Tangazo

August 18, 2012

MABWEPANDE WATAKIWA KUISHI KWA AMANI NA UPENDO

Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Bw. Saidi Meck Sadiki (kulia) akimkabidhi  msaada wa vyakula mbalimbali mwenyekiti na mlezi wa waislam katika eneo la Mabwepande  Bw. Mohamed Basta kwa  ajlili ya sherehe ya EID EL FITR.

 Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Bw. Saidi Meck Sadiki akizungumza na waumini wa dini ya Kiislam walio katika eneo la Mabwepande nje kidogo ya jiji la Dar es salaam baada ya kuwakabidhi msaada wa vyakula mbalimbali  kwa ajili ya sherehe za  Eid. Picha na Aron Msigwa - MAELEZO
 ***********************
Na Aron Msigwa – MAELEZO.

Wakazi wa eneo la Mabwepande lililo nje kidogo ya jiji la Dar es salaam wametakiwa kuheshimu sheria za nchi  kwa kuishi kwa amani, upendo na mshikamano ili kuepuka migogoro inayoweza kutokea.

Akizungumza na wakazi wa eneo hilo leo mara baada ya kuwatembelea  kwa lengo la kutoa msaada wa vyakula kwa waumini wa dini ya Kiislam wanaojiandaa kusherehekea siku kuu ya EID EL FITR,  mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadiki amesema maendeleo ya kweli yanapatikana kwa kufanya kazi kwa bidii na kuheshimu sheria zilizowekwa.

 Amewaambia wakazi hao kuwa ushirikiano baina ya waumini wa madhehebu tofauti walioko katika eneo hilo katika masuala mbalimbali ndicho chanzo cha mafanikio yao na kamwe wasiruhusu tofauti za dini ziwagawe.

Amesema serikali inaendelea kutatua changamoto na vikwazo mbalimbali vinavyowakabili wakazi hao waliopelekwa katika eneo hilo kutokana na athari za mafuriko yaliyolikumba jiji la Dar es salaam mwishoni mwa mwaka 2011.

Akifafanua kuhusu mpangiliao wa makazi katika eneo hilo amesema kuwa serikali imeshashughulikia suala la ramani kwa ajili ya kuonyesha mipaka ya eneo hilo sambamba na kuonyesha maeneo ya ujenzi wa nyumba za kuabudia kwa waumini wa madhehebu mbalimbali na utengaji wa maeneo ya makaburi.

“Napenda kuwafahamisha na kuwahakikishia kuwa kuwa tayari serikali imekwishashughulikia suala la ramani katika eneo hili, kwa upande wenu ninyi kama waumini wa dini ya kiislam eneo hilo litamilikiwa na Baraza Kuu la Waislam Tanzania  (BAKWATA) ambalo linatambuliwa na serikali ili kuondoa migongano inayoweza kutokea”

Nao viongozi wa dini ya kiislam katika eneo hilo la Mabwepande wakiongozwa na mwenyekiti wao na mlezi wa waislam Bw. Mohamed Basta wamemshukuru mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam kwa msaada alioutoa kwa wakazi hao hasa katika kipindi hiki kuelekea siku kuu ya Eid.

Katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Bw. Saidi Meck Sadiki ametoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 26 mwaka huu.

 Amewataka wakazi hao kutoa  ushirikiano kwa kuwapatia taarifa sahihi za kaya kwa makarani wa Sensa watakaopita katika makazi yao.

“Nawaombeni sana mtoe ushirikiano katika zoezi la Sensa litakalofanyika tarehe 26 mwezi huu, nawaomba msiwe na hofu kwa sababu zoezi hili litadumu kwa muda wa wiki nzima, halitaathiri shughuli zenu za kila siku hivyo kila mwananchi atapata fursa ya kuhesabiwa” amesema.

Aidha amewataka waumini hao kuvipuuza vikundi vya watu na baadhi ya viongozi wa dini hiyo wanaowahamasiha waumini wao kutoshiriki katika zoezi la Sensa huku akifafanua kuwa serikali itawachukulia hatua watakaokwamisha  zoezi kwani watakua wanavunja sheria za nchi kutokana na zoezi  hilo  kuendeshwa kwa mujibu wa sheria na 1 ya mwaka 2002

No comments: