Tangazo

March 19, 2012

Mama Kikwete awataka Wananchi kuilinda Miundombinu

Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA, Mke wa Rais Mama Salma Kikwete (alievaa traki suti ya bluu) akizindua Matembezi ya Mkakati wa Uboreshaji wa Miundo-mbinu ya Elimu katika Kata ya Kipawa, Manispaa ya Ilala Mkoa wa Dar es Salaam Machi,17,2012. Pichani (kutoka kulia wa pili mwenye miwani), ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Slaa,(akifuatiwa na alievaa traki suti nyeupe)  Diwani wa Kata ya Kipawa Bona Kalua, Sherehe hio pia imehudhuriwa na viongozi mbalimballi wa Serikali na wadau wa sekta ya uboreshaji wa miundo-mbinu  ya elimu na mazingira wa kata hiyo, Picha na Mwanakombo Jumaa- MAELEZO.
Na Anna Nkinda – Maelezo

Dar es Salaam Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka wananchi kulinda miundombinu iliyowekwa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo kwani kila mtu anahisa katika mali hizo kwa kuwa analipa kodi ambayo inatumika kuboresha na kuendeleza  miundombinu hiyo.

Wito huo umetolewa juzi na Mama Kikwete  ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) wakati akiongea na wakazi wa Kipawa walioshiriki matembezi ya Uzinduzi wa mkakati wa uboreshaji wa miundombinu ya elimu katika kata hiyo.

Mama Kikwete alisema kuwa suala la ujenzi wa Taifa ni la jamii nzima na halihusiani na itikadi za vyama hivyo basi kila mwananchi anatakiwa kuhakikisha kuwa amefanya mambo ambayo yataisaidia Serikali  na jamii yake ili iweze kuendelea  na kuacha malalamiko kuwa Serikali haiwatimizii mahitaji yao.

“Kuna baadhi ya watu wanalalamika kila siku kuwa Serikali haiwafanyii mambo ya maendeleo lakini hawajiulizi wao wamefanya mambo gani ya kuisaidia Serikali yao ili iweze kuendelea.

Siku hii ya leo  watu watachangia  fedha nyingi kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya shule katika kata yenu, jambo la muhimu ni kuangalia mtu atakayepewa dhamana ya kusimamia miundombinu hiyo kazi anayoifanya inaendana na fedha alizopewa au la! ”, alisema Mama Kikwete.

Aidha Mama Kikwete aliwataka wanafunzi kutokuharibu samani  zitakazonunuliwa kwa  kurukaruka juu ya madawati, viti na meza bali wazitunze ili  wenzao  waweze kuzitumia pia watambue kuwa elimu ndiyo nyenzo na silaha muhimu ya kumsaidia mtu yeyote kupata ujuzi na stadi za kumwezesha kuyatumia mazingira yake kujiendeleza binafsi, familia na jamii yake.

Kwa upande wake Mstahiki Meja wa Ilala Jerry Silaa ambaye pia ni mhamasishaji mkuu wa shughuli hiyo aliwataka wazazi  na wadau mbalimbali wa maendeleo kuchangia ili waweze kuboresha mazingira ya elimu kwa watoto wao bila kujali itikadi zozote.

Mstahiki Meja huyo alisema kuwa yeye kama kiongozi kijana mwenye chachu ya maendeleo kwa watanzania atahakikisha kuwa anawahamasisha wananchi ili waweze kuchangia katika zoezi hilo ili miundombinu ya elimu iweze kuimarika kwenye kata hiyo.

Akisoma risala kwa mgeni rasmi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Minazimirefu Winifrida Nyamwihura alisema kuwa matatizo ya kielimu yanayoikabili kata hiyo ni upungufu wa madarasa, matundu ya vyoo, nyumba za walimu, ofisi za walimu, stoo, vyumba vya maktaba, bwalo la chakula, maktaba, maabara, jengo la utawala.

Sambamba na hilo kuna upungufu mkubwa wa samani kama madawati, meza, viti, makabati, shelf na meza, ukosefu wa umeme, maji kwa shule zote na ukosefu wa uzio kwa shule za Msingi majani ya Chai, Mogo, karakata na Sekondari za Ilala na Majani ya Chai.

Kata ya Kipawa ina Shule  kumi na mbili kati ya hizo kumi ni za Msingi ambazo zina wanafunzi 7919 kati ya hao wavulana ni 3997 na wasichana 3922, wanafunzi wenye ulemavu wa akili ni 52 wavulana ni 33 na wasichana 19 ambapo shule za Sekondari ni  mbili  zenye wanafunzi 2171, wavulana 1146 na wasichana 1025.

Zaidi ya shilingi milioni 18 zilipatikana katika matembezi hayo ambapo Taasisi ya WAMA ilichangia shilingi milioni tatu, Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja pamoja na wadau wake wa maendeleo walichangia milioni 10.

No comments: