Tangazo

May 3, 2012

VIONGOZI WA VIJIJI MKOANI IRINGA WAMULIKWE WANAHATARISHA AMANI

RC Iringa, Dk. Christine Ishengoma
Serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka kuelekeza viongozi wa vijiji nchini taratibu za kushughulikia migogoro kisheria ili kuepusha viongozi kujichukulia hatua zinazohatarisha maisha ya wanawake ikiwa ni pamoja na kupigwa kikatili.

Serikali inapaswa kuchukua hatua kufuatia utafiti uliobaini kuwa viongozi wa kijiji cha Kidabaga, kata ya Dabaga wilaya ya Kilolo mkoani Iringa wamekuwa wakiwachapa viboko kikatili wanaume na wanawake hadi kusababisha mimba kuharibika.

Wananchi wamesema kuwa Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, Vicent Gaifalo na mwenyekiti wake Nicolous Katindasa huwa wanawachapa viboko kinywa watu wanaopelekwa kwenye ofisi ya kijiji kwa tuhuma mbali mbali.

Utafiti uliofanywa na TAMWA kwa kushirikiana na vyombo vya habari wiki mbili ulikusanya taarifa zinazoonyesha kwamba viongozi wa kijiji cha Kidabaga kwa nyakati tofauti waliwachapa viboko wanawake wawili hadi kusababisha mimba zao zikaharibika.

Wananchi wa kijiji hicho wamesema Mtendaji wa Kijiji hicho Gaifalo mwezi uliopita alimchapa mama Seidina Kidwangise viboko 30 mfululizo akimlazimisha kukubali kwamba alikuwa anajua ziliko fedha za mume wake aliyeripoti kwenye ofisi ya mtendaji huyo kuwa zimepotea. Mama huyo na mume wake walikuwa wamefika kijijini hapo kwa ajili ya msiba.

Mama huyo alisema ambaye alikuwa amefika kijijini hapo kwa ajili ya msiba alisema ingawa mume wake alimuomba Mtendaji huyo wa kijiji asimchape kwani alikuwa na ujauzito na mshono wa operesheni, lakini Mtendaji huyo alikataa na akaendelea kumchapa akimlazimisha akubali kuwa kaiba fedha hizo.

Alisema siku tatu baadaye mimba yake ilitoka na alipatiwa huduma ya awali katika zahanati ya kijiji cha Kidabaga lakini hali yake iliendelea kuwa mbaya na akapelekwa hospitali ya mkoa.

Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Iringa Deogratias Manyama alithibitisha kwamba mama huyo alifikishwa katika hospitali hiyo tarehe 19 mwezi huu akiwa na alama za kupigwa na uthibitisho wa mimba kutoka na kwamba mpaka sasa hawezi kusimama wala kutembea.

Wanakijiji hao walisema mwanamke mwingine Silivia Kimata, Mei mwaka jana 2011, alichapwa viboko 16 na Mwenyekiti wa jijiji hicho, Nicolous Katindasa hali iliyosababisha mimba yake ya miezi minne kutoka tumboni.

Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kilolo OC-CID Charles Mwakipesile alisema tayari wamemkamata Afisa Mtendaji huyo na kumfungulia kesi lakini kwa sasa yupo nje kwa dhamana akisubiri taratibu za kimahakama.

Hata hivyo wanaume na wanawake waliohojiwa katika kijiji hicho wamesema kutokana na rushwa kushamiri wana wasiwasi viongozi hao wa kijiji hawatachukuliwa hatua kisheria.

Wananchi hao alisema kuwa kwa muda mrefu tangu uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2010 ulipomalizika na aliyekuwa DC wa wilaya ya Kilolo Athumani Mfutakamba kuteuliwa kuwa Naibu Waziri, wilaya hiyo haina DC hali inayochangia matatizo mengi kushindwa kutatuliwa.

Imetolewa na Ananilea Nkya
Mkurugenzi Mtendaji-TAMWA

No comments: