Tangazo

June 25, 2012

Fly 540 yawasotesha abiria uwanjani

ABIRIA zaidi ya 70 waliokuwa wasafiri kwa ndege ya Kampuni ya Fly 540 kati ya Dar es Salaam na Mwanza juzi, walijikuta wakikwama kusafiri kutokana na matatizo ya kiufundi ambayo hayajafafanuliwa wazi.

Hadi jana jioni, abiria hao bado walikuwa hawajapatiwa ufumbuzi wa lini wataendelea na safari yao, huku uongozi wa kampuni hiyo ukikwepa kulizungumzia tatizo hilo.

Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana mchana, mmoja wa abiria hao, Peter Willson, alisema kuwa walikuwa waruke na ndege ya shirika hilo juzi saa 12:00 jioni kutoka katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JKN), lakini safari ikahairishwa.

Alisema baada ya ndege hiyo namba 5H527 kushindwa kutokea uwanjani hapo, ikatolewa taarifa na wafanyakazi wa shirika hilo kuwa kulikuwa na dharura iliyojitokeza katika ndege, hivyo ilipaswa kufanyiwa matengenezo kwanza.

“Tuliombwa tulale katika Hoteli ya Avon kwa gharama za shirika hilo ili tuendelee na safari leo (jana) saa 12:15 asubuhi, lakini kulipokucha tulisubiri usafiri wa kutuchukua hadi uwanjani bila mafanikio,” alisema.

Kwamba baada ya kuona kimya, wakajaribu kuwapigia simu wafanyakazi wa shirika hilo ili kuwauliza kwa kuwa muda wa safari umepita.

“Wakati huo ilikuwa inaelekea saa 2:00 asubuhi, hata hivyo simu zao hazikuwa na majibu, ndipo tulipoamua kuja uwanjani kwa gharama zetu,” aliongeza Willson.

Alisema kuwa walipofika wakaambiwa kuwa waendelee kusubiri hadi saa 7:00 mchana, kwani uongozi ulikuwa unafanya mpango ya kuagiza ndege nyingine toka jijini Nairobi nchini Kenya.

Willson alibainisha kuwa, waliendelea kusubiri hadi muda huo bila mafanikio na kujikuta wakiwa makundi matatu yaliyopaswa kusafiri na ndege ya shirika hilo.

“Unajua kuna wenzetu walikuwa wasafiri na ndege ya saa 5:00 asubuhi na saa 7:30 mchana, hivyo wote tukajikuta tumekwama uwanjani hapa baada ya kuikosa ndege hiyo, pia wenzetu wa Mwanza nao wamekwama wakisubiri, kweli huu ni ubabaishaji na hatari,” alilalamika Willson.

Tanzania Daima ilifanya juhudi za kuwasiliana na uongozi wa kampuni hiyo bila mafanikio kwani mmoja wa watendaji wake aliyejitambulisha kwa jina la Emma, alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu kukwama kwa abiria hao, alikata simu bila kusema chochote. Chanzo Tanzania Daima Juni 25.2012

No comments: