Tangazo

August 25, 2012

SMZ yamwaga sifa Ligi Kuu Z’bar kudhaminiwa na Grand Malt

Waziri asiye na Wizara Maalum SMZ,  Mh. Machano Othman Said (kushoto) akizungumza na viongozi wa vilabu vya Ligi Kuu ya Soka ya Grandmalt Zanzibar kwenye hafla ya kukabidhi vifaa kwa timu zote 12. Kulia ni Meneja Masoko wa Grandmalt, Fimbo Buttala.


Waziri asiye na Wizara Maalum SMZ,  Mh. Machano Othman Said (kushoto) akimkabidhi vifaa vya michezo kwaajili ya kutumia kwenye ligi kuu ya Grandmalt Zanzibar kwa Mwakilishi wa timu ya Jamhuri ya Pemba. Wa (pili kulia) ni Meneja Masoko wa Grandmalt, Fimbo Bittala na Makamu wa Rais wa ZFA, Ally Mohamed. Timu za Falcon na Jamhuri zitapambana kwenye mchezo wa Ngao ya Hisani jumamosi 01/09/2012 usiku katika uwanja wa amani. Picha zote kwa hisani ya Intellectuals Communications Limited
**************************
Na Mwandishi Wetu

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imeipongeza Grand Malt kwa kudhamini Ligi Kuu, ambapo kwa sasa inaamini itakuwa yenye ushindani mkubwa.
 
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa kwa timu 12 zinazoshiriki ligi hiyo iliyofanyika kwenye hoteli ya Zanzibar Ocean Viwe jana, Waziri Asiye na Wizara Maalum katika SMZ, Machano Othman Said, alisema huo ni mwanzo mzuri kwa soka la Zanzibar.
 
“Huu ni mwanzo mzuri kwa soka la Zanzibar na naamini tutafikia mafanikio yale tuliyokusudia. Nawashukuru Grand Malt kwa hili.
 
“Ila ninawaomba wadau wote wa ligi hii kuanzia Grand Malt, ZFA (Chama cha Soka Zanzibar) na klabu viweke wazi mikataba yote ili kusiwe na manung’uniko,” alisema.
 
Alivishauri klabu zote kufanya maandalizi mapema ili kuweza kuifanya ligi hiyo iwe ya ushindani mkubwa na kuvitaka kuhakikisha zina timu za vijana ili kuweza kupata timu bora kuanzia chini mpaka ngazi ya taifa.

Alisema ligi ilikosa msisimko katika miaka ya hivi karibuni kutokana na lkukosa mdhamini na ana uhakika kwa sasa kila kitu kitakuwa sawa.
 
Meneja Masoka wa Grand Malt, Fimbo Butallah naye alisema wameamua kudhamini ili kuleta changamoto na ushindani katika soka ya Zanzibar, kauli iliyoungwa mkono na Makamu wa Rais wa ZFA, Ally Mohamed. Timu hizo zilikabibidhiwa jezi, mipira, vizuia ugoko pamoja na vifaa vinginevyo.
 
Timu zinazoshiriki ligi hiyo ni pamoja na Super Falcon, Jamhuri , Chipukizi, Duma, Mundu, Mafunzo, KMKM, Mtende, Malindi, Bandari, Zimamoto na Chuoni.

No comments: