Tangazo

September 27, 2012

Ushirikiano wa pamoja unahitajika ili kumuinua Mwanamke na Mtoto wa kike

Mama Salma Kikwete
Na Anna Nkinda – Maelezo, New York

27/09/2012 Mshikamano  wa pamoja unahitajika baina ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea ili kuhakikisha kuwa mtoto wa kike ambaye hajapata nafasi ya kwenda shule anapata elimu, kuwainua wanawake kiuchumi na kupunguza vifo vya kinamama wajawazito na watoto vinavyotokana na tatizo la uzazi na  ugonjwa wa kansa.

Hayo yamesemwa  jana na Mke wa rais Mama Salma Kikwete wakati akichangia mada  kwenye mkutano wa The RAND African First Ladies Initiative uliofanyika makao Makuu ya Taasisi ya Ford mjini New York nchini Marekani.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa taasisi mbalimbali za Kiserikali na zisizo za kiserikali zinafanya jitihada kubwa ya kuhakikisha kuwa zinawasaidia wanawake wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za maisha  tatizo  lililopo ni upungufu wa rasilimai fedha za kuweza kukabiliana  na changamoto hizo  hivyo basi ushirikiano wa pamoja unahitajika ili kuweza kufanikisha malengo hayo.

Aliendelea kusema kuwa watoto wa kike wakipata elimu ya kutosha watakuwa na silaha muhimu katika maisha yao ya kuweza  kupambana na matatizo mbalimbali  ikiwa ni pamoja na maradhi, ujinga na umaskini  kwani elimu ni nguzo muhimu katika maendeleo ya taifa lolote Duniani bila ya watu kuwa na  na elimu nchi haiwezi kuendelea.

“Ukimuelimisha mtoto hasa mtoto wa kike  ambaye amekosa nafasi ya kupata elimu ni faida kwa mtoto, Taifa  na Dunia kwa ujumla kwani hivi sasa tumejionea wanawake wengi wakishika nafasi za juu za uongozi kitaifa na Dunia pia wameweza kujikwamua  kiuchumi tofauti na miaka ya nyuma”, alisema Mama Kikwete.

Mwenyekiti huyo wa Taasisi ya WAMA  alisema  kuwa   nchini Tanzania watoto wengi wa kike ambao ni yatima na wanaishi  katika mazingira hatarishi wameshindwa kupata elimu sawa na watoto wengine hivyo basi aliamua kuanzisha taasisi hiyo   ili aweze kuwasaidia watoto hao, kuwainua wanawake kiuchumi na kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto na wanaougua ugonjwa wa kansa  kwa kutoa elimu kwa wananchi na vifaa tiba katika vituo vya afya na Hospitali .

Mkutano huo wa siku moja ulihudhuriwa na wake wa marais na wakuu wa Serikali wa Afrika, mke wa rais mstaafu wa  Marekani Laura Bush na mke wa waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Cherie Blair, pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali na mashirika binafsi kutoka nchi wa Afrika na Marekani.

Katika mkutano huo  mambo mbalimbali yalijadiliwa ikiwa ni pamoja na kuangalia   jinsi gani wake wa maraisi na wakuu wa Serikali wanaweza kuleta mabadiliko katika nchi zao katika kuimarisha  afya ya mwanamke, kuhakikisha kuwa mtoto wa kike anapata elimu na na kuwainua wanawake kiuchumi pamoja na changamoto wanazoweza kukabiliana nazo.

No comments: