Tangazo

June 25, 2012

TBL yahakiki mradi wa maji Geita

Na Mwandishi wetu, Geita

UONGOZI wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), umetembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa maji ulioufadhili katika Kijiji cha Mkolani, wilayani hapa.

Katika ziara yake iliyofanyika hivi karibuni, Mkurugenzi wa Uhusiano na Sheria wa TBL, Stephen Kilindo, alifuatana na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochie, Mhandisi wa Maji wa Wilaya, Daudi Kweke na mwakilishi wa Kampuni ya Dydrotech Development Agencies Community iliyopewa zabuni ya kutekeleza mradi huo, Enock Kangasa.

Kangasa aliwaeleza viongozi hao kuwa juhudi zinafanyika kuhakikisha mradi huo unakamilika mapema iwezekanavyo ili kupunguza tatizo la uhaba wa maji linalowakabili zaidi ya wakazi 3,000 wa kijiji hicho.

Kwa mujibu wa Kilindo, TBL kupitia kampeni yake ya ‘Hakuna Maji Hakuna Uhai’, ilitoa msaada wa sh milioni 25 kwa ajili ya kugharimia uchimbaji wa visima vitatu vya maji, baada ya kuthibitisha ukubwa wa tatizo la uhaba wa maji kijijini hapo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochie, alimhimiza mkandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo kwa kiwango kinachokusudiwa, huku akishirikiana kwa karibu na Mhandisi wa Maji wa Wilaya ili kutimiza matarajio ya wakazi wa Kijiji cha Mkolani.

“Mara nyingi tunaamka usiku wa manane na kutembea umbali wa zaidi ya kilomita mbili kutafuta maji na baadhi ya wanawake tumekuwa tukigombezwa na kupigwa na waume zetu kiasi cha kutishia kuvunja ndoa baada ya kuwa tumechelewa kurudi nyumbani, lakini sasa tunatarajia kuwa visima hivi vitatuondolea tatizo hilo,” alisema Salome Paulo, mkazi wa kijiji hicho.

No comments: