Tangazo

August 28, 2012

MKUTANO WA MABADILIKO YA TABIANCHI BANGKOK: KUNDI LA G77 NA CHINA WAKUTANA

Washiriki kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira katika mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabia nchi mjini Bangkok. Picha na Evelyn Mkokoi.
 
*******************************
EVELYN MKOKOI, BANGKOK

Kundi la nchi za 77 na China limekutana leo kwa mara ya kwanza katika mkutano wa kimataifa wa maandalizi wa mabadiliko ya tabianchi unaoendelea nchini Thailand mjini Bangkok.

Mkutano huo umeanza kwa dakika chache za kuwakumbukuka viongozi wa nchi za Afrika waliopoteza maisha yako hivi karibuni, Rais wa Ghana marehemu John Evans Atta Mill na Waziri Mkuu wa Ethiopia marehemu Meles Zanawi.

Agenda zilizojadiliwa na kundi hilo ni kuhusu ripoti ya mkutano wa Bonn ya Kuhimili na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, masuala ya fedha, teknolijia pamoja na kujenga uwezo.

Baadhi ya washiriki wa kundi hilo walitoa michango yao katika mkutano huo ambapo Kiongozi wa kikundi kinachoratibu masuala ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi,  alifahamisha mkutano kuwa suala la kuhimili na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi linahusisha dunia nzima na siyo kundi la nchi 77 na China pekee kwa hiyo hakuna haja ya kugombana na kutofautiana juu ya hilo na kuna kila sababu ya kuhakikisha kuwa  kamati maalum ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi kuanza kazi mara moja.

Kwa upande wa mshiriki kutoka nchi ya Nicaragua, alisema kuwa suala la kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa nchi yao ni kipaumbele kutokana na sababu hiyo basi, kundi hili lina kila sababu ya kulipa kipaumbele suala la kuhimili mabadiliko ya tabianchi hasa katika Nyanja ya kujengea uwezo nchi zinazoendelea.

Mshiriki kutoka nchini Swaziland ambaye ni Mwenyekiti wa Kundi la Afrika , akizungumza kwa niaba ya Kundi la Afrika aliongeza kuwa, Afrika inakubalina  kuwa suala la kuhimili mabadiliko ta tabianchi ni muhimu sana kwa kundi zima la G77 na China ila changamoto  kubwa ni suala la upatikanaji wa fedha kwa ajii ya kutekeleza mipango madhubuti iliyoandaliwa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa nchi nyingi za Afrika hasa zile zilizo masikini sana (LDC), na kutaka nchi zilizoendelea kutoa fedha kama ilivyobainisha katika Mkataba  ili  kukabiliana na tatizo hilo.

 Aidha,  alisisitiza kuwa, kwa upande wa hasara na madhara yatokanayo na athari za mabadiliko ya tabianchi bado ni tatizo kubwa na jipya na kuna kila sababu ya kukuza uelewa hasa katika  eneo la kuongezeka kwa jagwa na kina cha bahari.

Kwa upande wa kundi la Nchi masikini duniani, mwakilishi wa kundi hili kwa niaba ya Mwenyekiti , akichangia zaidi katika suala la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, alisema ni kipaumbele kwa nchi 48 wanachama na wapo tayari kushirikiana  na nchi nyingine katika majadiliano yanayoendelea ili kuweza kufikia malengo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ingawa nchi masikini duniani ndio  waathirika zaidi wa suala mabadiliko ya tabianchi  kutokana na uwezo mdogo wa kuhimili.

Mkutano huu unaondelea mjini Bangkok ni muendelezo wa mkutano uliofanyika Mjini Bonn mwezi Mei ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mkutano wa dunia wa mabadiliko ya tabianchi unaotegemea kufanyika mjini Doha nchini Qatar mwezi Disemba mwaka huu.

No comments: