Tangazo

April 16, 2012

Mwizi wa Kichanga atiwa Mbaroni na Polisi Zanzibar

Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi Zanzibar

 Jeshi la Polisi Zanzibar linamshikilia mwanamke mmoja mkazi wa Tomondo mjini Zanzibar kwa tuhuma za kuiba mtoto mchanga mwenye umri wa miezi mitano kutoka katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja mjini Zanzibar .

 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar Kamishna Msaidizi Aziz Juma Mohammed, amemtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Fatma Abdallah Mohammed(26), ambaye alikamatiwa Bandarini akisafiri na mtoto huyo kwenda Pemba .

Kamanda Aziz amesema kuwa mtoto huyo aitwaye Aisha Nassor Ali, aliibwa Aprili 10, mwaka huu majira ya saa tano asubuhi wakati mama wa mtoto huyo  Bi. Rahma Hassan Ali, alipompeleka mtoto wake kupata matibabu katika Hospitali ya Kuu ya Mnazimmoja mjini Zanzibar .

Amesema wakati mama wa mtoto huyo akiwa katika foleni ndefu ya kutaka kupata kadi ya kumuona daktari, alitokea mwanamke mwingine ambaye sasa ni mtuhumiwa, akijifanya kuwa ni mwandishi wa Habari na alikuwa akifuatilia kezo za tiba katika Hospitali hiyo, lakini pia alikuwa akifahamiana na mmoja wa madaktari na hivyo kumtaka ampe msaada ili mtoto huyo aweze kupatiwa tiba kwa haraka.

Amesema mtuhumiwa huyo aliongea na simu na kujifanya kuwa alikuwa akionge na daktari na bwamba amemtaka apelekwe mtoto huyo kwake kwa matibabu na ndipo mtuhumiwa huyo alipomwambia mama wa mtoto kuwa ampatie mtoto ili atangulie naye kwa daktari na kumtaka mama wa mtoto akatafute daftari la kuandikia matibabu ya mtoto wake.

 Kamanda Aziz amesema mtuhumiwa huyo alimchukua mtoto huyo na kupanda ghorofani kwa daktari lakini baada ya mama wa mtoto huyo alipopata daftari na kumfuatilia mtuhumiwa huyo hakuweza kumpata na ndipo alipotoa taarifa Kituo cha Polisi Malindi na juhudi za kipolisi za kumtafuta mtuhumiwa pamoja na mtoto zilianza.

 Amesema hadi kufikia jana asubuhi Polisi wa kike Konstebo Jaala Juma Makame , wa Kikosi cha Polisi Wanamaji na Bandari Zanzibar , alimtia nguvuni mtuhumiwa huyo akiwa pamoja na kichanga hicho na baada ya kuwasiliana na viongozi wake Bandarini hapo, Wazazi wa kichanga hicho waliitwa na walipofika walimtambua mtoto wao.

 Aidha mama wa mtoto pia alimtambua mtuhumiwa kuwa ndiye aliyejifanya kuwa ni mwandishi wa Habari na kumkabidhi mtoto wake siku ya tukio ili amsaidie kwenda kwa daktari kupatatiwa matibabu.

Kufuatia kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali Saidi Mwema, ametoa cheti cha sifa na tuzo ya shilingi 200,000 kwa Konstebo Jaala Juma Makame, kutokana na juhudi na utambuzi wake  wa haraka wa kumpata mtuhumiwa ingawa siku hiyo kulikuwa na wanawake wengi waliokuwa wakisafiri na watoto wenye umri tofauti.

 Akikabidhi cheti hicho cha heshma na tuzo ya fedha kwa Konstebo Jaala, kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Mussa Ali Mussa, alisema kuwa Jeshi la Polisi hap nchini litaendelea kuwazawadia askari wote watakaofanya kazi zao kwa ubunifu na kufuata misingi ya sheria na haki, lakini pia kuwaadhibu na hata kuwafukuza kazi wengine watakaobainika kwenda kinyume na maadili ya Jeshi hilo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mh. Abdallah Mwinyi, amempatia Askari huyo mwanamke shilingi 50,000 kama motisha kwa juhudi alizofanya hadi kufanikisha kumkamata mtuhumiwa huyo akiwa pamoja na mtoto.

No comments: