Tangazo

April 22, 2013

NSSF NA GYMKHANA NGUVU SAWA

 Kikosi Kamili cha timu ya soka ya Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kikiwa katika picha ya pamoja kabla ya mcherzo wa na Gymkhana jijini Dar es Salaam. Timu hizo zilitoka sare ya mabao 3-3
Kikosi cha timu ya soka ya Gymkhana.
Mshambuliaji wa timu ya soka ya NSSF, Patrick Gandye akiwania mpira huku akizongwa na beki wa timu ya  Gymkhana,  Hayssam Srour.
 Clementi Sanga akiambaa na mpira huku akifuatiliwa kwa karibu na mchezaji wa NSSF, Kitwana Kidatu.
 Baadhi ya wafanyakazi wa NSSF wakifuatilia mchezo huo.
Kiungo wa timu ya Gymkhana, Clement Sanga ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Yanga akitafuta mbinu za kumtoka beki wa NSSF, Saleh Biboze wakati wa mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam.


DAR ES SALAAM,Tanzania

TIMU ya soka ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), juzi ilipigana kiume kutoka nyuma kwa mabao 3-1 na kuambulia sare ya mabao 3-3 na Gymkhana FC, katika mechi kali ya kirafiki iliyopigwa kwenye Uwanja wa Gymkhana, jijini Dar es Salaam.

Ikicheza kwenye dimba la nyumbani, Gymkhana FC ilimaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza ikiwa mbele kwa mabao 3-1 yaliyowekwa nyavuni na mshambulia Radwan Kerdi aliyefunga mara mbili na moja likitiwa kimiani na Erard Mutalemwa ‘Drogba.’

Bao la NSSF katika dakika 45 za kwanza lilifungwa kwa mkwaju wa penati na Nassor M. Nassor, baada ya beki Linus Bwegoge aliyepanda kusaidia mashambuliazi kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari na mwamuzi kuamuru adhabu hiyo.

Kipindi cha pili, NSSF walicharuka zaidi hasa baada ya mabadiliko yaliyofanywa na kocha mchezaji Khalid Jambia na kufanikiwa kusawazisha mabao hayo kupitia nyota wake Ahmed Hamisi ‘Kibela’ na Ali Chuo, hivyo kupata sare hiyo ya kuvutia ya 3-3.

Kocha wa NSSF, Khalid Jambia alikiri kufurahishwa na upiganaji wa nyota wake, uliowezesha kupata sare hiyo, iliyokuja baada ya mechi ya kwanza baina ya timu hizo kuvunjika wakiwa hawajafungana, baada ya taa za uwanja huo kuzimika.

Gymkhana FC itabidi ijilaumu kwa kutoibuka na ushindi katika mechi hiyo iliyokuwa na nia ya kuimarisha mahusiano mema baina ya Gymkhana - klabu inayohusisha michezo mbalimbali na NSSF, baada ya kupoteza nafasi kadhaa kupitia nyota wake.

Akizungumzia mechi hiyo mchezaji wa Gymkhana, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, alisema amekunwa na ushindani uliooneshwa, ingawa timu yake ilikuwa na nafasi ya kuibuka na ushindi, kabla ya kuponzwa na kuridhika kwao na uongozi wa 3-1.

“Nimeridhishwa na ushindani na matokeo. Si kwamba hatukutaka kushinda, ila mabadiliko ya kikosi chetu yalichangia, ingawa tumefanikisha lengo kuu la kuboresha mahusiano baina ya Gymkhana na NSSF na kuchezesha kila mchezaji wa kikosi chetu,” alisema Sanga.

No comments: