Tangazo

March 23, 2012

RWANDA YATIMUA WAFARANSA WA KUCHUNGUZA KESI ZA MAUAJI YA KIMBARI

 Martin Ngoga
Na Hirondelle, Arusha

Rwanda imewatimua wapelelezi wa Kifaransa waliokwenda nchini humo kuchunguza kesi za mauaji ya kimbari zilizoko mbele ya mahakama za Ufaransa, Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Rwanda, Martin Ngoga alisema.

‘’Timu ya mwisho iliyotumwa na Ufaransa kuja Rwanda wiki iliyopita tuliitimua kurejea kwao. Tuliwaambia rudini hadi mtakapokuwa tayari kufanyakazi kwa dhati ndipo nasi tutashirikiana nanyi,’’ Ngoga aliwaambia waandishi wa mjini Arusha Alhamisi.

Wapo Wanyarwanda wengi wakifanyiwa uchunguzi katika mahakama za Ufaransa kwa ajili ya tuhuma za kuhusika kwao na mauaji ya kimbari ya Rwanda, lakini hakuna kesi hata moja iliyoanza kusikilizwa mapaka sasa katika nchi hiyo ya Ulaya, ambayo inashutumiwa na serikali ya sasa ya Rwanda kwamba inaunga mkono serikali ya Kihutu iliyokuwa inatawala mwaka 1994.

Ngoga alisema hiyo ni ishara iliyotumwa Ufaransa kwamba,’’ Kama hawapo tayari kwa ajili ya kushughulikia kesi hizo inaweza kusimamisha uchunguzi.Wasiendelee kutupotezea muda;Wasiendelee kuja Rwanda mara chungu nzima zisizohesabika bila matunda yoyote.’’

Mwendesha Mashitaka huyo alielezea kutoridhika kwake kwa kusema ‘’ Ufaransa imekuwa ikikatisha tamaa sana kwa jinsi inavyoshugulikia kesi za mauaji ya kimbari.Katika takwimu zetu Ufaransa imetuma timu za uchunguzi mara nyingi zaidi kuliko nchi yoyote ya Ulaya,’’ Alisisitiza kwamba timu ya wapelelezi iliyorudishwa makwao ilikuwa ya 35 nchini Rwanda.

Kwa mujibu wa Ngoga kulikuwa na watuhumiwa waliokuwa bado wanasakwa 18 ambao walitiwa mbaroni nchini Ufaransa na kisha wote wakaachiwa huru kwa sababu mbalimbali na hivi karibuni kabisa jalada moja la kesi lilipotea na hawakujua mazingira yaliyosabbisha kupotea kwa jalada hilo.

‘’Nafikiri kama Ufaransa haitabadilisha namna inavyoshughulikia kesi za mauaji ya kimbari, sisi (ofisi ya mwendesha mashitaka) tutalazimika kufikiria upya uhusiano wetu wa kikazi na wao.Hatutaendelea  kukubaliana na visingizio kama vile hakuna bajeti. Huwezi kuzungumzia suala la ukosefu wa bajeti katika kushughulikia kesi za mauaji ya kimbari kwa nchi kama Ufaransa. Kwa maana hiyo kesi za mauaji ya kimbari zinashindania bajeti na kesi za makosa ya usalama barabarani,’’ alitoa mfano.  

No comments: