Tangazo

April 15, 2013

Safari Lager yafanya kweli Afrika

Meneja wa Chapa ya Safari Lager, Oscar Shelukindo akionyesha vikombe vya ushindi.
Na Mwandishi Wetu

TANZANIA imeingia katika ramani nyingine barani Afrika, baada ya bia ya Safari Lager inayotengenezwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kutwaa Tuzo ya Bia Bora Afrika.

Kutokana na hilo, kwa sasa Safari Lager ndiyo inayotambulika kama bia bora kuliko zote zinazozalishwa na kutengenezwa ndani ya bara la Afrika.

Ushindi wa Safari Lager umekuja kufuatia zoezi lililoendeshwa na Taasisi ya Utengenezaji wa Bia na Vileo (IBD), ambapo mashindano hayo ya kuangalia na kupima ubora wa bia yalifanyika, yakihusisha zaidi ya bia 50 kutoka makampuni maarufu barani humu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa Bia ya Safari Lager, Oscar Shelukindo alisema ushindi huo si wa TBL pekee bali ni wa Watanzania wote.

“Huu ni ushindi mkubwa sana na wa kujivunia sio tu kwa bia hii ya Safari Lager au TBL bali kwa taifa zima kwa ujumla, kwani umeleta heshima na kuonesha Watanzania wanaweza kutengeneza bidhaa bora na zenye kukidhi viwango vya kimataifa.

“Bia hii ya Safari Lager imeweza kuzishinda bia zote za Afrika na kukamata namba moja katika ubora, hii inathibitishwa na ukweli kuwa hata hapa nyumbani, ndiyo inayoongoza kwa mauzo kuliko bia nyingine yoyote tangu ilipozinduliwa mwaka 1977,” alisema.

Shelukindo alisema katika kuhakikisha Watanzania wote wanafurahia ushindi huo, watahakikisha wanafikisha ushindi huo bungeni hapo keshokutwa.

“Tunataka wabunge watambue kile ambacho Watanzania wanapaswa kujivunia nacho na tutaanza ziara ya kulizungusha kombe letu katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

“Ujumbe mkuu katika ziara hii utakuwa ni kuutangaza ushindi huu mkubwa wa bia hii inayotengenezwa na Watanzania. Lakini pia tutahamasisha watu wawe na uzalendo kwa kuziamini na kutumia bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.

“Tunaamini kuwa ziara hii itaongeza hamasa kwa watanzania kupenda bidhaa za nyumbani na hatimaye kusaidia kukuza uchumi wetu,” alisema.

Katika kusaka bia bora, IBD ilikusanya wataalamu huru kutoka katika mabara matatu tofauti ili kuonja bia na kutoa uamuzi usio na upendeleo wowote.

Katika mashindano haya bia hizi zilipimwa katika makundi tofauti kama vile, zinazotengenezwa kwa kutumia malighafi zinazopatikana sehemu inapotengenezwa bia yenyewe, bia zenye kiwango cha kilevi cha chini ya asilimia 5 na pia kundi la bia zenye kiwango cha kilevi cha zaidi ya silimia 5.

Tuzo ya Bia Bora ambayo ni ya bingwa wa jumla wa bia zote zilizoshiriki ilinyakuliwa na Safari Lager. IBD ilitoa taarifa rasmi kutoka Accra, Ghana kuhusu ushindi wa bia hiyo.

Bia ya Safari Lager pia imeshashinda jumla ya tuzo tano za Dhahabu katika mashindano maarufu Duniani yajulikanayo kama ‘Monde Selection. 

No comments: