Tangazo

August 18, 2012

NAPE AWAASA WAISLAM WAADILIFU KUIOMBEA NCHI IDUMU KATIKA AMANI

Nape Nnauye
- Ataka wanaoomba machafuko waombewe dua ya kuwaponya

NA MWANDISHI WETU, MOROGORO

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewaasa Waislam kuutumia uadilifu wao kuiombea Tanzania iendelee kuwa nchi ya  amani na utulivu.

Kimesema amani ikishamiri hapa nchini, Waislam kama Watanzania wengine wataunufaika nayo kwa kuweza kufanya mipango yao ya kuabudu Mungu na ya maisha yao ya kila siku bila mashaka tofauti na amani ikitetereka.

Hayo yalisemwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye wakati akizungumza na mabalozi wa nyumba kumi mkoani Morogoro, baada ya kuwafuturisha jana, futari aliyoandaa kwenye ukumbi wa shule ya  Sekondari Forest mjini hapa.

"Kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi, tumeona kwamba faradhi hii ya Funga ya Mwezi wa Ramadhani mnayotekeleza, pamoja na kuwa ni muhimu sana kwenu kama Waislam lakini pia ni muhimu sana kwa taifa letu kwa sababu tunaamini uchamungu huzaa uadilifu na uadilifu ni chanzo pia cha kudumisha amani na utulivu tulio nao hapa nchini, hivyo kwa niaba ya Chama nikaona ni vizuri tukafuru pamoja jioni ya leo", alisema Nape.

"Nachowaasa Waislam mliojumuka hapa na wale ambao hatukubahatika kuwa nao kwenye futari hii, endeleeni kuutumia uadilifu wetu mliouithibitisha mbele za Mungu kwa funga hii, kuiombea nchi yetu iendelee kuwa na amani na utulivu, maana amani ikitoweka huathiri kila kitu ikiwemo ibada", alisema Nape.

Nape aliwaomba waislam katika dua zao pia kuwaombea pepo wabaya wawatoke, watu ambao alisema wamekuwa kila kukicha wanatamani amani iliyopo nchini itoweke kutokana na uchu wa madaraka.

Mapema akimkaribisha kuzungumza kwenye futru, Kaimu Katibu wa CCM mkoa wa Morogoro, Sixtus Mapunda alikishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa uamuzi wake wa kuamua kuwafurutisha wajumbe wa nyumba kumi wa mkoa wa Morogoro akieleza kwamba tukio hilo limeongeza mshikamano kwa wana-CCM na wananchi kwa jumla mkoani humo.

Alisema, zaidi ya wajumbe 450 kutoka wilaya za mkoa huo, walifanikiwa kuhudhuria kwenye futari hiyo, na kukitaka Chama kujijengea uitaratibu huo hata kwa mikoa mingine.

"Uzuri wa futru hii ni kwamba  mbali na kwamba ni ibada kwa waislam, lakini pia inatuweka pamoja waislam na wasiokuwa waislam kwa kuwa watu wamealikwa hapa bila kutazama dini zao au kuchagua waliofunga na ambao hawakufunga kama Mzee wangu pale mkuu wa mkoa wa zamani wa mkoa huu (Morogoro) Steven Mshishanga", alisema, Sixtus.

Mbali na Mashishanga futari hiyo ilihudhuriwa pia na  Mkuu wa mkoa wa Morogoro,  Joel Bendera, Mwanasiasa wa siku nyingi mkoani Morogoro ambaye pia amewahi kuwa Mbunge, Semindu Pawa na viongozi mbali mbali wa CCM mkoani  humo.

No comments: