Tangazo

June 1, 2012

MAKALA YETU: KWANINI WATU WENGI HATUFANIKIWI VYA KUTOSHA?

Tamaa ya mafanikio katika maisha ni safari ndefu. Kwa wengi wetu ni safari ya kudumu. Kila mara tunataka zaidi. Tunataka kuwa kama fulani au fulani.Tunatamani kuwa na kiasi cha fedha kama au kuliko fulani. Kuwa na mke au mume mzuri na mwenye heshima kama fulani. Na kwa wale ambao maisha yao huendeshwa na tamaa za kuwa maarufu basi kila leo huwa wanataka kuwa kama mwanamuziki, muigizaji filamu,mwanasiasa fulani na vitu kama hivyo.


Ingawa ni vigumu sana kwa binadamu kufikia mahali ambapo anaweza kusema kwamba amesharidhika vya kutosha na alichonacho na hataki nyongeza yeyote zaidi, yawezekana kabisa mtu akafikia mahali pa kuridhisha ingawa hiyo haimaanishi kwamba akipata nafasi ya kupata zaidi hatoitumia. Hapa tunaweza kusema mtu anakuwa ameridhika kwa kiasi cha hali ya juu. Lakini kwanini basi baadhi yetu tunashindwa kufikia japo robo tu ya mafanikio tunayoyatamani? Ni mambo gani yanatukwamisha? Leo nimeona tuongelee kidogo sababu kadhaa ambazo zinatufanywa wengi wetu tukwame na hata kuishia kulaumu watu wengine bila kutambua kwamba yawezekana sababu sio ukosefu wa elimu ya kutosha,mtaji wala chochote kile bali sisi wenyewe;

Hujiamini vya kutosha: Ukijaribu kuangalia au kufuatilia maisha ya watu ambao sote tunaamini kwamba wana mafanikio zaidi yetu utagundua jambo moja muhimu;Wanajiamini. Wanaamini kwamba wanalo jambo au mambo ya msingi wanayoweza kuchangia katika jamii. Wanajiamini na wana madhumuni ya makusudi kuhakikisha kwamba jamii itawakumbuka. Watu hao pia huwa ni wajuzi wa kuketi chini wakajikosoa wenyewe na kisha kusonga mbele zaidi na zaidi. Je wewe hapo ulipo una kitu gani cha kipekee? Unayo maarifa au ujuzi (skill or talent) gani maalumu ambao hujaufanyia kazi kwa sababu ya kutojiamini tu? Kwanini usiamke leo ukaanza kujiamini zaidi kisha uone jinsi utakavyobadilisha muelekeo?

Hujui malengo yako: Hili ni tatizo kubwa miongoni mwetu. Tunafanya mambo mengi bila malengo maalumu.Akitokea mtu akakuuliza kuhusu malengo yako hapa duniani na kisha ukapatwa na kigugumizi,ujue pana tatizo hapo. Ni kwa sababu hujawahi kuketi chini na kuandika malengo yako. Matokeo yake ni kwamba kila kukicha unarukia lengo tofauti. Ni muhimu ukawa na uhakika na malengo yako.Nashauri uyaandike mahali.Ukishaandika nenda kwenye hatua ya pili ambayo ni kupanga jinsi ya kutimiza malengo yako. Yawezekana una malengo ya kuwa tajiri wa mali,kuwa mke au mume bora,kuwa na afya njema,kuwa na kazi nzuri au kufanya vizuri katika biashara. Vyovyote vile,ni lazima uwe na malengo ya uhakika.Unaweza kuyarekebisha malengo yako inapobidi. Lakini cha msingi hapa ni kujiuliza;una malengo gani hapa duniani?Una mpango gani katika kuyatimiza?

Umeridhika kupita kiasi na ulichonacho: Binadamu tuna tabia ya kuridhika. Hilo sio jambo baya. Linakuwa baya pale kuridhika kwetu kunapotufanya tushindwe kuendelea mbele zaidi,kupata zaidi ili pengine kusaidia watu wengi zaidi. Wengine hufikia hata hatua ya kujiuliza; kwanini nijisukume mbele zaidi wakati tayari nafanya vizuri hapa nilipo? Kwanini nifungue duka lingine wakati hili nililonalo tayari lina wateja wa kutosha? Wakutosha??Jiulize tena. Watu wanaofanikiwa zaidi hufanya zaidi. Huwa wanajaribu zaidi. Wanakabiliana na mitihani migumu zaidi. Jiulize; umeridhika kupita kiasi na hapo ulipo,ulichonacho? Kwanini usijaribu zaidi?

U-mvivu: Uliwahi kusikia uvivu ni adui kwa ujenzi wa taifa.Ni kweli. Ni adui pia wa mafanikio. Unaweza kuwa na mipango mizuri na mawazo mazuri.Lakini mipango bila vitendo havimfikishi mtu popote pale. Wengi wetu hupoteza muda mwingi katika mambo ambayo hayana msingi,ni ya kivivu. Ni muhimu kujiuliza maswali kuhusu jinsi unavyotumia muda wako na hatua unayopiga katika kuelekea kwenye mafanikio unayoyatamani. Kama wewe unataka kufanikiwa zaidi kama mwandishi;unaandika vya kutosha?Unasoma vya kutosha?(mwandishi mzuri ni msomaji mzuri pia) Kama wewe ni mtu wa masoko; je unauza vya kutosha? Kama wewe ni mkulima; je unalima vya kutosha? Epuka uvivu.

Hujichanganyi na watu waliofanikiwa: Ukweli lazima usemwe.Ndugu,jamaa na marafiki zako wanakupenda sana na ni watu wazuri sana. Lakini yaweza kutokea bahati mbaya wakawa hawakuchochei kufanikiwa zaidi.Ukiwaangalia unaona umefanikiwa vya kutosha wakati kumbe tukikuchanganya na wengine,unaweza kuonekana mwanafunzi! Sasa sikwambii usiambatane na ndugu,jamaa na marafiki zako. Hapana. Ninachotaka kukuambia ni kwamba, mara kwa mara jitahidi kuwa karibu na watu waliofanikiwa zaidi na zaidi.Watu wenye mawazo chanya. Watu wanaoelewa maana na tamaa ya mafanikio. Ukiwapata watu wa namna hiyo usisite kuwashirikisha katika mawazo na ndoto zako. Mara nyingi watakuunga mkono. Kwanini? Kwa sababu wao wameshafikia hayo malengo.Wanaamini inawezekana kwa sababu wameshaweza. Hali ni tofauti na ukimuuliza mtu ambaye hajafanikiwa. Mara nyingi anakuwa haamini kwamba inawezekana. Atakachokwambia ni ah…haiwezekani usipoteze muda wako.Achana na watu wa namna hiyo.

Kwa kumalizia kumbuka yafuatayo; mtu ambaye anatamani mafanikio zaidi ni wewe. Wewe pia ndio wa kuyafanyia kazi. Jitume zaidi.Usiogope kushindwa.Ni sehemu ya maisha.Kwa hiyo jaribu kufanikiwa zaidi.

No comments: