Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Jackson Mmbando (katikati), akizindua rasmi kampeni ya Imani katika elimu yenye lengo la kuchangisha pesa na kununua vitabu kwaajili ya shule tatu za watoto wenye mahitaji maalum za Dar es salaam ambazo ni Uhuru Mchanganyiko, Sinza Maalum pamoja na Buguruni shule ya Viziwi. Kulia ni Meneja Huduma kwa Jamii wa Airtel, Hawa Bayumi na (kushoto) ni Walter Bgoya Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Maendeleo ya Vitabu Tanzania (BAMVITA) ambao wanashirikiana na Airtel katika Kampeni hiyo.
*************************** KAMPUNI ya simu za mkononi ya Airtel inayotoa gharama nafuu zaidi Tanzania kwa kushirikiana na Baraza la Maendeleo ya Vitabu Tanzania BAMVITA wamezindua mradi maalumu wa kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum ili kupata nyenzo za kujifunzia ikiwemo vitabu na vifaa mbalimbali ili kuendeleza dhamira yao ya kuinua kiwango cha elimu nchini.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo Meneja Huduma za Jamii, Hawa Bayumi alisema “lengo la mradi wetu huu ni kutoa nafasi kwa jamii yetu kuweza kuchangia elimu ya msingi kwa watoto wenye mahitaji maalum kwa kuwanunulia Vitabu na nyenzo za walimu kufundishia. Airtel inatambua umuhimu wa Elimu kwakua tunatambua na kuamini Tanzania itajengwa na sisi wenyewe. Kwa kuanzia tumechagua shule tatu za jijini Dar es salaam ambazo ni Sinza Maalum, Uhuru Mchanganyiko na Buguruni viziwi ”.
“Ni matumaini yetu kuwa watanzania na wale wasio watanzania kwa ujumla wote watatuunga mkono ili tuweze kutimiza lengo hili la awali na kisha kuongeza shule za mikoani mara baada ya kukamilisha mahitaji haya katika shule hizi za Dar es salaam” alisema bi Bayumi.
Airtel Tanzania kwa kupitia ushirika na baraza la Vitabu Tanzania (BAMVITA), tutahakikisha kwamba michango yote itawafikia watoto hawa wenye mahitaji maalum kwa kuwanunulia vitabu na vifaa kama tulivyopanga kupitia kampeni hii kwa kushirikiana na walezi wa shule zote tatu”.
“Tunaamini kwamba kukamilika kwa Mradi huu kutasaidia sana kuongeza kiwango cha elimu kwa wototo wetu ambao ni watanzania wenzetu na kutoa mwangaza wa elimu kwao” alisema Bi Bayumi.
Akifafanua kuhusu muda wa kampeni hiyo, Meneja wa Uhusiano wa Airtel, Jackson Mmbando alisema kampeni hiyo ya Ushirika na Bamvita itaendeshwa kwa muda wa miezi mitatu na Watanzania wataweza kuchangia kwa kutuma neno “Vitabu” kwenda namba 15626 na kwakufanya hivyo kila SMS utakayotuma utakuwa umechangia shilingi 200 itakayoingizwa katika mradi huu”.
Vile vile wadau wengine wote wataweza kuchangia kwa kupitia huduma yetu ya Airtel Money ambapo jina la fumbo ni VITABU. Hivyo basi tunapenda kuwahamasisha watanzania wote kuchangia kiasi chochote watakachoweza.
Kwa upande wake mwakilishi kutoka BAMVITA, Walter Bgoya alisema “tunashukuru kwa Airtel pamoja na wadau wote waliojitolea ili tushirikiane katika mradi huu wa vitabu. Tumeweka malengo ya kuwafikia watoto wengi na shule nyingi zenye changamoto za vifaa vya kufindishia lakini tunategemea wadhamini na watanzania kutuunga mkono katika kuhakikisha watoto wetu wote nchi nzima wanapata elimu bora.”
Tunayomiradi mingi sana ikiwemo ile ya kuwajengea watoto tabia ya kusoma vitabu wakiwa wadogo, lengo la BAMVITA nikuhakikisha kuwa watanzania wanajenga tabia ya kusoma vitabu na kupata elimu na maarifa mbalimbali tofauti na ilivyo sasa ambapo tunachangamoto kubwa sana katika kujisomea vitabu.
Tunatoa shukurani zetu kwa Bw. Issa Michuzi wa Michuzi Media Group kwa kushirikiana nasi katika kampeni hii. Tunawakaribisha watanzania wote kuungana nasi na kuweza kuchangia kukuza kiwango cha elimu Tanzania.
Airtel Tanzania imekuwa mstari mbele katika kusaidia uboreshaji wa elimu na maisha ya jamii kwa kutoa misaada ya Vitabu kwa shule mbalimbali. Kwa mwaka huu shule zipatazo 93 za sekondari zitafaidika na mradi wa Airtel ujulikanao kama Airtel shule yetu, Shule hizi 93 zimepatikana kutokana na droo iliyochezeshwa mwezi huu ili kuweza kupata shule hizo.
Katika kuendeleza elimu Tanzania Airtel pia imeshamaliza ukarabati wa shule ya msingi ya Kiromo iliyopo nje kidogo ya jiji la DSM kando kando na barabara ya bagamoyo tangu kuanza ukarabati wa shule hiyo iliyoichagua mwaka jana 2011 huku mipango mingine ya mwaka huu ikiendelea ili kupata shule nyingine itakayofaidika kwa kujengwa na kukarabatiwa na mpango wa Airtel shule Yetu.
|
No comments:
Post a Comment