Tangazo

October 22, 2012

SHIGELA: RUSHWA, UBABE HAVITAPENYA KWENYE UCHAGUZI WA UVCCM

NA BASHIR NKOROMO, DODOMA

WAKATI Uchaguzi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) umemalizika juzi, huku ukidaiwa kugubikwa na ubabe na rushwa, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) umejitapa kwamba, utahakikisha vitendo hivyo havitokei katika uchaguzi wake mkuu utakaofanyika kesho mjini Dodoma.

UVCCM imeapa kwamba mgombea au hata mpambe atakayebainika kujihusisha na kampeni zilizo nje ya utaratibu na kanuni za UVCCM au kujihusisha na vitendo vya rushwa atashughulikiwa mara moja ikiwemo kuchukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM,Martine Shigela alisema, wameweka mtandao mpana wa kutosha kukabiliana na aina yoyote ya ukiukwaji wa tararibu, kanuni na sheria za uchaguzi wa UVCCM.

"Sisi hatuwezi kuzungumzia hayo mnayosema, yamejitokeza kwenye uchaguzi wa UWT,lakini kwa upande wetu tunawahakikishieni kwamba tutamkabili vilivyo tena bila mzaha,mgombea au mpambe yeyote atakayejaribu  kutumia mbinu chafu za kampeni ikiwemo kutoa rushwa", alisema Shigela.

Shigela alisema, taratibu za mkutano mkuu utakaoambatana na uchaguzi huo, zimekamilika na utafanyika kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere, uliopo Chuo Cha Mipango ambako ndiko ulikofanyika pia ule wa UWT.

Alisema, mkutano unaanza kesho, Oktoba 23, na utafunguliwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete."Hadi sasa maandalizi yamekamilika, leo Oktoba 22, tunakazi kupokea wageni mbalimbali kutoka maeneo kadhaa wakiwemo wa kutoka nchi za nje amabao watahudhuria mkutano wetu. alisema Shigela.

Katika nafasi ya Mwenyekiti wanachuana wagombea watatu, Lulu Mushamu Abdallah,  Sadifu Juma Khamis na Rashid Simai Msaraka wakati katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni Ally Salum Hapi, Paul Christian Makonda Mboni Mohamed Mhita.

Nafasi zingine ni, Halmashauri Kuu ya Taifa Viti sita (Bara) wagombea 40, Viti Vinne (Zanzibar) wagombea 22, Nafasi ya Baraza Kuu la Vijana Taifa Viti vitano Bara wagombea 39 na viti vitano Zanzibar wagombea 14,  Uwakilishi Wazazi Taifa na Jumuia ya Wanawake Tanzania (UWT) wagombea 16 kila nafasi.

No comments: