Tangazo

May 21, 2013

SEHEMU YA HOTUBA YA MH. SUGU...MGOGORO WA JIDE NDANI

7.2 Harakati za kudai haki za wasanii.
Mheshimiwa Spika, sanaa imeendelea kufanywa mtaji wa biashara na watu wachache ambao wanatumia nguvu waliyo nayo katika jamii na uwezo wao wa kifedha katika kukandamiza maslahi ya wasanii hapa nchini. Katika harakati za kutafuta haki za wasanii hapa nchini, mimi binafsi pamoja na wasanii wengine wachache, tulianzisha harakati za kudai haki kwa kupitia programu maarufu iliyojulikana kama 'Anti Virus' chini ya 'Vinega' ikiwa na lengo na juhudi za kudai haki za wasanii dhidi ya ukandamizaji unaofanywa na wajanja wachache kwenye muziki, ambao wametumia nafasi kama njia ya kutumia mitaji yao ya fedha kuwaendesha wasanii jinsi wanavyotaka wao.

Mheshimiwa Spika, Kama ilivyo kawaida, wasanii wengi walidharau jitihada zetu na kutotuunga mkono. Leo hii katika tasnia ya muziki, kuna mgogoro mkubwa uliofuka moto kati ya msanii maarufu Lady Jaydee dhidi ya wamiliki wa radio ya Clouds FM hatua iliyosababisha nyimbo za wanamuziki wa kizazi kipya maarufu kama 'Bongo Flavour' kutopigwa kwa siku moja katika kituo hicho. Sasa, ukiangalia kilio cha Lady Jaydee ni kilio kilekile kilichopelekea VINEGA kuingia vitani.

Mheshimiwa Spika, kama msemaji mkuu wa kambi ya upinzani bungeni, na mwenye dhamana na uchungu na tasnia ya sanaa nchini, niweke wazi kwa umma wa watanzania kuwa, tumefikia hapa tulipo si kwa kuwa na sheria kandamizi tu bali pia kwa kukosekana kwa umoja wa wasanii nchini. Wakati tukiwa na juhudi za kutetea maslahi ya watanzania kupitia Anti Virus, ni wasanii wachache ambao walituunga mkono na wengi wao wakibeza jitihada zetu, wakiwemo hawa ambao leo wanalalamika kuwa wananyonywa haki zao. Wengine walifikia hatua ya kusema kuwa tumepewa fedha ili kuzima harakati tulizozianzisha.

Mheshimiwa Spika, Umoja wa wasanii hasa wa muziki wa kizazi kipya nchini, unasimamiwa na chombo halali kinachojulikana TUMA-‘Tanzania Urban Music Association’, lakini kutokana na ujanja wa watu wachache, waliudhoofisha umoja huu kwa kuanzisha kampuni iliyosajiliwa kama TFU- ‘Tanzania Flavour Unit’ iliyowalaghai wasanii kuwa ni muungano wa wanamuziki wa Bongo Fleva na kuhodhi majukumu ya TUMA ambacho ni chama halali cha kusimamia wanamuziki wa Bongo Fleva. Mpaka tunapoongea leo hii, hata Studio iliyotolewa na Mheshimiwa Raisi, bado ipo katika mikono ya TFU pamoja na Serikali kuamuru irudishwe katika mikono ya Serikali ili ikabidhiwe kwa wasanii wote chini ya chama halali cha TUMA. Sasa tunataka wasanii wote nchini waache uoga na unafiki na wajiunge na vyama vyao halali ili viwatete haki zao.

Mheshimiwa Spika,Kumekuwa na upotoshaji mkubwa wa utetezi wa haki za wasanii kwa kuwa wanaotuhumiwa kunyonya haki za wasanii wameweza kutajirika na kuneemeka kwa kupitia jasho na mgongo wa wasanii. Hawa hawa wanaotuhumiwa kuhujumu wasanii ndio wanatumia nafasi yao kuupotosha ukweli wa tuhuma dhidi yao. Wanatumia fedha na rasilimali walizo nazo katika kunyanyasa wasanii, kuwakandamiza, kuwapokonya haki zao na kuwadhalilisha kuwa bila wao, wasanii wasingekua kitu.

Mheshimiwa Spika, Leo hii wasanii wanaishi kwenye hali ngumu, umasikini mkubwa lakini bado wanatolewa maneno ya kashfa na dharau na Serikali imeendelea kukaa kimya. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka Serikali kuacha siasa kwenye kutatua migogoro ya taifa hili. Siasa zimetumika sana katika kuzima jitihada za wanyonge kwenye taifa hili, leo hii wananchi hawana imani na Serikali kwa kuwa imeonesha wazi imeshindwa! Kushindwa kwa Serikali katika kutatua migogoro ya wasanii kwa kutotekeleza makubaliano mbalimbali yanayoafikiwa kati yake na wasanii, yameshusha hadhi yake kwa wasanii. Swali kubwa kwa Serikali sikivu ya CCM, Je mnasubiri migogoro mingapi ili mjue kuwa wasanii hawatendewi haki? Je mnasubiri vikao vingapi vya upatanishi na usuluhihishi ili mjue kuna tatizo? Ama mnataka wasanii wagombane, wapigane, wauane ili mjue kuwa kuna tatizo?

Mheshimiwa Spika,Leo hii, Serikali bila ya kukaa na wadau wa muziki wa dansi, taarabu, bongo fleva, hip hop, mnanda na mahadhi mengine na kuwasikiliza kwa makini wamejikuta wanajihusisha na mambo ambayo hawajui. Watendaji wa Serikali wameendelea kuwaingiza mkenge viongozi wa Serikali katika masuala ya sanaa nchini. Hivi karibuni,hapa Dodoma, bila ya kuwa na taarifa muhimu juu ya unyonyaji wa haki za wasanii, waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda, alishiriki katika tamasha la kudai haki za wasanii ambalo liliandaliwa na baadhi ya watu ambao kwa muda mrefu wamekua wakituhumiwa kuwa ni wanyonyaji wa kazi za wasanii.

Kiongozi mkuu wa Serikali, unashiriki katika kupiga mihuri na kuhalalisha mikakati ya kimafia ya kuua umoja wa wasanii bila ya kuwa na taarifa sahihi. Je, waziri mkuu ana taarifa kuwa walioandaa tamasha la kudai haki za wasanii ndio walalamikiwa namba moja nchini dhidi ya haki za wasanii hasa wa muziki? Tuinataka Serikali na wanasiasa wote kuacha kutumia wasanii kwa faida zao binafsi bali wasaidie kutatua matatizo halisi ya wasanii ili waondokane na umasikini.

No comments: