Katika mahakama hiyo pia tarehe hiyohiyo ilimpunguzia afisa mwingine adhabu kama hiyo ya kifungo cha maisha jela hadi miaka 15, afisa mwingine wa jeshi, Luteni Kanali Anatole Nsengiyumva. Kwa kuzingatia muda aliokwishatumikia akiwa kizuizini tangu atiwe mbaroni, mahakama iliamuru kuachiwa huru mara moja.  

Kesi ya mtuhumiwa wa ICTR kusikilizwa Rwanda kwa mara ya kwanza: Desemba 16, 2011, Mahakama ya Rufaa ilitoa uamuzi wa kihistoria kwa kuruhusu kesi ya mchungaji Jean Uwikinkindi kwenda kusikilizwa nchini Rwanda.Mahakama mapema ilitupilia mbali rufaa ya mtuhumiwa huyo kupinga uamuzi wa mahakama ya awali ulioamuru kesi hiyo kwenda kusikilizwa nchini Rwanda Juni 28, 2011. Umuazi huo unafungua njia kwa kesi nyingine za watuhumiwa wa ICTR kupelekwa kusikilizwa nchini Rwanda.

Matukio mengine muhimu ICTR


Uchaguzi wa Rais na Makamu wake ICTR: Jaji mwanamke, raia wa Pakistani, Khalida Rachid Khan alichanguliwa kuwa Rais wa ICTR,kuanzia Mei 27, 2011 kwa kipindi cha miaka miwili. Jaji Khan ambaye alikuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama namba III alikuwa Makamu wa Rais wa ICTR tangu Mei 29, 2007. Wakati hohuo, Rais huyo alitangaza Agosti 24, 2011 kwamba Jaji Vagn Joenson kutoka Denmark aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa ICTR. Jaji huyo alianza rasmi kazi hiyo Agosti 26, 2011.

 Kuachiwa mapema mfungwa wa mauaji ya kimbari: Mfungwa wa mauaji ya kimbari, Michel Bagaragaza, aliachiwa toka gerezani nchini Sweden alikokuwa anatumikia adhabu ya kifungo cha miaka nane jela baada ya kutumikia tayari theluthi mbili ya adhabu hiyo iliyotolewa na ICTR kwa kula njama za kufanya mauaji ya kimbari. Hii ni mara ya kwanza kwa Mahakama hiyo ya Umoja wa Mtaifa kuruhusu mmoja wa wafungwa wake kutoka jela kabla ya muda wa adhabu uliotolewa kumalizika. Bagaragaza alikuwa Mkuu wa Mamlaka ya Chai nchini Rwanda.

Wito kwa mataifa kupokea wanaoachiwa huru ICTR: Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limezitaka nchi wanachama wa umoja huo kuwapokea watuhumiwa wanaoachiwa huru na Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) na kuendelea kubaki chini ya uangalizi wa mahakama hiyo. Wapo watuhumiwa watano waliokwishaachiwa huru lakini bado wanatafuta nchi za kuwapokea.

No comments: