Waziri wa Mambo ya Nje, Bernad Membe |
Tarehe 13/2/2010 Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilifanya kikao cha pamoja na Menejimenti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kujadili taarifa ya Hesabu za Wizara kwa mwaka wa fedha 2009/2010.
Kufuatia kikao hicho baadhi ya vyombo vya habari vilitoa taarifa ambazo siyo sahihi kufuatia masuala yaliyojadiliwa katika kikao hicho.
Wizara inakanusha taarifa hizo zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari, na sio kweli kwamba Balozi zetu zina matatizo makubwa ya kifedha.
Kilichozungumziwa katika kikao hicho ni kuwa Balozi zetu bado zinatumia viwango vya Posho ya Utumishi wa Nje ambavyo vimepitwa na wakati. Ili kuhakikisha kuwa viwango hivyo vya Posho ya Utumishi wa Nje vinaboreshwa ili kuendana na hali halisi ya maisha;
Awali Wizara ilifanya mapitio ya Kanuni za Utumishi wa Nje (Foreign Service Regulations) zinazohusisha Posho ya Utumishi wa Nje na kuziwasilisha katika mamlaka husika.
Kwa kuwa mapitio Kanuni hizo ziliandaliwa muda mrefu uliopita, Wizara iliona kuwa upo umuhimu wa kuunda kamati maalum ya kupitia kanuni hizo za Utumishi wa Nje.
Kamati hiyo imeshakamilisha kazi yake na kuiwasilisha kwa Menejimenti ya Wizara kwa ajili ya uhakiki na hatimaye kuiwasilisha katika mamlaka husika.
Pamoja na kuwepo kwa changamoto hiyo ya kuwa na viwango vya Posho ya Utumishi wa Nje vilivyopitwa na wakati, Balozi zetu zimeweza kupelekewa mishahara yao ya kila mwezi
pasipo kuchelewa.
Aidha, tatizo jingine lililoelezwa ni upungufu wa Bajeti unaotokana na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya Fedha nyingine za Kigeni.
Katika kuwezesha kutatua tatizo hili Hazina imekuwa ikilipa kwa wakati fidia inayotokana na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania katika kila kipindi cha robo mwaka.
Kwa ujumla Balozi zetu zimeendelea kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kutumia rasilimali fedha zilizopo katika Bajeti.
Aidha, siku zote Wizara imekuwa ikipata ushirikiano mkubwa kutoka Hazina katika kushughulikia masuala ya fedha Balozini.
IMETOLEWA NA:
WIZARA YA MAMBO YA NJE
NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM
14/2/2012
NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM
14/2/2012
No comments:
Post a Comment