Tangazo

February 18, 2013

Changamkieni punguzo la gharama za umeme: Mama Salma Kikwete

Mama Salma Kikwete
Na Anna Nkinda – Maelezo , Lindi

18/2/2013 Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) taifa (NEC) Mama Salma Kikwete amewataka wakazi wa kijiji cha Kitumbikwela  na Mingoyo wilayani Lindi mjini kuchangamkia punguzo la kuingiza umeme katika nyumba zao na kuepukana na gharama za mafuta ya taa ambazo zinapanda mara kwa mara.

Mama  Kikwete ambaye pia ni Mke wa Rais aliyasema hayo jana wakati akiongea kwa nyakati tofauti na wananchi hao katika ziara yake ya kichama ya  kuwashukuru wanachama wa CCM kwa kumchagua kuwa mjumbe wa NEC kutoka wilaya ya Lindi mjini.

Alisema kuwa miaka ya nyuma gharama za kuweka umeme majumbani zilikuwa kubwa na kufikia  shilingi milioni mbili na nusu lakini hivi sasa zimeshuka hadi shilingi laki nne na arobaini elfu fedha ambazo hata mwananchi wa kawaida anaweza akajiwekea  akiba na kuzipata.

Mama Kikwete alisema, “Kuweka umeme katika  nyumba yako si utajiri kwani gharama za uwekaji zimepungua ukilinganisha na miaka ya nyuma  jambo la muhimu ni nyumba iwe imeezekwa vizuri na kuwekwa nyaya za kuingiza umeme ndani ya nyumba (wire ring).

Hata kama hauna hela unaweza kuweka akiba yako kidogokidogo kila mwaka pale unapouza  mazao na baada ya miaka michache utakuwa umepata fedha yote, nawasihi wananchi wenzangu hakikisheni kuwa umeme utakapofika kijijini mnautumia kwani wenzenu wanatamani kuwa na umeme lakini bado haujawafikia”.

Aidha Mama Kikwete pia aliwashimiza wanawake wajitokeze kwa wingi katika miradi ya kukopa mbuzi lipa mbuzi na kopa ng’ombe lipa ng’ombe kwani wakipata fedha kidogo pamoja na za waume zao pato la familia litaongezeka  na hivyo kujikwamua kimaendeleo.

Akiwa katika kijiji cha Mingoyo aliwasihi  wazazi kuwalea vijana wao katika maadili mema na kuwaelekeza pale ambapo wanapokosea kwani utandawazi unawaharibu vijana wengi na kujikuta wanajiingiza  katika matendo yasiyofaa ikiwa ni pamoja na utumiaji wa madawa ya kulevya na uvutaji wa bangi.

“Baadhi ya vijana wanaona fahari kuwa na wapenzi wengi jambo ambalo ni la hatari kwa kuwa unajiandalia mazingira ya kupata kirahisi maambukizi ya virusi vya Ukimwi na takwimu zinaonyesha kuwa kwa kila watanzania mia moja sita wanamaambukizi. Muache tabia hiyo  na kufuata vitabu vitakatifu vya dini vinavyosema kwani ugonjwa huu hauna dawa zaidi ya dawa za kupunguza makali tu”, alisema Mjumbe huyo wa NEC .

Kwa upande wake diwani wa kata ya Mingoyo Jamridi Mandowa alisema kuwa tangu Serikali ilipotangaza kuanza kwa mradi wa kusambaza umeme vijijini, kupunguza gharama za ufungaji wa umeme majumbani na kusogeza muda wa kupokea maombi wananchi wamejitokeza kwa wingi kutuma maombi lakini kasi ya usambazaji ni ndogo hawaelewi tatizo ni kitu gani.

Naye Diwani wa Kata ya Msinjahili ambaye ni Meya wa Lindi Mjini Frank Magali alisema kuwa kata yake inamradi wa kopa ng’ombe lipa ng’ombe na kopa mbuzi lipa mbuzi ambapo kwa upande wa ng’ombe walipata majike nane na dume mmoja na kuwakopesha wananchi ambao kwa kiasi kikubwa wamenufaika na mradi huo.

Mama Kikwete alifanya mikutano ya hadhara na kujibu maswali ya  wananchi  wa kata za Msinjahili, Mingoyo na Mitandi na kuwakabidhi kadi  wanachama  wapya wa CCM  37, Umoja wa vijana 37, Umoja wa Wanawake  92 na Jumuia ya Wazazi  73.

No comments: