Tangazo

March 2, 2012

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF) watakiwa kuboresha Huduma za Afya Vijijini

Mbunge wa Mbinga Mashariki, Mheshimiwa Gaudence Kayombo (kulia), akifuatilia kwa makini mada kuhusu utekelezaji wa mfuko wa afya ya jamii katika siku ya wadau wa mfuko huo iliyofanyika mjini Songea leo katika ukumbi wa Songea Club.

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF) nchini umeshauriwa kutafuta ufumbuzi wa kuviondolea vituo vya Afya mkoani Ruvuma uhaba wa watoa huduma wenye sifa hasa vijijini ili utendaji kazi wa mfuko upate mafanikio yaliyokusudiwa.

Rai hiyo imetolewa leo mjini Songea na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu wakati akifungua mikutano wa wadau wa mfuko wa Bima ya Afya mkoa wa Ruvuma katika ukumbi wa Songea club.

Mkuu wa Mkoa aliongeza kusema kuwa ukosefu wa watoa Huduma za afya wenye sifa unasababisha utoaji Huduma hafifu zisizokidhi kiwango kinachotakiwa kwa wanachama na wananchi.

Mwambungu alisisitiza na kutahadhalisha kuwa kutoa Huduma za afya bila utaalam ni maafa makubwa kwa maisha ya wananchi . “Hii ni hatari kubwa kubahatisha kutoa Huduma za tiba” alisema Mkuu wa Mkoa.

Aidha akijibu maombi yalitolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko Hamis Mdee alisema kuwa anasikitishwa na kitendo cha mkoa wa Ruvuma kuwa na asilima 0.3 ya wanachama wa mfuko wa Afya ya Jamii(CHF) Mwambungu aliwaagiza wakurugenzi wote wa Halmasahauri za wilaya na Manispaa kuhamasisha wananchi katika maeneo yao ili wanufaike na mfuko kwa kuhamasisha kaya kujiunga na mfuko wa afya ya Jamii.

Aliongeza kuwaagiza wakurugenzi kuwa waifannye CHF kuwa agenda muhimu katika mikutano yote ili wananchi waelimishwe na kufahamu manufaa ya kujiunga
Kuhusu matatizo wanayopata wanufaika wa mifuko hii mkuu wa mkoa aliwaasa watoa huduma afya kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kuitumia vyema mifuko hii wakijua kuwa mifuko hii inaingiza fedha nyingi inasaidia Kuboresha miundombinu ,vifaa tiba na hata kuajili watoa huduma wengi.

“Mwananchi hawezi kuona umuhimu wa mifuko hii ya Taifa ya Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii kama Huduma za wale wanaofika kwenye vituo vya afya hawahudumiwi ipasavyo,hawapokelewi kwa upendo na kutazamwa kama kero na baadhi ya watoa Huduma za afya” alisema Mwambungu.

Akitoa maelezo ya awali kabla ya ufunguzi Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF)Hamis Mdee alitoa wito kwa halmashauri zote nchini kutumia fursa ya uwepo wa huduma ya mikopo ya masharti nafuu ya vifaa tiba kwa vituo vya afya ambapo alisema huduma hii ya mikopo ikitumiwa vema itasaidia sana kuwapatia wananchi huduma bora za afya.

Aliongeza kusema kuwa katika kuadhimisha sherehe ya mfuko wa Bima ya Afya umetimiza miaka kumi tangu kuanzishwa hapo 2001 nakusema hadi sasa ni asilimia 13 tu ya wananchi zaidi wa milioni 41 wanaolengwa kufaidika na Huduma hii.

Hata hivyo amesema kuwa mfuko umejiwekea lengo kuwa ifikiapo mwaka 2015 utaweza kuwafikia wanachama asilimia 30 ya watanzania wote.

Aliongeza kutoa changamoto kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma kuongeza kasi ya kuchangia mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambapo kwa sasa ni asilimia 0.3 ya kaya za mkoa wa Ruvuma wamejiunga na mfuko hivyo akasema mkoa una kazi kubwa ya kuhakikisha kaya nyingi zaidi zinahamasishwa kujiunga.

Naye Makamu Mwenyekiti wa mfuko wa bima ya afya ya Taifa Ally Kiwenge alisema bodi yao iliona kuna umuhimu wa kuwa na semina hii ya wadau kwani wanastahili kushirikishwa mafanikio yaliyofikiwa.

Alisema kuna msemo wa waswahili ussemao “ukitaka kwenda kwa kasi nenda peke yako lakini ukitaka kwenda kasi zaidi nenda na wenzako”.Kwa muda wa miaka kumi ya mfuko alisisitiza kwa umelenga kuimarisha ushiriki wa wadau wote ili kupate suluhisho la changamoto zinazoukabili mfuko .

Kiwenge alisema kuwa wamepata ushirikiano mkubwa kutoka wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri nchinii kwa kuelimisha na kusimamia mfuko huu pamoja na ule wa afya ya Jamii tangu kuanzishwa kwake.

Kauli mbiu ya mfuko inasema “ Huduma bora za matibabu vijijini na afya bora kwa wote”, na kusisitiza kuwa vijijini ndiko kuna watu wengi hivyo B Kiwenge akawaomba viongozi wa wilaya na halmashauri mkoani Ruvuma kuwahamasisha wananchi kujitahidi kuchangia licha ya matatizo ya bajeti.

Mkutano huu wa wadau wa mifuko ya Bima za afya unawakutanisha wadau mbalimbali wapato 300 kutoka wilaya zote nne za Songea,Tunduru,Namtumbo na Mbinga ukijumuisha wawakilishi wa wanachama waajili na wananchi .

No comments: