August 01, 2012, Mbeya,
Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii
kuwapongeza kwa dhati kabisa washindi wa tuzo za kwanza za umahiri wa
dijitali zilizoandaliwa na kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom,
nchini Tanzania (The Vodacom Awards for Digital Excellence – VADE). Na
kwa upekee kabisa, napenda niwataje washindi hao ambao ni wafuatao:
Mikocheni Report, Issa Michuzi,
Wanamuziki Tanzania, Kipanya.co.tz, Vijana FM, Millardayo.com, Taste of
Tanzania, Jamii Forums, Mambo Magazine pamoja na DJ Fetty Blog.
Toka kutangazwa kwao, msimamo wangu
umekuwa ni kwamba, sina tatizo na washindi, maana mwisho wa siku naamini
hawakujichagua wao wenyewe. Lakini niongeze pia kuwa, huenda sina
tatizo na waliowachagua washindi hao, kwani ni wazi walichagua washindi
kulingana na vigezo ambavyo viliwekwa na ndio maana waandaaji hawakuwa
na lolote la kusema pindi walipotajwa washindi hao, zaidi ya kuwapa tuzo
zao.
Na baada ya hapo, bilashaka sasa
ninabakia na upande ambao nina matatizo nao. Upande wa waandaaji wa tuzo
hizi, na hapa nikimaanisha kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom.
Kwangu mimi, utoaji wa tuzo hizi,
umekuwa ni mwendelezo wa usanii ambao umekuwa ukifanywa na kampuni hii
katika kuhakikisha kuwa wanatumia udhaifu wa kisheria, weledi na
mshikamano baina ya waandishi wa habari wa mtandaoni, kujinufaisha zaidi
wao badala ya kuwanufaisha wanahabari hawa ambao ni wazi wamekuwa
wakiwafanyia kazi kubwa sana.
Yapo mambo kadhaa ambayo binafsi
nimeyaona kuwa ni usanii mkubwa sana ambao umefanywa na Vodacom hapa na
wala haikuwa kwa lengo la kuinua wahusika au tasnia ya uandishi wa
mtandaoni kwa ujumla wake na miongoni mwayo ni pamoja na vigezo ambayo
vilitumika katika utoaji wa tuzo hizo.
1. kati ya vigezo ambavyo nilisikia kuwa
walivitumia, ni pamoja na blog au blogger husika kuwa na blog ambayo
habari anazoziweka hazitokani na kutafsiri kutoka mitandao yoyote ile
iwe ya ndani au nje ya nchi wala kuwa imechukuliwa toka blog zingine.
Miongoni mwa blog ambazo zilishinda kama
ambavyo nimezitaja hapo juu, zipo ambazo zimekuwa zikiandika kazi za
wasanii wa nje ambazo wenyewe wamekuwa wakitamka kabisa maneno “…kwa
mujibu wa mtandao fulani, redio fulani, jarida fulani nk” Je, Vodacom
hawakuliona hili kuwa ni kinyume na vigezo vyao hapo?
2. Nimesoma mahali kuwa Vodacom
waliliasisi wazo hili mwezi uliopita, kwa maana ya mwezi Julai mwaka
huu, ingawa linaelezwa pia kuwa lilikuwa wazo la muda mrefu na kisha
mwezi huo huo tuzo hizo zikatolewa.
Je, Vodacom wanaweza kutusaidia kujua ni
jinsi gani waliwashirikisha blogger katika kuandaa tuzo zenyewe, kwa
maana ya kuweka vigezo, sababu ya vigezo hivyo, mechanism ya kuhakikisha
kuwa vigezo vinafuatiliwa (hasa linapokuja suala la takwimu), na mambo
mengine ya namna hiyo?
3. Katika kuangalia kile walichosema
kuwa habari kwenye hizo blog zinatakiwa ziwe zimeandikwa na mtu mwenye
ujuzi nazo, je walikuwa na mechanism gani pia katika kuhakikisha hili?
Maana Vodacom ni kampuni ya simu, haina wataalamu wala weledi wa masuala
ya habari.
Upo uwezekano mkubwa sana kuwa walitumia
kitengo chao cha mawasiliano na umma au kitengo chao cha habari nk,
(kulingana na wanavyokiita wao), lakini pia upo ukweli wa wazi kuwa
kitengo hiki sawa na kile cha masoko, vimekuwa vitengo vyenye kuonyesha
waziwazi udhaifu wao katika utendaji kazi wao kiasi cha kuzua maswali
miongoni mwa wenye kuvifuatilia.
Hebu tujiulize, si hawa hawa Vodacom
ambao walizua mjadala mkubwa sana baada ya kuwa miongoni mwa wadhamini
wa blog ambayo ilikuwa ikitajwa kuwa imejaa matusi mengine ambayo
hayafai hata kusimuliwa mbele za watu waliostaarabika? Watu wa habari
kama wapo, na kama walishindwa kubaini mapungufu ya kilichokuwa kimejaa
katikablog hiyo, leo hii wanawezaje kutushawishi kuwa walikuwa bora
katika kuibua na kutekeleza wazo la VADE? Na wale wa masoko nao
halikadhalika?
Je, Vodacom kweli walishindwa kuwa
waungwana walau hata kushirikisha waasisi wa fani hii katika Tanzania,
wakiwemo akina Ndesanjo Macha, Jeff, na wengineo ambao tunawajua kuwa
bila wao leo hii Watanzania bado tungekuwa tunasikia tu kitu blog katika
vyombo vya habari?
Ni aibu sana kwa kampuni kubwa kama hii
kuchukulia suala la tuzo kama mechi fulani ya wanywapombe wanaoamua
kujifurahisha katika kile wanachokipachika jina la Bonanza. Aibu
kwasababu, hata utoaji wa tuzo wenyewe, lilikuwa tukio ambalo lilikuwa
jepesi jepesi mno. Halikuwa na mwamko wa namna hiyo, na pengine ni
kutokana na ukweli kuwa wenyewe walishajua kuwa wamefanya madudu kwahiyo
ili kuepuka aibu, basi wasiifanye kuwa issue kubwa.
Na ni katika muktadha huu basi ambako
binafsi najiuliza, Je, Vodacom, wameona kuwa kilicho cha muhimu kwao ni
kujitangaza tu bila hata kujali kuwa kujitangaza kwenyewe kunahusisha
kuwa watupu? Lakini pia nageuka upande wa waandishi wa habari hususan
ambao wamezitwaa tuzo hizo.
Mmejisikiaje kupata kitu ambacho kama
wana taaluma mnaelewa wazi na nafsi zenu zinawaeleza kuwa mmefanywa
kombe lililofunikwa ili mwanaharamu fulani apite na aendelee na hamsini
zake?
Inawezekana kabisa kuwa wazo lilikuwa
zuri, na hakika ninaafiki sio tu kuwa wazo lilikuwa zuri, bali lilikuwa
zuri sana, lakini utekelezwaji wa wazo hili, umekuwa ni tukio la aibu
ambalo binafsi ninaamini kabisa kuwa Vodacom, watatakiwa kukaa na
kujitathmini juu ya namna wanavyowatumia waandishi wa habari.
Ni hadi pale tutakapofikia mahali pa
kutambuana na kuthaminiana ndipo tutaweza kusonga mbele kimaendeleo,
kinyume na hapo, hii tabia ya wengine kuwa wanyonge na wengine kuwa
mahiri katika kutumia udhaifu wa wengine kitaaluma, kiumoja na hata
kiueledi, itafikia mahali itatuumbua hadharani kweupeeeeee!! Kama
ambavyo imeshaanza kujionyesha sasa ambapo nasikia kuwa mmoja wa
washindi, ambaye ni Michuzi, amerejesha tuzo hiyo kwa waandaaji. Sijui
kwa kuikataa, kuona haimstahili anataka wambadilishie wampe nyingine au
vipi.
Niko tayari kukosolewa pale ambapo siko sahihi
Ramadhan Msangi
CEO – Jukwaa Huru Media
CEO – Jukwaa Huru Media
No comments:
Post a Comment