Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal ameiwakilisha Tanzania katika mkutanano wa Mazingira Endelevu jijini Rio De Janeiro unaofanyika jijini hapa ikiwa ni miaka 20 baada ya mkutano kama huo kufanyika mwaka 1992. Katika mkutano wa mwaka 1992, ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Rais wa wakati huo Alhaji Ali Hassan Mwinyi.
Mkutano wa mwaka huu unajadili kuhusu maazimio ya mwaka 1992 na namna yalivyotekelezwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wapatao 182 huku washiriki katika mkutano huu wakikadiriwa kutoka katika nchi 135. Sambamba na hilo mkutano huu unapitisha maamuzi mapya kuhusu kuiweka dunia na mazingira yake katika hali ya usalama ili yaweze kusaidia vizazi vijavyo.
Mkutano huu unafanyika ikiwa ni siku chache tangu kufanyika mkutano wa G-20 uliokuwa ukifanyika nchini Mexico na matokeo ya mkutano huo wa G-20 kwa namna moja ama nyingine yameongeza hamasa ya mkutano huu wa Rio +20. Hamasa kubwa kwa mataifa inabaki juu ya kutazama namna uchumi wa kijani utakavyoweza kusaidia kukuza maendeleo ya maisha ya watu duniani huku maendeleo hayo yakiiacha dunia katika hali ya kawaida katika mazingira yake ya asili.
Pia hoja ya kuhusu uzalishaji mkubwa wa gesi joto imepata mjadala mkubwa katika mkutano huu. Maeneo mengine ambayo yanajadiliwa ni kuhusu hali ya chakula duniani huku msukumo ukiwa kutoa uhuru kwa nchi kuzalisha chakula ili kutosheleza wananchi wa kila nchi husika.
Ujumbe wa Tanzania unaotolewa na Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal unalenga kuonesha namna Tanzania ilivyo na mikakati sadifu katika utunzaji wa mazingira yake sambamba na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo kikubwa yanachangiwa na nchi kubwa zenye viwanda. Ujumbe huu pia unaakisi nafasi ya nchi za Afrika katika kulinda mazingira pamoja na mikakati ya baadaye inayozingatia uzalishaji bila kuathiri mazingira kwa kiasi kikubwa.
Katika hotuba yake katika mkutano huu, Mheshimiwa Makamu wa Rais anazungumzia umuhimu wa nchi duniani kuzidi kushikamana katika kuhakikisha dunia inabakia kuwa sehemu bora ya kuishi kwa wanadamu wa sasa na wajao. Kufuatia mantiki hii, Mheshimiwa Makamu wa Rais anayakumbusha mataifa yote kuhakikisha yanazingatia maazimio ya mkutano huu wa Rio +20 ili uwe na mafanikio zaidi ya ule wa mwaka 1992.
Waliombatana na Mheshimiwa Makamu wa Rais na ambao wanashiriki mikutano ya kisekta ni pamoja na Mheshimiwa Terezya Huvisa, Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Fatma Fereji, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais SMZ pamoja na Mheshimiwa Mahadhi J. Maalim, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Kundi la Wabunge linawakilishwa na Mheshimiwa James Lembeli, Salehe Pamba na Magdalena Sakaya. Mkutano huu ulioanza Juni 20, 2012 unatarajiwa kumalizika Juni 22, 2012.
Imetolewa na: Boniphace Makene
Press Secretary to the Vice President
No comments:
Post a Comment