Tangazo

July 11, 2012

MGOMBEA YANGA AIVIMBIA TFF, AOMBA KURA

Sara Ramadhan akizungumza na wanahabari jijini Dar es salaam leo. Kushoto ni Ofisa wa Idara ya habari Maelezo, Mwirabi Sise.
********************
Na www.dinaismail.blogspot.com
MGOMBEA wa uenyekiti katika uchaguzi mdogo wa klabu ya Yanga uliopangwa kufanyika Jumapili jijiji Dar es Salaam, Sara Ramadhani amepinga kuenguliwa kwenye uchaguzi mdogo wa Klabu ya Yanga kulikofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF).

Sara, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga katika uongozi ulioingia madarakani Julai 18, 2010, amechujwa na kamati hiyo kwa hoja ya kutokidhi masharti ya kuomba uongozi kwa mujibu wa Ibara ya 10(4) na (5) ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.

Kwamba, Sara hakukidhi matakwa ya kanuni hiyo iliyoainishwa kwenye fomu namba 1, kwa kutojaza fomu na kutoambatanisha vithibitisho vya sifa za kugombea, uamuzi ambao umesisitizwa pia na TFF.

Akizungumza kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO,  jana, Sara alisema bado ni mgombea halali katika klabu hiyo kwani kitendo cha Shirikisho hilo kumzuia, ni kuingia mamlaka ya Kamati ya Uchaguzi ya Yanga chini ya Mwenyekiti wake Jaji John Mkwawa.

“Nimekuja kuwaeleza kuwa mimi bado ni mgombea wa nafasi ya uenyekiti katika klabu ya
Yanga, sitambui hatua ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuniengua, inajipa mamlaka yasiyo yake, inaingilia mambo ya klabu, ikitambua kuwa Yanga si ya soka pekee,” alisema Sarah.

Alisema inachofanya kamati ya uchaguzi ya TFF, ni kujipa mamlaka yasiyo yake kwa kuingilia mambo ya Yanga huku ikijua kuwa klabu hiyo ni ya michezo na sio ya soka pekee.

Aliionya kamati hiyo ya uchaguzi ya TFF kwamba iiache kamati ya uchaguzi ya Yanga iendeshe
zoezi hilo la uchaguzi kwa uhuru sio kuingilia na kupinga kile ambacho kimeridhiwa na kamati ya uchaguzi ya Yanga.

“Kamati ya uchaguzi ya TFF iache kuingilia mambo yasiyo yake, mimi sikutaka kupeleka vyeti kama walivyotaka kwa sababu wao hawahusiki na uchaguzi wa Yanga, uamuzi wa kamati ya uchaguzi ya Yanga ndio wa mwisho,” alisema.

Aidha, aliishutumu TFF kwa kuminya haki za kisheria kwa kupiga marufuku wadau wake kutokwenda mahakamani, nahodha wa Chelsea ya England, John Terry ameshitakiwa kwa tuhuma za kumfanyia vitendo vya kibaguzi Anthony Ferdinand wa Queens Park Rangers.

“Unajua TFF inatumia udhaifu wa Watanzania kutofuatilia mambo, masuala ya soka hayajazuiwa kwenda Mahakamani, Terry amefikishwa mahakamani tena kwa kosa lililofanyika ndani ya uwanja, mbona Fifa-(Shirikisho la soka la Kimataifa), limebaki kimya,” alihoji Sara.

Hata hivyo, alipoulizwa kuwa haoni kama jambo hilo lilipaswa kupingwa mapema kwa katiba za Klabu kutofuata mwongozo wa TFF, Caf na Fifa, alisema kila jambo lina wakati wake na ndio sasa.

“Hivi sisi tukisema tufuate matakwa ya kila mchezo itakuwaje, riadha watuambie hivi, TFF watake tufanye vile, ngumi nao watake hivi, tujiulize itakuwaje? sisi ni klabu ya michezo sio klabu ya soka,” alisema.

Wengine waliochujwa na kamati ya Uchaguzi ya TFF, ni Shaaban Katwila, Ahmed Waziri Gao na Ramadhani Kampira wakiungana na Ally Mayay, Abdallah Sharia, Jamal Kisongona Mohamed Mbaraka waliochujwa na Kamati ya uchaguzi ya Yanga.

No comments: